WAZIRI DKT MABULA ATAKA UWAJIBAKI KWA MAKAMISHNA WA ARDHI KUFIKIA MALENGO YA WIZARA

Na Ahmed Mamoud Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewataka Makamishna Wasaidizi wa Ardhi wa mikoa nchini kuwajibika na kutumia wajibu wao katika kutekeleza mikakati ya Wizara kufikia malengo. Aidha, amewataka Makamishna hao kuwapangia majukumu kwa malengo maafisa walio chini yao na kufuatilia kazi wanazowapa mara kwa mara. Dkt Mabula amesema, hayo tarehe 25 Februari 2022 wakati akifungua kikao kazi cha Menejiment na Makamishna wa Ardhi Wasaidizi wa mikoa kilichofanyika ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Arusha. ‘’Yapo malamiko ya lugha zisizofaa kwa wateja, hii haikubaliki fuatilieni hili na kulikemea vikali na kuzingatia misingi na kanuni za utumishi wa umma katika majukumu yenu ya kila siku ’’ alisema Dkt Mabula. Aidha, aliwataka katika utekelezaji mpango mkakati wa wizara wanazingatia vipaumbele vya serikali hususan maelekezo ya mhe. Rais Samia Suluhu Hassan na ukusanyaji wa maduhuli ya serikali kupitia kodi ya pango la ardhi. Akigeukia suala la makusanyo ya kodi ya pango la ardhi, Waziri wa Ardhi aliwataka Makamishna wa ardhi Wasaidizi wa mikoa kuwa wabunifu katika njia za kukusanya mapato. ‘’Sula la mtandao kutopataikana muda mwingi linaonekana kuwa kikwazo katika ukusanyaji maduhuli, lifanyieni kazi’’ alisema Dkt Mabula. Waziri Dkt Mabula pia alihimiza kuongezwa kwa kasi ya umilikishaji ardhi na kuwataka Makamishna hao na wakuu wa idara katika wizara kuweka malengo kwa kila ofisa mwenye taaluma ya ardhi kuandaa hati. Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Allan Kijazi alisema baada ya kuteuliwa alifanya ziara katika baadhi ya mikoa na kukutana na baadhi ya changamoto alizozitaja kuwa ni pamoja na kutofikiwa malengo ya ukusanyaji kodi ya ardhi pamoja na baadhi ya halmashauri kutohudumia idara za ardhi kwa madai ya idara hizo kuhamishiwa wizarani. ‘’Nimeanza kuchukua hatua ili kutatua changamoto hizo ambapo tayari nimetoa maagizo mbalimbali kwenye mikoa na menejimenti ya wizara na ni matarajio kikao kazi kutaibua suluhisho la changamoto hizo’’ alisema Dkt Allan Kijazi. Kwa mujibu wa Dkt Kijazi, Wizara ya Ardhi imekuwa ikinyooshewa vidole na wananchi kwa masuala ya ukiukwaji wa haki za wananchi na kuchafua taswira ya Wizara na kutaka watendaji wa sekta ya ardhi kujitafakari na kujisahihisha kwa kutimiza wajibu ili kuondoa dhana hiyo. Aligusia pia mpango wa urasimishaji makazi holela na kueleza kuwa, ni matarajio yake kupitia kikoa hicho washirikia wataibuka na mkakati wa uelekeo wa wizara katika kupanga miji sambamba na usimamamia fedha zilizotolewa kwa ajili ya mpango wa kupanga, kupima na kumilikisha ardhi maarufu kama KKK.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni