WANANCHI ZAIDI YA 100 WAVAMIA SHAMBA LA HEKA 33 LA WAZIRI MKUU MJIMPYA ENEO LA MABWEPANDE, NI WALIOBOMOLEWA NYUMBA MABONDENI JIJINI DAR ES SALAAM..
posted on
Wananchi zaidi ya 100, wakiwemo waliobomolewa maeneo ya mabondeni jijini Dar es Salaam, wamevamia shamba la Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye lenye ukubwa wa heka 33, lililopo Mji Mpya eneo la Mabwepande na kujikatia viwanja.
Sumaye ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa serikali ya awamu ya tatu kati ya mwaka 1995 hadi 2005, amekiri wananchi kuvamia shamba hilo lakini alisema hana wasiwasi kwasababu ana hati za umiliki.
Aidha alisema atafuata mkondo wa sheria kuhakikisha wavamizi hao wanaondoka kwenye shamba lake.
Juzi Nipashe ilishuhudia wananchi kadhaa wakiendelea kujenga nyumba za miti na wengine za matofali baada ya kujigawia kila mmoja eneo lake kwenye shamba hilo.
Musa Juma, aliyekutwa kwenye shamba hilo akijenga nyumba, alisema yeye ni miongoni mwa waathirika wa bomoa bomoa iliyofanyika Kinondoni Mkwajuni na kwamba amefika hapo baada ya mwenzao aliyemtaja kwa jina moja la Ema kuwaeleza kuwa kuna pori la Sumaye alilolitelekeza.
“Mwenzetu Ema alikuja kule bondeni tulikobomolewa na kutupa habari hiyo hivyo watu kama 100 tukaamua kuja na tukawakuta wengine tuliliona shamba hili likiwa ni pori kubwa ndipo tukaanza kujigawia vipande vipande,” alisema.
“Tumefanya kazi kubwa ya kulifyeka mpaka unaliona lipo katika hali hii, kazi haikuwa ndogo dada yangu, tumekutana na nyoka wakubwa, ukishuka kule bondeni kwenye kingo za shamba utajionea mwenyewe jinsi pori hili lilivyokuwa.”
Juma alisema walivamia shamba hilo mwezi Oktoba mwaka jana, na wengine walikuja baadaye baada ya kupata taarifa kuwa kuna shamba la bure ambalo limetelekezwa akiongeza kuwa wako pia watumishi wa serikali waliovamia shamba hilo.
“Aliwahi kuja mwanamke mmoja ambaye hatumfahamu akidai kuwa yeye ni mke wa kiongozi huyo na kutueleza kuwa tunapaswa kuondoka eneo hili eti ni mali yao lakini juzi kaja mwenyewe Sumaye; akatusalimia na kuondoka bila kusema lolote,” alisema.
“Mwamamke yule alikuja na watu wengine akiwemo mtu ambaye alikuwa akipiga picha na baadaye aliondoka hadi Alhamisi ya wiki hii walivyokuja wote na Sumaye mwenyewe ingawa hakusema lolote mpaka anaondoka hapa.
“Sumaye alikuja kwa sababu Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda, aliitisha mkutano na wananchi wa hapa, lakini tukiwa tumekusanyika tukimsubiria Makonda ghafla alifika Sumaye, ambaye hakushuka kwenye gari lake, alitusalimia kwa kutunyooshea mikono na kuondoka kwasababu Makonda hakuja siku hiyo.”
Alipoulizwa sababu za kuvamia shamba hilo, alisema walimsikia Rais John Magufuli kwenye kampeni akisema kuwa mashamba yote ambayo hayajaendelezwa yarudishwe serikalini na wapewe watu wenye uwezo wa kuyaendeleza.
Juma alisema wamejigawia shamba hilo na sasa wanasubiri serikali ije kuidhinisha kwa kuwamilikisha wao.
“Mtu anahodhi shamba kubwa kama hili halafu halijapimwa, tumetafuta alama za mipaka hakuna, wakati mashamba yote yaliyolizunguka shamba hili yamepimwa,” alisema.
Sumaye alisema anamiliki shamba hilo kihalali na ana hati zote na kwamba upo utaratibu wa kuchukua mashamba yaliyotelekezwa lakini sio huo walioutumia wananchi hao.
“Shamba hatujalitelekeza kama wanavyodai hao wananchi, tuna hati na ni letu kihalali, wanasema halina alama za mipaka je, waulize hati nilipataje? Shamba lina alama labda kama wamezing’oa kwa sababu ya jeuri.”
Sumaye alisema juhudi za kuhakikisha shamba hilo linarudishwa mikononi mwake zimeanza kufanyika na mamlaka husika na kusisitiza kuwa hatatumia nguvu kuwaondoa zaidi ya kufuata sheria.
Kuhusu kuonekana eneo hilo siku ya Alhamisi, Sumaye alisema alienda huko kwa sababu Makonda aliitisha mkutano na wananchi ili kutafuta suluhu ya mgogoro huo lakini hakufika baada ya kupata udhuru.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, Jastine Chiganga, alisema alipigiwa simu na Makonda akimweleza kuhusu mkutano huo lakini hakuweka bayana sababu za kuuitisha, ingawa aliuahirisha baada ya kupata dharura.
Makonda alilipoulizwa kuhusu lengo la mkutano aliouitisha na baadaye kuuairisha, alisema lilitokana na ofisi yake kupokea malalamiko ya uvamizi wa mashamba unaofanywa na wananchi eneo hilo.
Alisema baada ya kupokea malalamiko hayo aliomba kukutana na viongozi wa mitaa husika, wananchi, watu wa ardhi na wamiliki wa mashamba hayo ili kujua ukweli kuhusu mgogoro huo.
“Hilo shamba linalodaiwa kuwa ni la Sumaye, sijawahi kupokea malalamiko kutoka kwake dhidi ya uvamizi huo ila niliwahi kupigiwa simu na mmoja wa Makamanda wa Polisi Mkoa ambaye alinieleza kuhusu uvamizi huo,” alisema.
Aidha, Makonda alisema mbali ya shamba hilo la Sumaye yapo mengine likiwemo la Gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), marehemu Daudi Ballali ambalo nalo limevamiwa.
Alisema mkutano wake aliouitisha ulilenga kwenda kupata taarifa kamili ili hatua ziweze kuchukuliwa.
Makonda alitoa wito kwa watu wanaodai ni wamiliki halali wa mashamba yaliyovamiwa wajitokeze katika mkutano atakaouitisha wiki ijayo eneo hilo ili ufumbuzi uweze kupatikana.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni