Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye (mwenye suti ya kijivu) akiwaeleza
Waandishi wa Habari (hawapo pichani) juu ya Uamuzi wa Serikali wa
kulifuta Gazeti la MAWIO katika Daftari la Msajili wa Magazeti mara
alipokutana na waandishi hao 17 Januari 2016 katika Ukumbi wa Idara ya
Habari uliopo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya
Habari, Bw. Assah Mwambene, wa pili kulia ni Mkurugenzi Msaidizi
anayeshughulikia usajili wa Magazeti, Bw. Raphael Hokororo na
anayemfuatia ni Mwanasheria wa Wizara Bw. Patrick Kipangula
Baadhi
ya Waandishi wa Habari wakifuatilia taarifa ya Serikali toka kwa Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye (hayupo
pichani) juu ya Uamuzi wa Serikali wa kulifuta Gazeti la MAWIO katika
Daftari la Msajili wa Magazeti mara alipokutana na waandishi hao 17
Januari 2016 katika Ukumbi wa Idara ya Habari uliopo jijini Dar es
Salaam.
(PICHA ZOTE NA BENEDICT LIWENGA-MAELEZO)
………………………………………………………………………………………………..
Na Benedict Liwenga-Maelezo.
Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeamua kulifuta kutoka katika Daftari
la usajili wa magazeti, gazeti lijulikanalo kama “MAWIO”.
Amri ya
kulifuta Gazeti hilo imetolewa leo na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo, Mhe. Nape Nnauye wakati alipokutana na Waandishi wa Habari
katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) uliopo Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Nnauye
amesema kuwa kupitia Tangazo la Serikali Na. 55 lililotolewa tarehe 15
Januari, 2016 Serikali imelifuta Gazeti hilo ikiwa ni uamuzi uliotolewa
kwa mujibu wa Sheria ya Magazeti Sura ya 229, kifungu 25(1).
Alieleza
kuwa, hatua ya kulifuta gazeti hilo inazuia pia gazeti la Mawio
kuchapishwa katika njia nyingine yoyote ikiwa ni pamoja na mitandao
(Online publication) kwa mujibu wa Sheria ya Mawasiliano ya Kieletroniki
na Posta Sura ya 306.
‘’Serikali
kwa masikitiko makubwa, imechukua uamuzi huu kutokana na mwenendo wa
uandishi wa gazeti hilo usioridhisha wa kuandika na kuchapisha habari
zenye mwelekeo wa uchochezi na kuhatarisha amani, utulivu na usalama wa
nchi yetu’’, alisema Nnauye.
Aidha,
alifafanua kuwa hatua hiyo ya kulifuta gazeti hilo imechukuliwa baada ya
Msajili wa Magazeti kufanya juhudi kubwa za muda mrefu kuanzia Juni,
2013 hadi Januari, 2016 kumtaka Mhariri wa gazeti hilo kubadili aina
ya uandishi wa habari na makala katika gazeti lake, bila mafanikio.
‘’Msajili wa
magazeti kwa juhudi zake alifanya mawasiliano na Mhariri wa gazeti hilo
mara nane kwa lengo la kutaka afanye marekebisho ya mtindo wa kutoa
habari zake lakini mhariri wa gazeti hilo hakuzingatia ushauri mzuri
aliopewa na Msajili wa Magazeti,
Ninatoa wito
kwa wamiliki, wahariri, waandishi na watangazaji wa habari kuzingatia
sheria, Kanuni na taratibu za taaluma ya uandishi wa habari ambazo
zikizingatiwa hakutakuwa na migogoro yoyote. Aidha Serikali inasisitiza
kwamba inaheshimu uhuru wa vyombo vya habari unaozingatia maadili,
weledi na Sheria za nchi na kwamba Serikali itaendelea kushirikiana
navyo’’ alisisitiza Mhe. Nnauye.
Katika hatua
nyingine, Waziri nape alitoa pongezi kwa Vyombo vyote vya habari nchini
vinavyozingatia maadili, weledi na Sheria zinazosimamia taaluma ya
habari na sheria nyingine za nchi.
‘’Kwa namna
ya pekee Serikali inawapongeza wamiliki na wahariri wa vyombo vya habari
ambavyo vinapofanya makosa vikielekezwa hujirekebisha na kutoa
ushirikiano kwa Serikali na pia kubadili mwenendo wao; hawa ni pamoja
na wahariri wa magazeti ya; Mwananchi Tanzania, Mtanzania, The East
African, Magazeti ya Daily News na Habari Leo, Uhuru na mengineyo’’,
alisema Mhe. Nnauye.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni