Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kushoto akivishwa
Skafu na Kijana Omar Amour Said wa Skauti nje ya Ukumbi wa Baraza la
Wawakilishi wa zamani Kikwajuni Mjini Zanzibar kabla ya kuzungumza na
Vijana wa Chama cha Sakauti Zanzibar.
Kati kati yao ni Raius wa Chama cha Skauti Zanzibar ambae pia ni
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Riziki Pembe Juma.
Balozi
Seif akiambatana na Rais wa Skauti Zanzibar Mh. Riziki Pembe Juma
wakielekea ndani ya Ukumbi wa Mkutano kuzungumza na Vijana wa Skautio
Zanzibar wanaotarajiwa kuondoka Zanzibar kuelekea Mkoani Dodoma katika
maadhimisho ya Miaka 100 ya Skauti Tanzania.
Balozi
Seif akimpongeza Kijana Kassim Yussuf Msoma Mashairi ghibu baada ya
kughani kwenye Mkutano wa Skauti Zanzibar uliofanyika kwenye Ukumbi wa
Mikutano wa Baraza la Wawakilishi wa Zamani Kikwajuni.
Baadhi
ya Skauti wa Zanzibar wakifuatilia Mkutano wa Chama hicho uliohutubiwa
na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi uliokuwa wa
matayarisho ya mwisho wa Vijana wake kujiandaa kuelekea Dodoma katika
Tamasha la Miaka 100 ya Skauti Tanzania.
Baadhi
ya Makatibu wa Skauti wa Mikoa ya Unguja wakifuatilia Hotuba ya Balozi
Seif ambaye hayuko pichani hapo katika Ukumbi wa zamia wa Baraza la
Wawakilishi Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiwahutubia VBijana wa Chama
cha Skauti Zanzibar wanaojiandaa kuelekea Dodoma katika Tamasha la
Miaka 100 ya Skauti Tanzania.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema wakati umefika kwa Chama cha Skauti Nchini kuongeza nguvu za kuwaelimisha Vijana wenzao hasa walioko Vijijini ili wajikomboe kupenda kujishughulisha na kazi au miradi ya ujasiri amali.
Alisema Vijana wengi wamekuwa na tabia ya kujihusisha na vigenge vya kihuni mitaani vinavyopelekea kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya wizi pamoja na vitendo vya kudhalilisha watoto wanawake na watu wenye mahitaji Maalum.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa Kauli hiyo wakati akizungumza na Vijana wa Chama cha Skauti Zanzibar wanaojiandaa kuelekea Mkoani Dodoma kushiriki Tamasha la Wiki Moja la Maadhimisho ya Miaka 100 ya Skauti Tanzania hapo katika Ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Alisema zipo fursa nyingi za ajira zinazopatikana katika Sekta ya Utalii ambazo Vijana endapo wataamua kuzichangamkia zinaweza zikawapatia kipato kwa kutumia soko la bidhaa zinazotokana na kilimo cha mboga mboga na mazao ya Baharini.
Balozi alifahamisha kwamba Uskauti kwa vile hauna mafungamano ya itikadi ya Kisiasa wala Dini unalengo la kuwaunganisha Vijana katika harakati zao za kimaisha kupitia misingi ya kujenga Utaifa wao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisisitiza umuhimu wa vijana wa Skauti kufundishwa mbinu na mafunzo ya kuogelea na kuzamia kutokana na majukumu yao yaliyowazuunguka ya kuwa wao ni miongoni mwa Taasisi zinazotoa huduma wakati yanapotokea maafa au majanga.
Balozi Seif alielezea kuridhika kwake na Kanuni 10 za Skauti zinazoelekeza uzalendo unaojenga Taifa lenye Wananchi wanaopendana na kuwa na nguvu za kukabiliana na changamoto zinazowazunguuka katika misingi ya nidhamu na uwajibikaji.
Mapema Kamishna Mkuu Msaidizi wa Chama cha Skauti Zanzibar Maalim Suleiman Takadir alisema Skauti iliasisiwa Zanzibar mnamo mwaka 1912 na Mwaka 1917 ikaanzishwa upande wa Tanzania na kufifia katika miaka ya 60.
Maalim Takadir alisema Chama hicho kilianzishwa tena Mwaka 1992 chini ya Rais wa Awamu ya Tano Dr. Salmin Amour ili kufufua ari ya kuwajenga Vijana katika uzalendo.
Alisema Chama cha Skauti kimejiwekea Kanuni Kumi zinazoiongoza Taasisi hiyo ikiwa ni pamoja na kuaminika, adabu, huruma, utiifu, uchangamfu, uadilifu pamoja na usafi wa vitendo.
Akizungumzia changamoto zinazokikabili chama hicho cha Skauti Zanzibar Kamishna Mkuu Msaidizi huyo wa Skauti Zanzibar alizitaja kuwa ni pamoja na ukosefu wa Ofisi ya kufanyia kazi pamoja na uwanja wa kufanyia mazoezi kwa Vijana wake.
Maalim Takadir aliwaomba Wakuu wa Mikoa na Wilaya Nchini kufanya kazi kwa karibu na Makamishna wa Skauti wa Mikoa ili kufanikisha malezi ya vijana katika maeneo hayo.
Akitoa salamu Rais wa Chama cha Skauti Zanzibar ambae pia ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Riziki Pembe Juma amemshukuru Rais Mstaafu wa Zanzibar wa Awamu ya Tano Dr. Salmin Amour kwa busara zake za kuifufua tena Skauti Zanzibar.
Waziri Riziki alisema ule ukakamavu unaoonyeshwa na Vijana Skauti katika matendo yao ya kila siku yamewawezesha kuwa na nguvu za mawazo na kiakili zinazowasababishia kufanya vizuri katika masomo na mitihani yao.
Alisema Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar ina wajibu wa kutoa Elimu na malezi kwa Watoto wote bila ya ubaguzi ambao ni wajibu wa lazima na sio wa kupendelea.
Timu ya Vijana hao walioteuliwa 40 wa Skauti Zanzibar wanaondoka Visiwani kesho kuelekea Mkoani Dodoma kushiriki Wiki ya Tamasha la kuadhimisha Miaka 100 ya Skauti Tanzania.
Othm,an Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
19/7/2017
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni