MAGUFULI:MTANZANIA ALINDE NA KUIMARISHA MUUNGANO



Kila mtanzania ametakiwa kuhakikisha anafanya jitihada za kuimarisha na kulinda Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulioasisiwa miaka 53 iliyopita.

Akizungumza leo wakati akihutubia wananchi katika sherehe za Maadhimisho ya miaka 53 ya Muungano katika uwanja wa Jamhuri uliopo mjini Dodoma, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alisema kuwa ni muhimu watanzania wakalinda Muungano kwa vile una manufaa kwa nchi zote mbili.

“Kila mtanzania ahakikishe anafanya jitihada za kuimarisha na kulinda Muungano wetu, kwa vile Muungano na amani iliyopo nchini ndio chachu ya maendeleo yetu” alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli alisisitiza kuwa “Muungano ndio silaha yetu, ni nguvu yetu, mimi na mwenzangu Dkt. Shein tutaulinda Muungano kwa nguvu zote na yeyote atakayejaribu kuuvunja atavunjika yeye” alisema Rais Magufuli

Akitaja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika miaka 53 ya Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar ni pamoja na kuunganisha mataifa mawili na kuunda taifa moja lenye nguvu.

Rais Magufuli alitaja mafanikio mengine ni pamoja na kuwa ni kuimarisha miundombinu ya usafiri wa anga, majini, nchi kavu na reli, kukabiliana na matatizo ya umaskini, ukosefu wa ajira na kukua kwa uhusiano wa diplomasia kati ya Tanzania na mataifa mbalimbali ambapo yamepelekea mafanikio katika nyanja za kiuchumi, kisiasa, na jamii.

Aidha, hii ni mara ya kwanza kwa sherehe za Maadhimisho ya Muungano kufanyika mkoani Dodoma ambapo, Rais Magufuli alisema kuwa Serikali imeendelea kufanya jitihada mbalimbali za kujenga miundombinu ili kufikia azma yake ya kuhamishia makao yake makuu mjini Dodoma ifikapo mwaka 2020.

“Niwahakikishie wana Dodoma na Watanzania kwa ujumla kwamba Serikali sasa tumefika Dodoma na hatutarudi nyuma tena,ambapo awamu ya kwanza ya watumishi wa Serikali takribani 3,000 kwa ngazi za Mawaziri,Naibu Waziri,Makatibu wakuu na Manaibu Katibu wakuu wameshahamia Dodoma, kama tulivyoahidi kufikia mwaka 2020, Serikali yote itakuwa imehamia hapa”, alisisitiza Rais Magufuli.

Sherehe za Maadhimisho ya miaka 53 ya Muungano zenye kauli mbiu isemayo “Miaka 53 ya Muungano, tuulinde na kuimarisha, tupige vita dawa za kulevya na kufanyakazi kwa bidii”, zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali pamoja na wajane wa viongozi waasisi wa Muungano ambapo ni Mama Maria Nyerere na Mama Shadya Karume.

SERIKALI YAWATAKA WAAJIRI KUHAKIKISHA MITAMBO NA VIFAA VYA KAZI VINAFANYIWA UKAGUZI MARA KWA MARA.


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Vijana), Mhe. Antony Mavunde akitoa hotuba yake wakati wa mkutano na waandishi wa habari ulioandaliwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pa Kazi (OSHA) kuhusu maandalizi ya maadhimisho ya siku ya Usalama na Afya mahali pa kazi uliofanyika Aprili 25, 2017 Dodoma. Baadhi ya Watumishi wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pa Kazi (OSHA) wakimsikiliza Naibu wake Ofisi ya Waziri Mkuu Mhe. Antony Mavunde (hayupo pichani) wakati wa Mkutano wa waandishi wa habari ulioandaliwa na Ofisi hiyo ikiwa ni maandalizi ya ya maadhimisho ya siku ya Usalama na Afya mahali pa kazi uliofanyika Mjini Dodoma. Kaimu Mtendaji Mkuu OSHA Bi. Khadija Mwenda akizungumza wakati wa mkutano na Waandishi wa habari juu ya maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Usalama na Afya mahali pa Kazi uliofanyika Mjini Dodoma Aprili 25, 2017. Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Bw.Peter Kalonga akichangia hoja wakati wa Mkutano na waandishi wa habari juu ya maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Usalama na Afya mahali pa Kazi uliofanyika Mjini Dodoma Aprili 25, 2017. Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Vijana), Mhe. Antony Mavunde akisalimiana na Mwakilishi wa TUCTA Bw.Ramadhani Mwenda mara baada ya mkutano wa waandishi wa habari Aprili, 25, 2017 DodomaNaibu wake Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Vijana), Mhe. Antony Mavunde (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watendaji wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA)mara baada ya kumaliza mkutano na waandishi wa habari Aprili 25, 2017 Mjini Dodoma. (PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU-DODOMA)

Na. Mwandishi Wetu- Dodoma

Serikali imewataka waajiri wote na wadau kwa ujumla kuhakikisha kuwa sehemu za kazi, mitambo na vifaa vya kufanyia kazi vinafanyiwa ukaguzi mara kwa mara ili kuhakikisha kuwa havileti madhara kwa wafanyakazi.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Ajira na Vijana Mhe. Antony Mavunde wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo mjini Dodoma kuhusu maandalizi ya maadhimisho ya siku ya Usalama na Afya mahali pa kazi.

“Kwa upande wa Serikali jukumu letu kubwa ni kuweka na kusimamia sera ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi, kutunga na kusimamia Sheria za Usalama na Afya Mahali pa Kazi, na kuweka viwango mbalimbali vya usalama na afya sehemu za kazi” alisisitiza Mavunde.

Mavunde alisema kuwa kwa sasa kanuni ya kuripoti ajali na magonjwa imekamilika na kuanza kutumika tangu mwezi Septemba, mwaka 2016.

Ambapo ameshauri wafanyakazi kuwasaidia waajiri wao kusimamia mifumo iliyopo, kujilinda wao binafsi ili wasiumie ama wasipate magonjwa yatokanayo na kazi sambamba na kutumia ipasavyo vifaa vyote vya kujikinga wawapo kazini.

Mavunde alisema kuwa serikali inaendelea kuboresha mfumo wa ukusanyaji takwimu za ajali na magonjwa yatokanayo na kazi, hivyo bado kuna changamoto ya kupata taarifa kuhusu ajali na magonjwa yatokanayo na kazi hii inatokana na waajiri wengi kutoripoti taarifa hizo kama sheria inavyoelekeza.

kwa mantiki hiyo Serikali inaandaa mfumo ambao utaongea na mifumo mingine ili kupata taarifa za ajali na magonjwa.

Aliongeza kuwa “Serikali kupitia Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) imejipanga kuhakikisha kuwa Usalama na afya za wafanyakazi hao zinalindwa kwa kuhakikisha kuwa waajiri wanazingatia taratibu zote za Usalama na Afya kwa mujibu wa sheria na 5 ya Mwaka 2003, ili kulinda nguvu kazi ya taifa hili”.

Aidha, tarehe 28 Aprili ya kila mwaka, Tanzania inaungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku ya Usalama na Afya Mahali pa kazi ili kuwakumbuka wahanga wa majanga yanayotokea sehemu za kazi.

Madhumuni makubwa ya kuadhimisha siku hii ni kuendesha kampeni ya Kimataifa ya kuboresha usalama na afya kazini na kuhamasisha utengenezaji ajira zenye staha. Kwa kuhamasisha waajiri na wafanyakazi na umma kwa ujumla kuchukua hatua za makusudi ili kuhakikisha kuwa suala la ajali na magonjwa yatokanayo na kazi yanapungua au kutotokea kabisa sehemu za kazi.

Maadhimisho ya mwaka huu yanatarajia kufanyika Moshi Mkoani Kilimanjaro kwa kujumuisha shughuli hizo kuanzia tarehe 25 hadi tarehe 27 ambapo yatatanguliwa na kongamano la wadau wa Usalama na Afya.

ZANZIBAR YAJIANDAA KUMALIZA KABISA MALARIA 2023

Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar Dkt, Fadhil Mohd Abdalla akimkaribisha Naibu Waziri wa Afya Harusi Said Suleiman kuzungumza na waandishi wa habari katika maadhimisho ya siku ya Malaria Duniani katika ukumbi wa Wizara ya Afya Mnazimmoja Mjini Zanzibar. 
Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Bi. Harusi Said Suleiman akizunguza na waandishi wa habari katika maadhimisho ya siku ya Malaria Dunia katika ukumibi wa mikutano wa Wizara ya Afya Mnazimmoja Mjini Zanzibar. 
Mwandishi wa habari wa ITV/Radio One Farouk Karim akiuliza swali katika maadhimisho hayo yaliyofanyika kwa mkutano wa waandishi wa habari katika Wizara ya Afya Mnazimmoja. Meneja Kitengo cha Kumaliza Malaria Zanzibar Mwinyi Issa Khamis akijibu maswali ya waandishi wa habari katika maadhimisho ya siku ya malaria yaliyoadhimishwa kwa mkutano wa waandishi wa habari Wizara ya Afya Zanzibar .Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar.

Na Ramadhani Ali/Maelezo Zanzibar

Naibu Waziri wa Afya Harusi Said Suleiman amesema pamoja na mafanikio makubwa katika kupambana na Malari Zanzibar, bado shehia tano zinaendelea kutoa wagonjwa wa maradhi hayo zaidi ya asilimia tano.

Akizungumza na waandishi wa habari katika maadhimisho ya siku ya Malaria Dunia katika ukumibi wa mikutano wa Wizara ya Afya Mnazimmoja, amezitaja shehia hizo kuwa ni Tumbatu Jongowe, Miwani, Micheweni, Chukwani na Kiwengwa.

Hata hivyo amesema maambukizi ya malaria katika maeneo hayo yanasababishwa na wasafiri wanaoingia na kutoaka nje ya Zanzibar mara kwa mara ambapo mwaka jana asilimia 55 ya wagonjwa waliogundulika walikuwa na tabia hiyo.

Amesema takwimu za Malaria Zanzibar zinaonyesha mafanikio mazuri ambapo mtu mmoja kati ya watu mia moja hupata ugonjwa huo katika jamii isipokuwa shehia hizo tano.

Naibu Waziri wa Afya amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga na Malaria ikiwemo kutumia vyandarua vilivyotiwa dawa na kusafisha mazingira kwa lengo la kuondosha mazalio ya mbu wanaoeneza maradhi hayo.

Ameongeza kuwa Serikali kwa upande wake mwaka jana iligawa vyandarua 705,000 bila malipo na kufanya zoezi la kupiga dawa nyumba za wananchi ya kukinga malaria bila ya kuangalia vyeo vya wamiliki wa nyumba hizo licha ya kukabiliana na changamo nyingi katika kazi hiyo.

Amesema baadhi ya wananchi wamekuwa wakikataa kupigiwa dawa nyumba zao kwa madai kwamba zinawaletea athari za afya jambo ambalo halina ukweli kwani dawa hiyo ni salama kwa afya.

Amekubusha kuwa Sheria ya Afya ya Jamii na Mazingira ya mwaka 2012 pamoja na mambo mengine inasisitiza juu ya udhibiti wa mbu na mazingira hivyo wananchi watakaokataa kupigiwa dawa sheria itawabana.

“Watu wanaokataa nyumba zao kupigiwa dawa ya kukinga maluaria bila sababu za msingi zinazokubalika, sheria hii itawabana na hatua muafaka zitachukuliwa dhidi yao, ” alisisitiza Naibu Waziri.

Meneaja Kitengo cha kumaliza malaria Mwinyi Khamis alisema Zanzibar imeweka mikakati ya kumaliza kabisa malaria ifikapo mwaka 2023 hivyo juhudi za jamii na Wizara ya Afya ni muhimu.

Amesema mwaka jana watu watano walibainika kufa kwa malaria Zanzibar wakiwemo watoto wawili wenye umri chini ya miaka mitano.

Mapema akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Kinga na Elimu ya Afya Dkt. Fadhil Mohd amewashauri wananchi wasikubali kula dawa ya malaraia bila kupimwa na kuthibitishwa kuwa wanayo malaria.

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu inasema Malaria bado ipo Zanzibar, chukua tahadhari.

EfG YAPONGEZWA KUFUNGUA KLABU ZA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA SOKO LA ILALA BOMA JIJINI DAR ES SALAAM


Mfanyabiashara wa nguo za mitumba ya kike katika Soko la Ilala Boma jijini Dar es Salaam, Daud Omary (kushoto), akitoa maelezo Dar es Salaa jana ya vitendo vya ukatili wa kijinsia wanavyofanyiwa na baadhi ya askari polisi wa Kituo cha Pangani kwa Mwezeshaji wa kisheria katika soko hilo (kulia) kutoka Shirika la Equality for Growth (EfG), wakati wa uhamsishaji wa kufungua klabu za mabadiliko ya kupinga ukatili wa kijinsia masokoni unaofanywa na Shirika hilo kwa kusimamiwa na Kituo cha Msaada wa Kisheria kwa Wanawake Tanzania (WLAC) kupitia kampeni ya miezi miwili ya Tunaweza. Katikati ni mfanyabiashara Seleman Adam.
Fundi ushonaji nguo katika Soko la Ilala Boma, Abdallah Omari (kulia), akitoa maelezo kwa mwezeshaji sheria kutoka Shirika la EfG, Aisha Juma wakati wa kujiunga na klabu ya mabadiliko ya wapinga ukatili wa kijinsia.
Fundi ushonaji nguo katika Soko la Ilala Boma, Hamisi Bweni (kulia), akitoa maelezo kwa mwezeshaji sheria kutoka Shirika la EfG, Aisha Juma wakati wa kujiunga na klabu ya mabadiliko ya wapinga ukatili wa kijinsia.
Mama Lishe, Zaina Amri (kushoto), akijieleza kwa mwezeshaji wa sheria, Irene Daniel, wakati akijiunga na klabu hiyo.
Wafanyabiashara katika soko hilo wakijiunga na klabu hiyo. Kutoka kulia ni Fatuma Bayuni, Ibrahim Said na kushoto ni mwezeshaji wa kisheria Irene Daniel kutoka EfG.
Mama Lishe Sauda Mwinyi akisoma kipeperushi kabla ya kujiunga na klabu ya mabadiliko.
Mama Lishe Wanamabadiliko wakiweka bango la kupinga ukatili huo. Kulia ni Fatuma Bayuni na Zaina Amri.
Mwezeshaji wa Kisheria masokoni, Irene Daniel (kulia), pamoja na wanamabadiliko wa Soko la Ilala Boma, wakionesha vipeperushi vya kupinga ukatili wa kijinsia masokoni. Kutoka kushoto ni Zaina Amri, Ibrahim Saidi na Fatuma Bayuni.

Na Dotto Mwaibale

WAFANYABIASHARA katika Soko la Ilala Boma jijini Dar es Salaam wamelipongeza Shirika la Equality for Growth (EfG) kwa kuwahamasisha kufungua klabu za kupinga ukatili wa kijinsia masokoni.

Wakizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, walisema kufunguliwa kwa klabu hizo kutawasaidia kwa karibu kukabiliana na vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia vinavyofanyika katika soko hilo na mengine.

“Binafsi nalipongeza shirika hili kwa hatua hii nzuri waliofikia ya kutuhamasisha kuwa mabalozi wa kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia na kutusogezea huduma hii karibu ambayo itapunguza kama sio kumaliza kabisa vitendo vya ukatili masokoni” alisema Abdallah Omari ambaye ni mshonaji nguo katika soko hilo.

Omari alisema changamoto kubwa waliyokuwa nayo ni wapi walipaswa kutoa taarifa za ukatili huo wa kijinsia kwani wengi wao walikuwa hawajui lakini kwa kuanzishwa klabu hizo na kuwa na namba za wawezeshaji wa kisheria kwao milango ya utoaji wa taarifa hizo sasa imefunguliwa.

Mfanyabiashara wa kuuza nguo za mitumba za kike katika soko hilo, Daud Omari alisema kuna baadhi ya polisi kutoka kituo cha Pangani wamekuwa wakiwafanyia ukatili wa kijinsia pale wanapoenda kuwakamata na kuanza kuwapiga na kibaya zaidi wanakuwa hawajitambulishi mpaka wanapofika kituoni.

“Unajua hapa sokoni kunakuwa na mambo mengi hasa pale tunapopishana na wenzetu na kwenda kushitaki polisi wakifika wao uanza kupiga watu bila ya kujitambulisha na ukifika polisi ndipo wanajitambulisha kuwa wao ni polisi kitendo hicho kwetu tunahesabu kuwa ni ukatili wa kijinsia tunaofanyiwa na askari hao” alisema Omari.

Omari Lubuva mfanya biashara katika eneo hilo alisema mtu anapotoa oda ya chakula kwa mama lishe akipelekewa anapo muambia mama lishe husika kuwa ondoka na chakula chako umekichelewesha nimemuagiza mwingine aniletee huo ni ukatili wa kijinsia dhidi ya mama lishe.

Aliwaomba wafanyabiashara wenzake wenye tabia hiyo kuacha kufanya hivyo kwani jambo hilo ni ukatili mbaya kwa mama lishe hao.

Seleman Adam aliwapongeza EfG kwa hatua walioifikia ya kuwasogezea huduma hiyo kwa mara nyingine hivyo akayaomba mashirika mengine kujitokeza kusaidia wananchi katika maeneo mengine kwani katika jamii kuna changamoto nyingi.

Mwanasheria wa Shirika hilo, Muna Abdallah alisema muitikio wa kufungua klabu za mabadiliko za kupinga ukatili wa kijinsia katika masoko waliyoyatembelea ni mkubwa mno.

“Kwa kweli watu wengi wameonesha kuchoshwa na vitendo hivyo na wamepokea kwa mikono miwili mradi huu tuliouanzisha wa kufungua klabu za mabadiliko za kupinga ukatili wa kijinsia masokono” alisema Abdallah.

Mratibu wa mradi huo ambaye pia ni Mwanasheria wa Shirika hilo, Mussa Mlawa alisema msimamizi mkuu wa mradi huo kupitia kampeni ya Tunaweza ni Kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wanawake Tanzania (WLAC) lakini EfG wao wanaiendesha kampeni hiyo ya miezi miwili katika masoko matano yaliyopo jijini Dar es Salaam ambayo ni Ilala Boma, Ferry, Mchikichini, Temeke Sterio na Buguruni.

Alisema lengo kubwa la mradi huo ni kuwa na wanamabadiliko masokoni ambao watasaidia kupambana na vitendo hivyo si katika maeneo ya masoko pekee bali hata majumbani kwa jamii.

MTOTO WA MIAKA MIWILI ALIYEKUWA AKIVUTA SIGARA 40 KWA SIKU AACHA KUVUTA SIGARA


Mtoto wa kiume wa miaka miwili aliyekuja kuwa maarufu kimataifa baada ya kuwa na tabia ya kuvuta zigara katika kijiji kimoja nchini Indonesia ameacha tabia hiyo na kupungua uzito na sasa amekuwa anafanya vizuri katika shule anayosoma.

Mtoto huyo Aldi Rizal alipata umaarufu mnano mwaka 2010 alipogundulika katika kijiji kimoja masikini huko Sumatra, Indonesia, akivuta sigara 40 kwa siku huku akiendesha kigari cha watoto.

Miaka miwili baadaye mtoto huyo aliacha tabia hiyo ya uvutaji sigara kwa msaada wa serikali ya Indonesian kwa kumpatia tiba maalum ya kuondokana na tabia hiyo, na kufanikiwa kuachana kabisa na uvutaji sigara.
                                    Mtoto Aldi Rizal akivuta sigara yake huku akiendesha kigari cha watoto
                            Mtoto Aldi Rizal anavyoonekana sasa akiwa na umri wa mika tisa 
                  Mtoto Aldi Rizal akicheza shuleni hivi sasa amekuwa ni mwenye tabia nzuri 

MAONESHO YA WIKI YA USALAMA NA AFYA KAZINI 2017 MKOANI KILIMANJARO

Maonesho ya wiki ya usalama na afya kazini yameanza leo siku ya Jumatano tarehe 26/04/2017 katika viwanja vya Ushirika mjini Moshi mkoani Kilimanjaro ambapo taasisi mbalimbali za serikali na binafsi zimepata fursa ya kuonyesha namna zinavyozingatia masuala ya usalama na afya kazini kwa wafanyakazi wao.

Miongoni mwa taasisi zilizopata fursa ya kushiriki maonyesho hayo kwa mwaka huu ni pamoja na kampuni za uchimbaji wa madini za Bulyanhulu, Buzwagi na North Mara ambazo zinamilikiwa na kampuni ya uchimbaji ya Acacia.

Ambapo katika maonesho hayo migodi hiyo ya imekuwa ikionesha vifaa mbalimbali vya uokozi pamoja pamoja na mbinu zitumikazo kuhakikisha mazingira ya usalama kwa wafanyakazi wao wawapo kazini.

Maadhimisho ya mwaka huu ya siku ya afya na usalama mahali pa kazi yameandaliwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) yakiwa na kauli mbiu ya “ Ongeza wigo wa ukusanyaji na utumiaji wa takwimu za usalama na afya” .Maadhimisho hayo yanatarajiwa kufikia kilele chake Aprili 28,2017.

Zifuatazo ni picha mbalimbali wakati wa maonesho hayo siku ya kwanza Aprili 26,2017

Banda la mgodi wa Bulyanhulu-Maafisa kutoka mgodi wa Bulyanhulu wakiandaa kupokea wageni mbalimbali
Maandalizi yanaendelea
Maafisa kutoka mgodi wa Bulyanhulu
Msaidizi wa Meneja Mkuu wa mgodi wa Acacia Bulyanhulu Margaret Mandia akimkaribisha Mkaguzi wa Mitambo Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kanda ya Kaskazini Boysafi Sabato katika banda la mgodi wa Bulyanhulu
Mkaguzi wa Mitambo Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kanda ya Kaskazini Boysafi Sabato akifurahia jambo baada ya kufika katika banda la mgodi wa Bulyanhulu
Afisa Mazingira mgodi wa Bulyanhulu Florence Nyuki akimwelezea Mkaguzi wa Mitambo Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kanda ya Kaskazini Boysafi Sabato namna mgodi huo unavyotunza mazingira na kuhakikisha usalama unakuwepo katika maeneo yao ya kazi
Afisa Mazingira mgodi wa Bulyanhulu Florence Nyuki akitoa ufafanuzi kwa mwananchi aliyefika katika banda la mgodi wa Bulyanhulu
Afisa uhakiki wa usalama kutoka mgodi wa Bulyanhulu Amina Mohamed akimwelezea kuhusu masuala ya usalama mgodini kwa mmoja wa wananchi waliofika katika banda hilo
Afisa Mazingira mgodi wa Bulyanhulu Florence Nyuki akitoa maelezo kwa maafisa kutoka shirika la Umeme nchini Tanzania (TANESCO) waliotembelea banda hilo
Wananchi wakiwa katika banda la mgodi wa Bulyanhulu
Afisa rasilimali watu mgodi wa Bulyanhulu Mwanaisha Mosha akiwaelezea watalii kuhusu DVD ya Bulyanhulu inayohusu usalama mgodini na mahusiano ya jamii
Afisa viwango vya usalama mgodi wa Bulyanhulu Setieli Kimaro akitoa elimu kuhusu mambo ya usalama mgodini kwa wananchi waliotembelea banda la la mgodi wa Bulyanhulu
Mdau kutoka Mgodi wa Williamson Diamonds Limited Gamba Isack akiangalia bango kubwa lililopo katika banda la mgodi wa Bulyanhulu
Wananchi wakiwa katika banda la mgodi wa Bulyanhulu
Afisa afya mgodi wa Bulyanhulu Tumaini Sylvanus akielezea kuhusu masuala ya afya mgodini
Afisa Mahusiano mgodi wa Bulyanhulu William Chungu akifurahia jambo na mwananchi aliyembelea banda la mgodi wa Bulyanhulu
Mhandisi wa uchimbaji mgodi wa Bulyanhulu Fikiri Thomas akiwaonesha wananchi namna wanavyochimba madini
Banda la mgodi wa Buzwagi- Maafisa kutoka mgodi wa Buzwagi wakijiandaa kwa ajili ya maonesho
Nje ya banda la mgodi wa Buzwagi
Mkufunzi Idara ya Uokozi mgodi wa Buzwagi Azaeli Kitange akitoa elimu kuhusu usalama mgodini kwa wananchi waliotembelea banda la mgodi wa Buzwagi
Maandalizi yanaendelea
Afisa usalama na afya mgodi wa Buzwagi Mustapha Mlewa akiwaelezea wananchi kuhusu namna mgodi huo unavyojitahidi kuhakikisha wafanyakazi wake wanakuwa salama mgodini
Mwananchi akiuliza swali kwa maafisa kutoka mgodi wa Buzwagi
Mkufunzi Idara ya Uokozi mgodi wa Buzwagi Azaeli Kitange akimwonesha mwananchi aliyetembelea banda la mgodi huo vifaa vinavyotumika katika uokoaji mgodini
Afisa usalama na afya mgodi wa Buzwagi Mustapha Mlewa akitoa somo kwa wananchi waliotembelea banda la mgodi wa Buzwagi
Afisa Usalama na afya mgodi wa Buzwagi Deogratius Nyantabano akimwelezea mwananchi namna mgodi huo unavyojitahidi kuhakikisha wafanyakazi wake wanakuwa salama kazini
Afisa Usalama na afya mgodi wa Buzwagi Deogratius Nyantabano akiendelea kutoa elimu kwa wananchi
Afisa Usalama na afya mgodi wa Buzwagi Deogratius Nyantabano akieleza jambo kwa mwananchi aliyetembelea banda la mgodi wa Buzwagi
Dkt. Ludovick Silima kutoka mgodi wa Buzwagi akitoa elimu ya usalama kwa wananchi waliotembelea banda la mgodi huo
Dkt. Ludovick Silima kutoka mgodi wa Buzwagi akielezea masuala ya afya kwa wananchi waliotembelea banda la mgodi wa Buzwagi
Wananchi wakiwa katika banda la mgodi wa Buzwagi
Banda la Mgodi wa North Mara- Maafisa kutoka mgodi wa North Mara wakijiandaa kuanza kufanya maonesho
Afisa usalama mgodi wa North Mara Samwel Nyansika akimwelezea masuala ya usalama mgodini mwananchi aliyetembelea banda hilo
Kulia ni Mratibu wa Huduma za Afya na Matibabu mgodi wa North Mara Dkt. Robert Mazengo akiwaeleza wananchi kuhusu masuala mbalimbali ya afya mgodini
Kiongozi wa awali Idara ya Mahusiano mgodi wa North Mara Annamaria Baisi akitoa somo kwa wananchi waliotembelea banda la mgodi huo
Mratibu wa Huduma za Afya na Matibabu mgodi wa North Mara Dkt. Robert Mazengo akimwonesha mwananchi kifaa kinachotumika kubaini ulevi kwa wafanyakazi wanaoweza kufika kazini huku wamelewa
Afisa usalama na afya mgodi wa North Mara Athanas Fredrick akiwaelezea masuala ya usalama mgodini wanafunzi waliotembelea banda la mgodi huo
Mwananchi akitembelea banda na mgodi wa North Mara
Mratibu wa Huduma za Afya na Matibabu mgodi wa North Mara Dkt. Robert Mazengo akitoa elimu kwa wanafunzi wa shule za msingi waliotembelea katika banda hilo
Afisa Mazingira mgodi wa North Mara Sara Cyprian akimwelezea mwanannchi namna mgodi huo unavyotunza mazingira
Afisa usalama na afya mgodi wa North Mara Alfred Mwema akitoa elimu kwa mwananchi aliyetembelea banda hilo
Mratibu wa Huduma za Afya na Matibabu mgodi wa North Mara Dkt. Robert Mazengo akimpima kilevi mmoja wa wananchi waliotembelea banda hilo wakati akiwaelezea namna wanavyopima wafanyakazi mgodini
Kiongozi Idara ya Mahusiano Jamii mgodi wa North Mara Fatuma Mssumi akielezea masuala mbalimbali kuhusu mgodi huo katika kuimarisha afya na usalama kazini.  Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog