WAZIRI KIGWANGALLA ATOA SIKU 90 KWA TAWIRI KUFANYA SENSA YA MAMBA ZIWA RUKWA NA TFS KUANDAA MPANGO WA KITAIFA WA UVUNAJI MISITU



Na Hamza Temba, Songwe
…………………………………………………………..
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla ametoa miezi mitatu kwa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) kufanya utafiti na sensa ya mamba katika ziwa Rukwa ili kubaini idadi yake na hatimaye kuishauri Serikali namna ya kudhibiti madhara yanayosababishwa na mamba hao kwa wananchi hususan wa jimbo la Songwe ikiwemo kuwavuna kama idadi yao itabainika kuwa kubwa kupita kiasi.
 
Dk. Kigwangalla ametoa agizo hilo jana katika kijiji cha Maleza, kata ya Mbangala, wilaya ya Songwe mkoani Songwe alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wakati wa ziara yake ya siku moja wilayani humo kwa ajili ya kutatua mgogoro uliopo baina ya wananchi na Mamba wa ziwa Rukwa.
 
“Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori ambayo ipo chini ya wizara yangu, nawaagiza wafike hapa mara moja, ndani ya miezi mitatu wanipe majibu nini kifanyike kupunguza madhara yanayotokana na mamba kwenye ziwa Rukwa, wafanye sensa watuambie kuna Mamba wangapi lakini pia watushauri nini tufanye ili kudhibiti mamba hao wasiendelee kusababiaha athari kubwa kwenye maisha ya watu wanaoishi jirani, lakini pia wanaoutumia ziwa.
 
“Kwa sababu madhara yanaweza yakawa mengi, inawezekana mamba wameshakuwa wengi na samaki wamebaki wachache, kwahivyo hata mamba nao mwishowe wataanza kufa ama wataanza kutafuta chanzo kingine cha chakula pengine ndio maana wameanza kutafuta binadamu wanakwenda ziwani kwasababu wanakuwa na njaa, inabidi wasogee ufukweni wawinde chochote kinachosogea karibu na maji” alifafanua Dk. Kigwangalla. 
 
Dk. Kigwangalla ametoa agizo hilo kufuatia malalamiko mbalimbali yaliyowasilishwa kwake na mbunge wa Jimbo la Songwe, Phillipo Mulugo ambaye amesema kumekuwepo na matukio mengi ya mamba kushambulia na kuuwa wananchi wa vijiji jirani wanaofata huduma mwambao wa ziwa Rukwa. 
 
Katika hatua nyingine Dk. Kigwangalla ametoa miezi mitatu kwa Wakala wa Huduma za misitu Tanzania kuandaa mpango wa kitaifa kwa kila wilaya na vijiji nchini utakaoweka utaratibu maalum wa namna na sehemu wananchi watakayopata huduma ya kuni mkaa.
 
“Utaratibu uwekwe na muuweke nchi nzima, kila wilaya, kila kata, kila kijiji uwekwe utaratibu wananchi watapata wapi mkaa, watapata wapi kuni, kibali cha kuvuna kitapatikana wapi, utaratibu uwe wazi, sio kusubiri kwenye mageti unakamata, hapana weka utaratibu kwanza, ukishaweka utaratibu atakayevunja sheria hata ukimkamata ukimpeleka polisi utakuwa umemrahisishia OCD kazi. 
 
“Kwa sababu hata OCD atakuwa anajua kwamba katika hii wilaya ninayoiongoza hapa ndio mipaka ya mkaa, hapa ni mipaka ya kuni, wewe umetoa wapi, kibali chako kiko wapi, umevunja sheria, mahakamani” ameeleza Dk. Kigwangalla. 
 
Wakati huo huo, Dk. Kigwangalla ametangaza kutaifishwa kwa greda ambalo limekutwa likiwa limetelekezwa na watu wasiojulikana ambao walikuwa wakichimba mchanga wa dhahabu (makinikia) kinyume cha sheria ndani ya Hifadhi ya msitu wa Patamela wakati wa ziara yake wilayani Songwe.
 
Kufuatia tukio hilo, amemuagiza Kamanda wa Polisi wa wilaya hiyo kulinda eneo hilo na kutafuta dereva atakayeendesha greda hilo hadi kituo cha polisi kwa ajili ya kufuata taratibu za sheria za kulitaifisha na wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla akizungumza na wananchi wa kijiji cha Maleza kata ya Mbangala wilaya ya Songwe mkoani Songwe alipofanya ziara ya kikazi katika kijiji hicho jana kwa ajili ya kutatua mgogoro wa mamba wa ziwa Rukwa ambao wamekuwa wakidhiru wananchi wa kijiji hicho na vijiji jirani.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla akitoa agizo la kutaifishwa kwa greda (pichani nyuma) lililokutwa ndani Hifadhi ya Msitu wa Patamela baada ya kutelekezwa na watu watu wasiojulikana waliokuwa wakichimba mchanga wa dhahabu (makinikia) kinyume cha sheria ndani ya Hifadhi hiyo katika wilaya ya Songwe mkoani Songwe jana.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla akitoa maelekezo kwa uongozi wa wilaya ya Songwe kufuatia greda lililokutwa ndani Hifadhi ya Msitu wa Patamela ambalo limetelekezwa na watu wasiojulikana waliokuwa wakichimba mchanga wa dhahabu (makinikia) kinyume cha sheria ndani ya Hifadhi hiyo katika wilaya ya Songwe mkoani Songwe jana.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla akishirikiana na baadhi ya viongozi wa wilaya ya Songwe kuzima moto uliokutwa ukiwaka ndani ya Hifadhi ya Msitu wa Patamela wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani humo jana.
Dk Hamisi Kigwangalla akishirikiana na baadhi ya viongozi wa wilaya ya Songwe kuzima moto uliokutwa ukiwaka ndani ya Hifadhi ya Msitu wa Patamela wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani humo jana.
Juhudi za kuzima moto zikiwa zinaendela.
Dk Kigwangalla akiwa anazungumza na wananchi wa kijiji Maleza.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla akimsikiliza Mbunge wa Jimbo la Songwe, Philipo Mulugo alipokuwa akiwasilisha malalamiko ya wananchi wa jimbo lake ambao wamekuwa wakipata madhara makubwa ya mamba wa ziwa Rukwa.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni