MVUA KUBWA YASITISHA USAFIRI WA NDEGE NA TRENI NCHINI INDIA

Mvua zilizoanza upya katika mji wa Chennai kusini wa India zimesababisha mafuriko makubwa na kusababisha ndege na treni kusitisha usafirishaji na mamia kuachwa bila umeme.

Jeshi la India limepelekwa katika mkoa huo kuwaokoa maelfu ya watu waliokwama baada ya mvua kunyesha kwa siku mbili.

Watu wapatao 188 wamethibitishwa kufa kutokana na mafuriko katika jimbo la Tamil Nadu tangu mwezi uliopita.
                   Wanafamilia wakimsaidia kumuokoa mwanamke mwenye ulemavu
      Wananchi wakiwa kwenye boti huku polisi wakilisukuma kuwavusha kwenye mafuriko.

UINGEREZA KUAMUA IWAPO WATAUNGA MKONO NCHI YAO KUWASHAMBULIA IS

Wabunge wa Uingereza wataamua iwapo wataunga mkono mashambulizi ya anga dhidi ya wapiganaji wa kundi la Dola ya Kiislam (IS) nchini Syria.

Wabunge watajadili suala hilo kwa saa 10 katika bunge la makabwela, iwapo Uingereza ijiunge na nchi za Marekani, Ufaransa, Urusi na nyinginezo kushambulia mji wa Raqqa ambao ndio ngome ya IS pamoja na maeneo mengine.

Waziri Mkuu wa Uingereza Bw. David Cameron amesema kundi la IS ni tishio kwa usalama wa nchi hiyo pia.

PICHA YA PAPA FRANCIS AKIWA AMESHIKA MIC KAMA RAPA YAPATA UMAARUFU

Picha ya Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis iliyopigwa akiwa katika pozi la mithili ya mwanamuziki wa rap akiwa nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) imesambazwa mara nyingi kwenye mitandao ya jamii.

Picha hiyo iliyojizolea umaarufu kwa sasa duniani ilipigwa wakati Papa Francis akitoa hotuba katika Jiji la Bangui, ime-twitiwa mara 100,000.

Watumiaji wa twitta wamekuwa wakitengeneza mistari yao kuendana na pozi la Papa Francis.
Twitti hizo za mistari kadhaa ya kubuni zinakwenda na #PopeBars.

KENYA YASHIKA NAFASI YA TISA KWA RUSHWA KATIKA NCHI ZA AFRIKA

Nchi ya Kenya imeshika nafasi ya tisa kwa vitendo vya rushwa kati ya mataifa 28 katika eneo la jangwa la Sahara, kwa mujibu wa utafiti mpya wa rushwa uliotolewa taasisi za Transparency International pamoja na AfroBarometer.

Kwa mujibu wa utafiti huo wananchi wengi wa Kenya ambao ni zaidi ya asilimia 60, wanaamini kuwa tatizo la rushwa limeongezeka nchini humo katika miezi 12 iliyopita. Aidha nchi za Madagascar, Liberia na Zimbabwe zinaongoza kwa rushwa.

Rushwa imejikita zaidi katika jeshi la polisi, mahakamani pamoja wakati wa kutafuta nyaraka mbalimbali kama vile vitambulisho pamoja na vibali.

Mataifa mengine yaliyohusikakatika utafiti huo wa rushwa ni pamoja na Nigeria, Zimbabwe, Liberia, Ghana, Benin, Sierra Leone, Uganda, Tanzania pamoja na Madagascar.

SERIKALI KUTUMIA TSH. BILIONI 5 KUHUDUMIA KAMBI ZA MADAKTARI BINGWA WA MOYO

Na Nyakongo Manyama -MAELEZO
Dar es salaam

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imetenga kiasi cha Tsh. Bilioni 5 katika mwaka 2015/16 kwa ajili ya kuhudumia kambi za Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za matibabu ya magonjwa hayo kwa Watanzania.
 

Lengo la mkakati huo ni kuhakikisha Wagonjwa wengi wanahudumiwa katika kipindi kifupi pamoja na kupunguza gharama za kusafirisha wagonjwa nje ya nchi, ambao wengi wao husafiri kwa ajili ya matibabu ya magonjwa ya moyo, figo na saratani.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Donald Mmbando wakati wa ziara yake ya kutembelea Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete iliyopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Dkt. Mbando alisema katika wiki ya kwanza iliyoanza wiki hii Madaktari hao wanatarajia kutoa huduma kwa wagonjwa 20 na kuifanya Serikali kuokoa kiasi cha Tsh. Milioni 500 ambazo zingetumika kuwasafirisha wagonjwa hao nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.
 

“Tumeokoa kiasi cha Tsh. Bilioni 1 zilizopaswa kutumika kuwapeleka nje ya nchi wagonjwa hawa, tutahakikisha kuwa Wataalamu hawa wanafanya kazi kwa pamoja na Madaktari wetu ili waweze kuwajengea uwezo katika kutibu magonjwa haya” alisema Dkt. Mmando.
Alisema Serikali pia ipo katika mchakato wa kuzijengea uwezo hospitali mbalimbali nchini ikiwemo Taasisi ya Kansa ya Ocean Road na Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) kwa kuziwezesha hospitali hizo kuwa na Wataalamu na majengo ya kisasa kwa ajili ya kutoa huduma za matibabu kwa Watanzania.
Aidha alisema Serikali imepanga kufanya mazungumzo na taasisi za kiraia na nyingine ikiwemo taasisi ya Rotary Club zilizokuwa zikisafarisha watoto wenye matatizo ya ugonjwa wa moyo, kuwekeza nguvu nchini kwani Tanzania kwa sasa ina wataalamu wa kutosha kwa ajili ya kuwatibu wagonja hao.
Kwa mujibu wa Mmbando alisema magonjwa ya moyo ni miongoni mwa magonjwa yasiyoambukiza, hivyo aliwataka Watanzania kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara na kuacha kunywa pombe na uvutaji wa sigara na kutazama desturi za ulaji.
Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Prof. Mohammed Janabi alisema katika kipindi cha wiki mbili ambazo madaktari hao watakuwepo hapa nchini wanaweza kuhudumia jumla ya wagonjwa 55, na hivyo kuifanya Serikali kuokoa kiasi cha Tsh. Bilioni 1.2

TUMIENI TEKNOLOJIA YA MAWASILIANO-MKURUGENZI MTENDAJI WA TaGLA

Na Anna Nkinda – Maelezo
WATANZANIA wametakiwa kutumia technolojia ya mawasiliano ikiwemo kufanya mikutano kwa njia ya video ambayo itawaondolea gharama ya kusafiri na hivyo kuokoa fedha  na muda.

Rai hiyo imetolea   hivi karibuni na Mkurugenzi Mtendaji wa TaGLA Charles Senkondo wakati akiongea na waandishi wa habari wakati wa mkutano wa kazi wa video conference kati ya Ofisi ya Rais  Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Taasisi zake, Sekretarieti za mikoa na Mamlaka za Serikali za mitaa.

Senkondo alisema kufanya mikutano kwa njia ya video kunamfanya mtu asisafiri na hivyo kuepukana na ajali, kutopoteza muda awapo safarini na na kupata wasaa wa  kukaa na familia yake.

“Kuanzishwa kwa TaGLA kumeongeza uwezo wa kufanya kazi kwa ubunifu zaidi, kwa njia ya kisasa, kwa maamuzi zaidi ya kiuendeshaji kwa kuangalia kila mara mahitaji ya wadau na kutumia mbinu za soko katika utoaji wa huduma bora”.

“Kabla ya kukuwa kwa teknolojia watu walikuwa wanasafiri umbali mrefu kwenda kushiriki mikutano hivi sasa wamepunguza safari zisizo na umuhimu.  Mtu atasafiri katika mikutano ya umuhimu tu zamani ilikuwa lazima mtu aje sasa hivi anafuatwa popote alipo na kuletwa katika video conference”, alisema Senkoro.

Akiongelea kuhusu kituo hicho Mkurugenzi huyo alisema zaidi ya washiriki elfu 20 wameshiriki midaharo na mafunzo 783 ya  kubadilishana maarifa kupitia Wakala wa Mafunzo kwa njia ya Mtandao (TaGLA) .

Senkondo alisema wakala hiyo imeweza kutoa mafunzo kwa viongozi wakiwemo mawaziri, wakuu wa taasisi mbalimbali za umma na binafsi na kuleta urahisi wa vikundi na watu waliotengwa kijiografia kuonana, kusikilizana na kukubaliana kwa wakati mmoja.

“Wakala kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa kutumia mitandao ya teknolojia imeweza kufundisha watendaji wakuu wa Taasisi za Serikali, wakurugenzi wa Halmashauri za wilaya zote na wakurugenzi wa rasilimali watu wapatao 1,200 mfumo wa malipo ya mishahara kwa watumishi wa Serikali (HCMIS) Lawson version 7”, alisema Senkoro.

Mkurugenzi  huyo mtendaji alizitaja changamoto wanazokabiliana nazo kuwa ni fikra potofu juu ya matumizi ya TEHAMA na kukubalika kwa kasi kwa teknolojia  na kuwaomba waandishi wa habari pamoja na wadau wengine kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa matumizi ya Tehama.
Senkoro alisisitiza, “Tunawaalika wadau mbalimbali wakiwemo taasisi za Serikali na zisizo za kiserikali, waandishi wa habari, watu binafsi na asasi za jamii watumie huduma zetu ambazo tunazitoa kwa gharama naafuu kuweza kuwafikia wadau wengi kwa muda mfupi bila kujali umbali au changamoto za kijiografia. 

Wakala wa Mafunzo kwa njia ya Mtandao umewezesha kufanyika kwa mahakama kwa kutumia mikutano ya video katika kesi mbalimbali kwa kutoa ushahidi wake kwa njia ya video na kusaidia kupunguza gharama  na kuhamasisha maamuzi na hivyo utoaji wa haki katika kesi husika.

Mkutano huo wa kazi wa video conference kati ya Ofisi ya Rais  Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Taasisi zake, Sekretarieti za mikoa na Mamlaka za Serikali za mitaa ulijumuisha viongozi wa Serikali kutoka mikoa ya Dodoma, Lindi, Geita, Singida, Pwani, Mara, Iringa, Mtwara, Shinyanga na Njombe.

POP UP BONGO ILIVYOFANA, TRINITI BAR OYSTERBAY CHINI YA UDHAMINI WA SMIRNOFF

Co- founder wa Pop Up Bongo Natasha Stambuli akionesha bidhaa za duka lake la Secret Habit ambalo nalo lilionesha bidhaa zake siku hiyo.
Andrew Mahiga na rafiki ake walikuwapo.
Mmoja kati ya wanawake wajasiriamali mahiri mjini, Aika Lawere mmiliki wa Mbezi Garden alikuwapo pia.
Mbunifu wa mavazi nchini wa lebo ya Branoz Collection, Bahati Kombe (kulia) akipanga bidhaa zake wakati wa Tamasha la Pop Up Bongo lililofanyika juzi Triniti Oyster bay chini ya udhamini wa kinywaji cha Smirnoff. 
Meneja chapa (Pombe kali) wa kampuni ya bia ya Serengeti (SBL) Shomari Shija, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) 
Wauzaji wa bidhaa mbalimbali kutoka duka la Beauty Haven wakiwa kwenye banda lao wakati wa Tamasha la Po Up Bongo lililofanyika juzi Triniti Oyster bay chini ya udhamini wa kinywaji cha Smirnoff.
Tanya akiwa na wadau mbalimbali waliojitokeza kwenye Pop Up shop .
Atu Mynah akimtaja mshindi wa bahati nasibu siku hiyo. 
Kutokea banda la Beauty Heaven kulikuwa na bidhaa mbalimbali pia.
Natasha akizungumza na mmoja kati ya washiriki waliojitokeza kuonesha bidhaa siku hiyo.
Na Mwandishi Wetu
ONESHO la mauzo ya bidhaa mbalimbali zitengenezwazo na wabunifu wa hapa nchini, Pop Up Bongo lilifanyika hivi karibuni na kuhudhuriwa na watu mbalimbali.


Mratibu wa onesho hilo lililofanyikia Triniti Oyster bay,Natasha Stambuli alisema kuwa zaidi ya wajasiriamali 15 walijiotokeza kuonesha na kuuza bidhaa zao.

Alisema kuwa bidhaa mbalimbali kama vile nguo, vito, viatu na vinginevyo viliuzwa na wajasiriamali hao walipata wasaha wa kuongeza wigo wao kibiashara kwa kukutana na wanunuzi.
"Pop Up Bongo inalenga kuwaweka karibu zaidi wajasiriamali na wanunuzi hao kwa kuwakutanisha mahala hapa na kisha hata wakishafanya mauzo wanakuwa na wasaha wa kuonana hata baada ya Tamasha hili na kuendeleza uhusiano wa kibiashara" alisema Natasha.
Pia ametoa wito kwa wanajamii kujenga utamaduni wa kuhudhuria maonesho mbalimbali ya biashara ili kupanua wigo zaidi wa ufahamu wa aina mbalimbali za bidhaa ziuzwazo nchini.
Natasha alisema kuwa kwa kutembelea maonesho hayo watapata wasaha wa kufahamu aina mbalimbali za bidhaa ziuzwazo na wafanyabiashara mbalimbali na kujua ni wapo pa kwenda kujipatia mahitaji.
Alisema kuwa Pop Up Bongo ikiwa chini ya udhamini wa kinywaji cha Smirnoff inalenga kuwakutanisha pamoja wafanyabiashara wa bidhaa mbalimbali zitengenezwazo hapa nchini na wanunuzi kwa lengo la kuwasaidia wajasiriamali wa hapa nchini kuongeza pia wigo wa biashara zao.
Kwa upande wake Meneja chapa (pombe kali) wa kampuni ya bia ya Serengeti (SBL) Shomari Shija, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) alisema kuwa kwa kampuni hiyo inatambua nafasi ya wajasiriamali katika kuendeleza uchumi wa nchi na ndio maana imeamua kuunga mkono Pop Up Bongo.
"SBL kwa kupitia kinywaji chetu cha Smirnoff tumeamua kudhamini Pop Up Bongo kwa kuwa ni mahala pazuri kwa wapenzi wa kinywaji hiki kukutana huku wakijipatia mahitaji yao kadhaa kutoka kwa wauzaji wanaouza bidhaa zao katika Pop Up Bongo" alisema Shomari.