MTO WA MBU KUKUMBWA NA BAA LA NJAA


Mbunge wa Monduli ,Julius Kalanga akitazama migomba iliyoharibiwa na upepo mkali uliotokea jana jioni katika kata ya mto wa mbu na kuharibu migomba mingi katika kata ya mto wa mbu.

                                                                          habari picha na woinde shizza,monduli

Wananchi wa Kata ya Mto wa Mbu iliyoko wilaya ya Monduli wako hatarini
kukumbwa na baa la njaa kutokana na upepo mkali uliotokea jana majira
ya saa kumi na moja jioni na kuangusha migomba ya ndizi ambayo
hutegemewa kama chakula kikuu na zao la biashara.

Wakulima hao walisema kuwa upepo huo mkali umeathiri mashamba makubwa ya migomba hivyo wameiomba serikali ichukue hatua za haraka kunusuru hali ngumu ya upatikanaji wa chakula itakayojitokeza siku zijazo.

Leyan Ngaboli na Moses Lengine ni wakulima wa ndizi wamesema kuwa
upepo huo utasababisha kusimama kwa biashara ya ndizi kwa kiasi kikubwa kwani tayari wakulima wameanza kupata hasara kwa kulazimika kuuza ndizi kwa bei ya chini ili zisiharibikie mashambani.

Afisa Mtendaji wa Kata ya Mto wa Mbu Kusumu Hassan alisema kuwa
karibu kaya na hekari zimeathiriwa na upepo huo hivyo ameiomba serikali isaidie wakulima hao waweze kurejea katika kilimo hicho ambacho huzalisha ajira nyingi.

Kwa upande wake Mbunge wa Monduli Julius Kalanga aliyefanya ziara ya
kuwatembelea waathirika wa upepo huo amewataka wananchi kuchukua
tahadhari huku akiahidi kushirikiana na serikali kutafuta chakula cha msaada kutoka serikalini ili kuwasaidia wakulima hao kwa kipindi ambacho wanaanza upya kulima mashamba yao kwani zao hilo huchukua muda mrefu.

"Nitazungumza na Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa mkoa tuangalie uwezekano wa
kupata chakula cha msaada ili kunusuru kaya zilizoathirika" Alisema Kalanga

Kata ya Mto wa Mbu hutegemea kilimo cha matunda matunda kama zao la
biashara na chakula ambapo matunda mengi kutoka kata hiyo hupelekwa katika masoko ya ndani nan je ya mkoa wa Arusha.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni