Na. Mwandishi Maalum
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu na Bunge;
Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama
(Mb) ameuagiza uongozi wa Shirika la Tija la Taifa kuwa wabunifu katika
utoaji wa elimu kwa umma ili jamii iweze kujua kazi na huduma
zinazotolewa na shirika hilo.
Mhe.
Mhagama ametoa agizo hilo alipotembelea Shirika la Tija la Taifa (NIP)
Januari 15,2016 kwa lengo la kujionea kazi zinazotekelezwa pamoja na
changamoto zinazolikabili shirika hilo.
“Uongozi
lazima uangalie changamoto zinazolikabili shirika hili na kuangalia
namna ya kugeuza changamoto hizo kuwa fursa muhimu na kutoa elimu kwa
umma wa Watanzania ili wajue umuhimu wa kutumia huduma yenu kwa lengo la
kujiletea maendeleo,”alisema Mhagama
Waziri
alielekeza kuwa lazima viongozi wa NIP wawe wabunifu katika kutumia
vyombo mbalimbali vya habari vinavyoweza kuwafikia wananchi wa aina zote
huku akisisitiza kuangalia vipindi ambavyo havihitaji kulipiwa.
"Nendeni
mkaongee na wadau wa vyombo vya habari maana utakuta kuna fursa nyingi
mngeweza kuzitumia bila gharama yoyote. kuna vipindi kama vile Kipindi
cha Jambo Tanzania cha TBC 1, kipindi cha Kumekucha cha ITV, kipindi cha
360 Clouds Tv na Tuongee asubuhi cha Star Tv na vingine vingi amabavyo
mnaweza kuvitumia kuwafikia wananchi wengi," alisisitiza Mhe. Mhagama.
Waziri
alisema kuwa kwa kutumia ubunifu na fursa zilizoko kwenye vyombo vya
habari shirika litapata kujitangaza bila kutumia gharama na kuweza
kuyafikia malengo kama kuboresha ujuzi na uelewa wa usimamizi wa
rasilimaliwatu, kuchapisha na kusambaza fasihi na kuboresha utendaji wa
Taasisi za umma na zisizokuwa za umma.
Wakati
akimkaribisha waziri, Mkurugenzi Mtendaji wa NIP Bw.Novatus Massao
alieleza kuwa miongoni mwa changamoto zinazokabili shirika hilo ni
suala la taswira hasi kwa jamii na uelewa mdogo wa jamii kuhusu faida
na umuhimu wa Shirika hilo.
Kwa
upande wake mwenyekiti wa Bodi ya NIP, Prof.Samwel Wangwe aliahidi kuwa
shirika hilo litahakikisha linatekeleza maagizo yote ya Mhe. Mhagama
ili kuwezesha watanzania kuelewa na kutumia huduma za shirika hilo.
Aidha,
Mkurugenzi wa Fedha na Utawala Bw.Raphael Loishiye alimshukuru Mhe.
Waziri kwa kufanya ziara katika Shirika hilo na kujionea mazingira na
changamoto wanazokabiliana katika utekelezaji wa majukumu yao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni