AFRIKA YAAZIMIA KUZALISHA UMEME WA KUTOSHA-MAJALIWA


WAZIRI MKUU Kassima Majaliwa amesema nchi za Bara la Afrika zimeazimia kujiimarisha katika uzalishaji wa umeme hadi vijijini ili uweze kuleta maendeleo.

Aliyasema hayo jana (Jumatatu Januari 29, 2018) alipozungumza baada ya mkutano wa Viongozi wa Wakuu wa Nchi za Afrika uliofanyika mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Katika Mkutano huo ambao Waziri Mkuu alimuwakilisha Rais Dkt. John Magufuli, alisema nchi za Afrika zimejipanga kuzalisha umeme wa kutosha mijini na vijijini.

Waziri Mkuu alisema nchi hizo zimeazimia kuzalisha umeme mwingi kwa lengo la kuinua kiwango cha maisha ya wananchi wake na kuharakisha maendeleo ya kiuchumi.

Alisema nchi za Afrika zinatakiwa zijitegemee kiuchumi, ambapo nchi za Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya nyingine za Afrika zimefikia amapendekezo ya kuimarisha uzalishaji wa umeme.

“Tanzania iko vizuri kwa sababu ina vyanzo vingi vya kuzalisha umene na sasa inamikakati ya kuzalisha umeme wa kutosha kuendesha viwanda vikubwa na kukaribisha wawekezaji kwenye maeneo mbalimbali.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alisema maelengo ya mkutamo huo yalikuwa ni kupokea taarifa za tume mbalimbali zilizoundwa katika kikao kilichopita.

Alisema miongoni mwa taarifa hizo ni pamoja na ya tume iliyokuwa inashughulikia masuala ya usalama na amani katika Bara la Afrika.

“Tume nyingine ilihusika na mapitio ya namna kuhamasisha nchi za Afrika kufikia kwenye maendeleo na nyingine ilikuwa inahamasisha mahusiano ya nchi kupitia kwenye Jumuia zilizopo ndani ya Bara la Afrika kama SADC.”

Pia Waziri Mkuu alisema mkutano huo ulifanya mapitio ya mapendekezo ya namna nchi za Afrika zinavyoweza kupata mitaji kupitia michango ya nchi mbalimbali, ambapo kanuni ziliandaliwa ili kuwezesha kila nchi kuchangia katika mfuko mkuu wa Umoja wa Afrika.

Alisema Tanzania ilihusika kutoa mchango juu suala la amani na usalama katika nchi za Afrika. ambapo kila nchi inawajibika kujilinda yenyewe na kulinda nchi jirani pamoja na Jumuia zake.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMANNE, JANUARI 30, 2018.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni