SERIKALI imekopa takriban Shilingi bilioni 49 kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya Kituo cha Umahiri cha Mafunzo ya Taaluma za Usafiri wa Anga na Operesheni za Usafirishaji ambacho kina majukumu ya kutayarisha Wataalam wa Sekta ya Usafiri wa Anga.
Kauli hiyo imetolewa Jijini Dodoma na Mkuu wa Chuo Cha Taifa Cha usafirishaji NIT Prof. Zacharia Mganilwa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema kuwa Fedha hiyo imegawanywa katika upande wa ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya kufundishia Wataalam na jumla ya majengo matano yatajengwa Dar es Salaam kwa gharama ya Shilingi bilioni 21 na baadae itajenga majengo mkoani Kilimanjaro kwa sababu lazima Marubani wafundishiwe ndani ya Viwanja vya Ndege.
"Fedha nyingine itatumika kununua vifaa vya mafunzo, kwa kuwa Kituo kitafundisha Marubani, Wahandisi wa Ndege, Wahudumu Ndani ya Ndege na Waajiriwa wa Viwanja vya Ndege, chuo kimenunua ndege mbili zenye injini moja za mafunzo ambazo ziko njiani kuja Tanzania kwa gharama ya Shilingi Dola za Marekani milioni 1.2,
Katika Mwaka wa Fedha, 2022/23, Chuo kinanunua tena ndege yenye injini mbili kwa ajili ya mwanafunzi kukamilisha mafunzo yake kwa sababu mafunzo ya Urubani yanamtaka mwanafunzi ajifunze ndege yenye injini moja na injini mbili,"alifafanua.
Pia alisema kuwa Kumfundisha Rubani mmoja nje ya nchi ni Shilingi milioni 200, hivyo Serikali inapofanya uwekezaji huo inalifanya Shirika la Ndege Nchini kuleta matumaini ya nchi katika kukuza utalii na uchumi kwa sababu Wataalam wa usafiri wa anga watafundishwa hapa hapa nchini.
"Tanzania ina zaidi ya ndege 400 zilizosajiliwa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga ambapo asilimia 60 ya Marubani ni wageni, hivyo ndege hizi zitakapofika vijana wa kitanzania wenye sifa za kusomea Urubani watafundishwa na kupata ajira ndani ya nchi,
Kwa uwekezaji huu unaofanyika, tuna matumaini kuwa Shirika la Ndege la Tanzania litaweza kuwa Shirika bora kwa Afrika,"alieleza.
Alisema kuwa Serikali inaendelea kukuza Uchumi wa Buluu, hivyo kupitia uwekezaji wa mradi wa Benki ya Dunia wameweza kusomesha Wataalam wa kujenga meli na kusanifu meli kwa mara ya kwanza tangu kupatikana kwa Uhuru. Kuanzia mwaka 2023, kutakuwa na vijana ambao tayari wamemaliza masomo hayo.
"Kwa mara ya kwanza tangu tumepata Uhuru, chuo kinafundisha pia Diploma ya Uchomeleaji na Uungaji wa Bomba la Mafuta, hii itasaidia tusipeleke tu madereva na kina mama lishe bali tupeleke pia Wataalam watakaokuwa wanachoma bomba la mafuta,"alisema.
Alisema wana Kituo kingine cha Umahiri cha Kikanda katika usalama Barabarani ambacho kinafadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa Dola za Marekani Milioni 2.1 kwa mradi wote kikiwa na majukumu ya kufanya utafiti wa sababu za ajali na nini kifanyike pamoja na kufundisha Wakufunzi wa Madereva katika ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,Na Kwa mwaka wa masomo wa 2022/23, tunatarajia kufikisha wanafunzi 14,000.
Kwa upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa alisema kuwa Serikali iliamua kuwa na Chuo cha Usafirishaji kwa sababu kuendesha vyombo vya moto ni taaluma na ujuzi na kuna miongozo inayotakiwa kuzingatiwa, kinyume cha hapo ni hatari.
Alisema Safari inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita ya kuwekeza kwenye maeneo muhimu ya uchumi itategemea sana kuwa na wataalam wetu wa ndani kwani hakutakuwa na kunufaika na thamani ya miradi kama tunategemea wataalam kutoka nje.
"NIT watawezesha vijana wetu kunufaika na miradi mikubwa inayoendelea nchini mathalan ndege tano zinazotarajiwa kuja nchini, ambapo kwa mwaka 2023, ndege nne zitaingia nchini,"alisema.
Chuo cha Taifa cha Usafirishaji ni chuo cha elimu ya juu kinachotoa mafunzo kwenye njia kuu zote za uchukuzi na usafirishaji ikiwemo usafiri wa barabara, reli, anga, maji na mifumo ya mabomba,Chuo hiki kinatoa mafunzo, kinafanya utafiti na kinatoa ushauri wa kitaalamu, chuo kinatoa programu za Stashahada 25, Shahada za Kwanza 15, Shahada za Uzamili 3 na Postgraduate Diploma 9.
Chuo kina wafanyakazi 360, kina Wakufunzi mahiri katika Afrika na vifaa vya kisasa. Kwa mwaka wa masomo wa 2021/22, chuo kilikuwa na wanafunzi 13,000.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni