UJUMBE WA WATAALAMU WA AFYA KUTOKA BRAZIL WAKUTANA NA WAZIRI WA AFYA ZANZIBAR.


6 (5)
BALOZI wa Heshima wa Brazil hapa Zanzibar, Abdulsamad  Abdulrahim (suti buluu) akiwa na Ujumbe wa wataalamu wa Afya kutoka Brazil wakitembelea Kituo cha Afya Fuoni.
1 (4)
 WAZIRI wa Afya Zanzibar Hamad Rashoid Mohamed akizungumza na Ujumbe wa Wataalam wa Afya kutoka Nchi ya Brazil Afisini kwake Mnazi Mmoja Mjini Zanzibar.
7 (3)
UJUMBE wa wataalamu wa Afya kutoka Brazil wakiangalia takwimu za mama wajawazito wanaofika kupata huduma ya kujifungua Kituoni hapo.
Na Ramadhani Ali – Maelezo
Ujumbe wa watu nane wa Wataalamu wa afya kutoka Serikali ya Brazil upo Zanzibar kutekeleza ombi la Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Muhamed Shein kuitaka nchi hiyo kuzidisha ushirikiano  katika sekta ya Elimu, Afya na Utalii.
Ujumbe huo ukiongozwa na Mratibu Mkuu wa Kanda ya Afrika, Asia, nchi za Oceanic na Mashariki ya mbali Fabio Webber umefanya mazungumzo na Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed kujifunza changamoto zinazowakabili mama wajawazito na watoto wachanga.
Webber alisema Rais wa Zanzibar alipofanya mazungumzo na Balozi wa Brazil aliomba nchi hiyo kufungua ubalozi mdogo Zanzibar, kusaidia kuimarisha masuala ya afya na kuwajengea uwezo wafanyakazi wa sekta hiyo.
Balozi wa Heshma wa Brazil hapa Zanzibar Abdulsamad Abdulrahim alisema baada ya Serikali ya Brazil kufungua Ubalozi mdogo Zanzibar, wanaelekeza nguvu zao juu ya afya ya mama mzazi na mtoto pamoja na kuwajengea uwezo wafanyakazi wa kitengo hicho.
Alisema ujumbe huo utafanya ziara katika vituo mbali mbali vya afya Unguja na Pemba kuangalia changamoto zinazowakabili mama wajawazito wakati wa kujifungua na watoto wachanga na hatiamae kuzitafutia ufumbuzi.
Waziri wa Afya aliueleza ujumbe huo kuwa Serikali inaendelea kuimarisha huduma za afya ya msingi vijijini ili vituo vya afya vya huko viwe na uwezo na vifaa vya kutosha na wananchi waviamini na wavitumia.
Alisema hivi sasa kumekuwa na msongamano mkubwa wa wazazi katika Hospitali kuu ya Mnazimmoja huku vituo vya afya vijijini vyenye uwezo wa kutoa huduma za kuzalisha vinakosa wazazi kutokana na dhana kuwa huduma ni ndogo.
Alisema kuimarika kwa vituo vya afya vya vijijini vinavyotoa huduma ya mama na mtoto kutaipunguzia hospitali hiyo msongomano wa wazazi na kumudu kutoa huduma zilizo bora zaidi.
Ujumbe huo umeanza kazi ya kutembelea vituo vya afya vinavyotoa huduma ya kuzalisha kuona hali halisi na kujua changamoto zinazovikabili vituo hivyo na baadae kufanya uchambuzi wa kujua masuala yanayopaswa kutekelezwa kuongeza mashirikiano .

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni