Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Joelson Mpina akiwahutubia wananchi wa kijiji cha Bwai Kumusoma wilayani Musoma leo ambapo alishiriki zoezi la kuchoma nyavu haramu zilizokamatwa na kikosi kazi cha kudhibiti uvuvi haramu Kanda ya Ziwa Victoria alichokiunda hivi karibuni, kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dkt. Vincent Anney akisoma majina ya Wavuvi Haramu (Na John Mapepele)
Asisitiza operesheni ya kutokomeza uvuvi haramu kanda ziwa ni ya kudumu
Na John Mapepele, Mara
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ameagiza viwanda vinne vya kuchakata samaki na mazao yake vilivyofungwa katika Mikoa ya Mwanza na Mara kuanza kazi mara moja ifikapo Julai Mosi mwaka huu, ambapo amewataka wamiliki kupeleka mipango kazi ya namna ya kuvifufua kabla ya kufikia mwezi Machi mwaka wizarani kwake.
Alivitaja viwanda hivyo kuwa ni Tan Perch Limited na Supreme Perch Limited vilivyopo Mwanza na Mara Fish Packers Limited na Prime Catch Limited katika mkoa wa Mara.
Waziri Mpina alizungumza hayo jana wakati alipokuwa kwenye ziara ya kikazi mkoani Mara na Mwanza kukagua operesheni maalum ya kutokomeza uvuvi haramu kanda ya Ziwa Victoria inayofanywa na kikosi kazi maalum alichokiunda hivi karibuni.
“Mimi kama Waziri mwenye dhamana ya Sekta ya Uvuvi nchini niliyepa kulinda raslimali za uvuvi nitahakikisha kwamba ulinzi wa raslimali hizi ni wa kudumu, na usio na mwisho hadi uvuvi haramu utakapoisha hapa nchini” alisisitiza Mpina
Waziri Mpina alipata fursa ya kuzungumza na Mkuu wa Mkoa wa Mara na Kamati ya Ulinzi ya Mkoa huo, wananchi katika maeneo tofauti na hatimaye kushiriki katika zoezi la kuchoma nyavu haramu ambapo hadi sasa zaidi ya nyavu zenye thamani ya shilingi bilioni nne zimechomwa moto katika zoezi linaloendelea la kudhibiti uvuvi haramu mkoani Mara.
Kamanda anayeongoza kikosi cha kupambana na kudhibiti uvuvi haramu na utoroshaji wa mazao ya uvuvi Kanda ya Mara, Bakari Lulela alimweleza Waziri Mpina kuwa operesheni hiyo imefanyika katika Wilaya za Musoma, Butiama, Rorya na Bunda na kufanikiwa kukamata na kuteketeza zana haramu zenye thamani ya sh. bilioni 3.2 huku wavuvi na wafanyabiashara wa samaki na mazao yake waliokiuka sheria ya uvuvi wakitozwa faini ya sh. milioni 189.
Waziri Mpina aliziagiza mamlaka zinazohusika kuwachukulia hatua Maafisa Uvuvi wa Kijiji cha Bwai Kumsoma waliotuhumiwa kushirikiana na wavuvi haramu kuondolewa mara moja katika kijiji hicho ili kupisha uchunguzi na ikithibitika wachukuliwe hatua kali kwa mujibu wa sheria.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dk. Vincent Anney amesema kwamba hayuko tayari kuona Wilaya yake inaendelea kuishi na watumishi wanaojihusisha na uvuvi haramu na kwamba sheria kali zitachukuliwa dhidi yao ikiwa ni pamoja na kuwaondoa katika wilaya hiyo.
Aidha Waziri Mpina ameiagiza Wizara yake kuandaa bei elekezi ya kununua samaki itakayowezesha kuondokana na tabia ya wenye viwanda kushusha hovyo bei pindi samaki wanapoongezeka na hivyo kuwadhulumu wavuvi kupata malipo stahili yanayotokana na kazi yao.
Waziri Mpina alisema Ziwa Victoria ni hazina na raslimali kubwa kwa Tanzania ambapo inaaminika kuwa ni la kwanza kwa ukubwa katika bara la Afrika kwa kuwa na eneo la 68,000Km2 na la pili duniani.
Alisema pamoja na umuhimu wa ziwa hili katika kukuza uchumi na kuboresha maisha ya watanzania bado linakabiliwa na shughuli za uvuvi haramu uliokithiri ambapo tafiti zinaonyesha kwamba kama hakutakuwa na jitihada za haraka za kutokomeza uvuvi haramu, ziwa hilo hali halitakuwa na raslimali za uvuvi ikiwa ni pamoja na samaki katika kipindi cha miaka miwili ijayo.
Alitaja uvuvi haramu unaofanywa kuwa ni pamoja na kuvua katika maeneo yasiyoruhusiwa, kutumia valiyombo visivyosajiliwa, kuvua bila leseni,kutumia sumu, kutumia nyavu za utali na kuvua samaki wachanga ama wazazi wasioruhusiwa.
Uvuvi haramu mwingini nikuvua kwa kokoro na nyavu zenye macho madogo chini ya kiwango kinachokubalika kisheria, katuli, kumbakumba na gizagiza ambapo alisema Serikali imedhamilia kutokomeza uvuvi huo haramu.
Aidha alisema operesheni hiyo katika kanda ya Ziwa Victoria dhidi ya uvuvi haramu ni ya kudumu na inafanyika kwa kuzingatia Sheria ya Uvuvi Na.22 yaMwaka 2003 na Kanuni 58(1) ya Uvuvi ya Mwaka 2009 na Sheria ya Mazingira Na 20 ya Mwaka 2004 kifungu Na(1), 65(1)a pia Sheria ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Na 29 ya Mwaka 1994 ili kudhibiti uvuvi haramu ulioshamiri kiasi cha kutoweka kwa raslimali ya samaki katika ziwa hilo kwa faida ya vizazi vya sasa na baadaye.
Waziri Mpina alisema Tanzania inamiliki 51% ya Ziwa hili ikifuatiwa na Uganda 43% na nchi ya Kenya inamiliki 6%. Ziwa hili ni moja ya maziwa yanayozalisha samaki kwa wingi duniani kwa makadirio ya takribani tani 1,000,000 kwa mwaka ambapo asilimia 60 ya uzalishaji wa samaki wake unatoka Tanzania hivyo juhudi za pamoja za kutokomeza uvuvi haramu zinahitajika |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni