KAIMU JAJI MKUU AWAAGIZA MAJAJI KUZIPA KIPAUMBELE KESI ZENYE MASLAHI KWA UMMA

Na Lydia Churi- Mahakama, Arusha
Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Prof.Ibrahim Juma amewaagiza Majaji wote nchini kuzipa umuhimu wa kipekee wa kuzisikiliza na kuzimaliza kwa haraka kesi zote zenye mvuto kwa jamii na zenye maslahi kwa Umma ili kuongeza imani ya wananchi juu ya Mahakama kama chombo cha utoaji wa haki.
Akifungua mafunzo ya Majaji wa Mahakama ya Rufani pamoja na Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania alizitaja kesi zinazotakiwa kusikilizwa na kumalizwa kwa haraka kuwa ni zile zinazohusu dawa za kulevya, ujangili, ugaidi, Mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi pamoja na mauaji ya vikongwe kwa imani za kishirikina.
Prof. Juma alizitaja kesi nyingine zinazotakiwa kupewa umuhimu wa kipekee kutokana na mvuto wake kwa jamii kuwa ni pamoja na kesi za rushwa kubwa, utakatishaji wa fedha, matumizi mabaya ya madaraka kwa viongozi, na kesi zinazohusu changamoto za ukuaji wa demokrasia na uendeshaji wa masuala ya siasa.
Kesi nyingine zilizotajwa na Jaji Mkuu katika kupewa umuhimu wa kipekee ni  zile zinazohusu miradi mikubwa kama Reli, mashamba makubwa ya uwekezaji, gesi, ujenzi wa barabara, kesi za mabenki na kesi zinazohusisha kundi kubwa la watu zinazogusa migogoro ya umiliki wa ardhi na migogoro ya wakulima na wafugaji.
“Tukichukua hatua za dhati kuhakikisha kesi hizi zinaisha kwa wakati tutakuwa tumetoa mchango mkubwa katika kukuza uchumi na kuongeza imani ya wananchi kwa Mahakama”, alisema Kaimu Jaji Mkuu.
Alisema ni Jambo muhimu kwa Mahakama kuzipa umuhimu wa kipekee kesi hizi hasa katika kipindi hiki  ambacho Serikali inatekeleza mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano (2016/17-2021) ambao kauli mbiu yake ni “kujenga uchumi wa viwanda  ili kuchochea mageuzi ya uchumi na Maendeleo ya watu”.
Aidha, Kaimu Jaji Mkuu pia amewataka Majaji kuangalia namna ya kutoa huduma kwa haraka kwenye makundi yenye mahitaji maalum kama vile wazee, walemavu na wajane hususan wakati huu ambapo Mahakama inaelekeza nguvu zaidi katika kuondosha mlundikano wa mashauri mahakamani.
Aliwakumbusha Majaji hao kupanga kesi kwa siku kwa kuzingatia masaa kama njia ya kuwaepusha wananchi wenye kesi mahakamani na adha ya kusubiria kwa muda mrefu kesi zao kuitwa.
Akizungumzia usikilizwaji wa kesi Mahakamani, Prof. Juma alisema kwa mwaka 2016, Mahakama kuu ya Tanzania pamoja na divisheni zake zote ilifanikiwa kumaliza kesi kwa idadi sawa na zilizosajiliwa. Alisema, jumla ya kesi 276,147 zilisajiliwa na kwamba kesi 278,226 zilimalizika. Kesi 57,326 zilibaki mahakamani.
Alisema bado kuna changamoto ya mlundikano wa kesi kwenye Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu ambapo lengo kuu la Mafunzo hayo kwa Majaji ni kujadili namna ya kumaliza mlundikano wa kesi kwenye Mahakama hizi.
Aliongeza kuwa Mahakama za Mwanzo pekee ndizo zenye mafanikio makubwa ya kutokuwa na mlundikano wa kesi. Mpaka kufikia Desemba 2016,  Mahakama za Mwanzo zilimaliza kesi zote zenye umri unaozidi miezi sita mahakamani.

Majaji wa Mahakama ya Rufani na Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wanaendelea na Mafunzo ya siku tano mjini Arusha ambapo wanajifunza mambo mbalimbali yanayohusu utendaji wao wa kazi likiwemo suala la kuondosha mlundikano wa kesi kwenye Mahakama zote nchini. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni