MAMLAKA HIFADHI YA NGORONGORO KULIPENDEZESHA JIJI LA DODOMA


????????????????????????????????????
Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Profesa Davis Mwamfupe (katikati), Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi na Kaimu Meneja Uhusiano Mamlaka Hifadhi ya Ngorongoro, Joyce Mgaya wakisaini hati ya makubaliano ya kuboresha mandhari ya mizunguko ya magari kwenye barabara kuu za jiji hilo. Kwenye uboreshaji huo wa mandhari Mamlaka Hifadhi ya Ngorongoro itaweka vivutio mbalimbali kutangaza utalii
……………………
Na: Abuu Kimario
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imeingia makubaliano na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuboresha mandhari ya mizunguko ya magari (roundabout) kwenye barabara kuu za jiji hilo.
Makubaliano hayo yamefikiwa leo kwenye hafla ya fupi ya kutiliana saini ambapo jiji la Dodoma liliwakilishwa na Meya, Profesa Davis Mwamfupe na Mkurugenzi Mtendaji,  Godwin Kunambi na upande wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro iliwakilishwa na Kaimu Meneja Uhusiano, Joyce Mgaya kwa niaba ya Mhifadhi Mkuu wa mamlaka hiyo Dkt. Fredy Manongi.
Kwenye makubaliano hayo Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imekubali kuifanyia ukarabati mizunguko mitatu ya magari ambayo ni mizunguko ya barabara kuu za Dar-es-Salaam (Shabiby), Singida na Arusha.
Akiwasilisha salamu za Mhifadhi Mkuu, Kaimu Meneja Uhusiano Mgaya amesema, uongozi wa jiji la Dodoma kuichagua mamlaka hiyo ni heshima kubwa na wanaipokea kwa mikono miwili na pia mamlaka hiyo itaendelea kushirikiana na halmashauri ya jiji kwenye kuibua fursa mbalimbali za kitalii.
Aidha, Mgaya ameongeza kuwa makubaliano hayo yaliyofikiwa ni fursa ya Halmashauri ya jiji la Dodoma na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kubadilishana uzoefu kwenye maeneo ya uhifadhi wa mazingira na kuboresha mandhari.  
Kwa upande wake Meya wa Jiji la Dodoma, Mstahiki Davis Mwamfupe amesema nia ya uongozi wa jiji la Dodoma ni kulifanya liwe jiji la mfano wa kuigwa na majiji mengine ya Tanzania, barani Afrika na duniani kwa kuwa na mazingira bora kuishi na mandhari yenye kuvutia.
Nae Mkurugenzi Mtendaji, Godwin Kunambi ameishukuru Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa kukubali ombi la kutengeneza sanamu kubwa ya tembo kama ishara ya kuhifadhi historia ya chimbuko la jina la mkoa wa Dodoma. Kwa mujibu ya maelezo ya wenyeji wa mkoa huo jina Dodoma limetokana na neno la kigogo “idodomya” baada ya tembo kudidimia ardhini miaka mingi iliyopita.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni