T.I.B YAKUBALI KUTOA FEDHA UJENZI WA HOSPITALI ARUSHA


ARUSHANa Mahmoud Ahmad Arusha
………………………………………
BENKI ya uwekezaji nchini TIB, imekubali kutoa shilingi bilioni 31 kugharimia ujenzi wa hospital ya rufaa ya mkoa wa Arusha, ambayo itajengwa kwenye eneo la hospital ya mkoa ya Mount Meru mapema mwaka huu.
Mkuu wa mkoa wa Arusha, Felix Ntibenda, amesema kuwa tayari taratibu za kupatikana kwa fedha hizo ambazo ni mkopo zimekamilika na hivi karibuni kutasainiwa mkataba kati ya benki hiyo na ofisi ya katibu tawala mkoa ili ujenzi huo uweze kuanza mara moja.
Ntibenda, amesema mkoa unaendelea wa kuboresha,majengo na huduma ya afya kwenye hospital hiyo ya mkoa wakati wakisubiri hospital ya rufaa ijengwe.
Amesema,ukarabati wa hospital hiyo unaofanywa kwa kushirikiana na wadau umewezesha kuirejesha hadhi ya hospital hiyo.
Amesema kuwa mkoa umewezesha kuanzishwa kwa bohari la dawa la MSD,ambalo tayari maandalizi yamefikia 95% na itafunguliwa wakati wowote na kuanza kutoa huduma za dawa kwa bei nafuu zaidi kuliko zinavyouzwa kwenye maduka binafsi.
Kwa upande wake,Katibu tawala mkoa wa Arusha, Adoh Mapunda, amesema kuwa wiki ijayo mkoa utasaini makubaliano ya kupatiwa mkopo na benki hiyo na kufuatiwa na hatua ya kutangaza zabuni ili kumpata mkandarasi atakae jenga hospital hiyo yenye majengo ya ghorofa tano ya hospital hiyo ya rufaa.
Amewapongeza wadau ambao wamejitokeza kuchangia ukarabati wa hospital hiyo ya mkoa unaoendelea na tayari jengo la wadi ya Grade one ,ambalo lilikuwa likihudumia kulaza wagonjwa katika hospital hiyo ya mkoa limefungwa likisubiri kubomolewa kutokana na uchakavu.
Akiwasilisha mpango kazi na mchoro wa jengo hilo, Mhandisi wa mkoa, Edward Amboka ,amesema kuwa hospital hiyo iliyojengwa mwaka 1915 majengo yake yamechakaa sana na hayafai kuendelea kutumika kama hospital .
Hospital hiyo ilijengwa ikiwa ni kambi ya kutibia majeruhi wa vita ya kwanza ya dunia hivyo mpango uliopo ni kujenga majengo mapya ya ghorofa na kubomoa ya zamani ambayo yamechakaa.
Amesema ujenzi huo utahusisha maeneo manane zikiwemo nyumba za watumishi ,mafunzo, mapumziko na maegesho ya magari.na mipango mingine ya uendelezaji wa hospitali hiyo
Amesema lengo la kujenga majengo hayo ni kupunguza mzigo wa wagonjwa mkoani Arusha ikiwemo vizazi na vifo vinavyotokana wakati wa kujifungua hivyo wanajenga jengo moja la ghorofa tano ambalo litatosheleza mahitaji badala ya kuwa na utitiri wa majengo
Kwa upande wake mganga mfawidhi wa hospital hiyo, Dakta Jacklin Urio, amesema hospital hiyo ina vitanda 500 na ina hudumia watu milioni 1.6 kwa mwaka lakini kutokana na ukuaji wa mji na ongezeko la watu hospital hiyo kwa sasa haitoshelezi mahitaji kutokana na wingi wa watu.
Amesema kuwa ujenzi wa hospital mpya ya rufaa utaiwezesha hospital ya rufaa kuwa na vitanda 600 ,kutakuwa ni vitanda 50 kwa ajili ya wagonjwa mahututi, ICU, na kati yake vitatu ni kwa ajili ya watu maalumu (VIP) wakiwemo viongozi wa kitaifa na kimataifa .
Jengo la Grade A,lilikuwa na vitanda 6,lakini kwa sasa halikidhi mahitaji na jengo jipya litakuwa na maabara ,wataalam, vitanda 50 vya wagonjwa wa Mahututi,(ICU) na huduma zingine .

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni