MAGUFULI:MTANZANIA ALINDE NA KUIMARISHA MUUNGANO



Kila mtanzania ametakiwa kuhakikisha anafanya jitihada za kuimarisha na kulinda Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulioasisiwa miaka 53 iliyopita.

Akizungumza leo wakati akihutubia wananchi katika sherehe za Maadhimisho ya miaka 53 ya Muungano katika uwanja wa Jamhuri uliopo mjini Dodoma, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alisema kuwa ni muhimu watanzania wakalinda Muungano kwa vile una manufaa kwa nchi zote mbili.

“Kila mtanzania ahakikishe anafanya jitihada za kuimarisha na kulinda Muungano wetu, kwa vile Muungano na amani iliyopo nchini ndio chachu ya maendeleo yetu” alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli alisisitiza kuwa “Muungano ndio silaha yetu, ni nguvu yetu, mimi na mwenzangu Dkt. Shein tutaulinda Muungano kwa nguvu zote na yeyote atakayejaribu kuuvunja atavunjika yeye” alisema Rais Magufuli

Akitaja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika miaka 53 ya Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar ni pamoja na kuunganisha mataifa mawili na kuunda taifa moja lenye nguvu.

Rais Magufuli alitaja mafanikio mengine ni pamoja na kuwa ni kuimarisha miundombinu ya usafiri wa anga, majini, nchi kavu na reli, kukabiliana na matatizo ya umaskini, ukosefu wa ajira na kukua kwa uhusiano wa diplomasia kati ya Tanzania na mataifa mbalimbali ambapo yamepelekea mafanikio katika nyanja za kiuchumi, kisiasa, na jamii.

Aidha, hii ni mara ya kwanza kwa sherehe za Maadhimisho ya Muungano kufanyika mkoani Dodoma ambapo, Rais Magufuli alisema kuwa Serikali imeendelea kufanya jitihada mbalimbali za kujenga miundombinu ili kufikia azma yake ya kuhamishia makao yake makuu mjini Dodoma ifikapo mwaka 2020.

“Niwahakikishie wana Dodoma na Watanzania kwa ujumla kwamba Serikali sasa tumefika Dodoma na hatutarudi nyuma tena,ambapo awamu ya kwanza ya watumishi wa Serikali takribani 3,000 kwa ngazi za Mawaziri,Naibu Waziri,Makatibu wakuu na Manaibu Katibu wakuu wameshahamia Dodoma, kama tulivyoahidi kufikia mwaka 2020, Serikali yote itakuwa imehamia hapa”, alisisitiza Rais Magufuli.

Sherehe za Maadhimisho ya miaka 53 ya Muungano zenye kauli mbiu isemayo “Miaka 53 ya Muungano, tuulinde na kuimarisha, tupige vita dawa za kulevya na kufanyakazi kwa bidii”, zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali pamoja na wajane wa viongozi waasisi wa Muungano ambapo ni Mama Maria Nyerere na Mama Shadya Karume.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni