Selemani
Jaffo, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi) akisikiliza
maelezo kutoka kwa mama Abia Magembe kuhusu bidhaa zinazotokana na zao
la muhogo. Kushoto kabisa ni Mratibu wa Mradi wa Green Voices kutoka
Hispania, Alicia Cebada na kulia ni Mratibu wa mradi huo nchini
Tanzania, Secelela Balisidya.
NAIBU
Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani
Jaffo, amesema halmashauri zinawajibu wa kuunga mkono jitihada za
utunzaji wa mazingira na kupambana na mabadiliko ya tabianchi.
Kutokana
na hali hiyo, ameonya mtu yeyote asikwamishe jitihada zinazofanywa na
akinamama washiriki wa mradi wa Green Voices Tanzania huku akiahidi kuwa
serikali iko nao bega kwa bega. Alisema kwamba, endapo kuna mtu katika
idara zilizo chini ya wizara yake atakwamisha jitihada zao, basi
akinamama hao wawasiliane naye moja kwa moja.
Akizungumza
wakati wa uzinduzi wa awamu ya pili ya mradi wa Green Voices nchini
Tanzania uliofanyika kwenye Hoteli ya Golden Tulip jijini Dar es Salaam,
Naibu Waziri Jaffo alisema kwamba, wizara yake ndiyo yenye jukumu kubwa
la kuwawekea mazingira mazuri akinamama hao kutekeleza miradi yao chini
ya halmashauri husika, hivyo akawaahidi kuwapatia ushirikiano wa
kutosha kuhakikisha miradi hiyo inakuwa endelevu na suala la mazingira
linapewa kipaumbele.
Mradi
wa Green Voices unatekelezwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani,
Morogoro, Kigoma, Mwanza na Kilimanjaro, kukiwa na miradi 10 ikiwemo ya
kilimo cha mihogo, kilimo cha matunda, uyoga, ufugaji wa nyuki,
ukaushaji wa mbogamboga na utengenezaji wa majiko rafiki wa mazingira.
Bidhaa za mbogamboga zilizokaushwa kutoka Morogoro.
Akinamama walioanzisha miradi hiyo – miradi na mikoa watokayo vikiwa kwenye mabano –ni Regina Kamuli (Mkuranga, Pwani – Majiko Banifu), Abiah Magembe (Kisarawe, Pwani – Usindikaji wa Muhogo na Mtama), Magdalena Bukuku (Kinondoni, Dar es Salaam – Kilimo cha Uyoga), Mariam Bigambo (Dakawa, Morogoro – Ufugaji wa Nyuki), na Esther Muffui (Morogoro – Ukaushaji wa Mboga na Matunda).
Wengine ni Farida Makame (Kilimanjaro – Majiko ya Umeme-Jua), Leocadia Vedastus (Ukerewe, Mwanza – Kilimo na Usindikaji wa Viazi Lishe), Monica Kagya (Kisarawe, Pwani – Ufugaji wa Nyuki), Dkt. Sophia Mlote (Kinyerezi, Dar es Salaam – Kilimo Hai cha Nyanya na Mbogamboga), na Evelyn Kahembe (Uvinza, Kigoma – Kilimo cha Matunda).
Kupitia
miradi hiyo, zaidi ya wanawake 300 wamepatiwa mafunzo mbalimbali huku
program nyingine za mafunzo kwa vitendo zikiendelea katika makundi yao.
“Serikali
ya Tanzania na hasa wizara hii, na wizara hii Mheshimiwa Rais mwenyewe
ni wizara yake, naomba niwahakikishie kwamba tutashirikiana na Green
Voices kwa nguvu zote na nitawapa pasiwedi ya kuwasiliana na ofisi yangu
moja kwa moja ili kama mnakwama mambo yenu yaweze kwenda huko katika
halmashauri mlipo,” alisema Jaffo, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la
Kisarawe mkoani Pwani.
Akaongeza:
“Nitawaunganisha na mkurugenzi maalum wa idara za serikali katika
wizara yangu, kwamba ninyi mkikwama katika halmashauri kwa jambo lolote
lile mnawasiliana naye moja kwa moja mradi mambo yenu yaweze kwenda
mpate sapoti, sauti ya wanawake iweze kusikika, mambo ya mazingira
yaweze kubadilika, kilimo, mifugo na kadhalika ili mwisho wa siku watu
waseme kwamba kuna kundi la watu walikwenda Hispania na wakajifunza
wakaleta mabadiliko nchini.”
Aidha,
Naibu Waziri Jaffo alisema kundi hilo la akinamama wa Green Voices ni
muhimu na serikali itahakikisha inawaunga mkono kwa kila hali.
"Ninyi
ni kioo cha jamii na watu wengi wanatakiwa wajifunze kutoka kwenu.
Kumbukeni, katika suala la mazingira maeneo mengi yameathirika sana,
mnaweza kuona jinsi maeneo mengi yanavyokumbwa na mafuriko kutokana na
watu kukata miti na kuharibu mazingira, wakati mwingine tunashuhudia
ukame wa kutisha.
“Kwahiyo
ninyi mradi wenu unakwenda kukabiliana na changamoto hizi, ni muhimu
sana, mna wajibu mkubwa sana kwa sababu suala la mazingira ni muhimu na
linaathiri dunia.
“Tunatakiwa
tutoke katika miradi isiyo halisi (artificial projects) na kwenda
kwenye miradi halisi ili tuweze kubadilisha maisha ya watu.”
Vile vile, aliwaasa akinamama hao kwamba, wakienda huko waongee lugha rahisi na wananchi ili iwe rahisi kueleweka.
“Ninyi
hapa wote ni wasomi, lakini mkienda huko ongeeni lugha rahisi ili
mwananchi wakawaida akisikia aweze kuielewa na kuleta mabadiliko ya
kweli. Mama mwingine hajasoma hata darasa moja na inawezekana kuwepo
kwako wewe kukabadili maisha yake,” alisema.
Naibu Waziri wa Tamisemi, Selemani Jaffo, akizungumza katika uzinduzi huo.
Secelela Balisidya akipokea cheti.
Mmoja
wa washiriki wa mradi wa Green Voices, Mariam Bigambo, mkulima wa
Mvomero ambaye amejikita katika ufugaji wa nyuki akiwa na kikundi cha
wanawake 15, alisema kwamba licha ya umuhimu wa mradi huo, lakini
wanakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinakwamisha maendeleo yao.
“Changamoto
kubwa tunayokabiliana nayo ni kushushwa kwa mizinga yetu na watu
wasiojulikana kwa sababu tumeiweka porini,” alisema na kuongeza: “Kila
mara tunakuta mizinga yetu imeshushwa, tumekwishatoa taarifa kwa
serikali ya kijiji pamoja na kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Mvomero na hata Polisi.”
Aidha,
alisema kwamba, ufugaji wa nyuki unahitaji uvumilivu na mpaka sasa
baadhi ya wanakikundi wamevunjika moyo kwa sababu bado hawajanufaika na
matunda ya kazi yao. Kutokana na hali hiyo, alisema, wameamua pia
kugeukia kilimo cha uyoga ili kuongeza tija.
Mratibu
wa mradi wa Green Voices nchini Tanzania, Secelela Balisidya, alisema
awamu ya kwanza ya mradi huo ililenga katika uanzishwaji na uzalishaji,
lakini awamu ya pili inalenga kuwapatia stadi akinamama ili kuboresha
bidhaa wanazozizalisha ili ziongezeke ubora la kuwaletea tija.
“Hivi
sasa katika awamu ya pili akinamama watapatiwa mafunzo ya namna ya
kutengeneza bidhaa zao kama vifungashio ili kuongeza ubora na thamani na
tunataka bidhaa zao ziingie sokoni katika viwango ambavyo
vinakubalika,” alisisitiza.
Akizungumza
katika uzinduzi huo wa awamu ya pili, Mratibu wa mradi wa Green Voices
kutoka Hispania kutoka taasisi ya Women for Africa Foundation
inayodhamini mradi huo, Alicia Cebada, alisema wamefarijika na mradi huo kwa kuwa umeonyesha mafanikio makubwa nchini Tanzania katika awamu ya kwanza na ndiyo maana wameamua kuwaongezea uwezo akinamama hao katika awamu hii.
“Tumekuwa
tukiwasiliana mara kwa mara na Secelela (Mratibu wa Green Voices
Tanzania) kuhusu mafanikio na changamoto za mradi huu na kwa kweli
tunafarijika kuona miradi yote inakwenda vizuri,” alisema Alicia.
Alisema,
changamoto pekee ambayo ipo mbele yao ni kuhakikisha miradi hiyo
inasimama na kuwafundisha wanawake wengi kadiri wawezavyo ili
kuhakikisha wanajiletea maendeleo katika maeneo yao kiuchumi na kijamii.
Mwaka
2016 rais wa mfuko wa Women for Africa Foundation, Mama Maria Tereza
Fernandez de la Vega, alizuru nchini Tanzania na kushiriki uzinduzi wa
mradi huo Julai 11, 2016 ambapo ulizinduliwa rasmi na Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan.
Katika
uzinduzi huo, Mama Samia aliahidi kwamba serikali yake itahakikisha
inakuwa bega kwa bega kusaidia miradi hiyo iwe endelevu ili kuunga mkono
juhudi za utunzaji wa mazingira na kupambana na mabadiliko ya
tabianchi, kuongeza uhakika wa chakula, kuwakwamua wananchi na umaskini
pamoja na kuongeza ajira, hasa kwa wanawake.
Kwa
upande wake, Mama Maria Tereza, ambaye ni makamu wa rais mstaafu wa
Hispania, alieleza kufurahishwa kwake na jitihada za akinamama wa
Tanzania na kusema taasisi yake inaangalia namna ya kuwasaidia zaidi.
Mratibu
wa Mradi wa Green Voices kutoka Hispania, Alicia Cedaba (kushoto) akiwa
na Leocadia Vedasto kutoka Ukerewe anayeratibu kilimo cha viazi lishe
pamoja na usindikaji wa bidhaa zake. Katikati ni mdau mwingine
aliyehudhuria uzinduzi wa awamu ya pili ya Mradi wa Green Voices
Tanzania.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni