MAADHIMISHO YA SIKU YA MOYO DUNIANI YAFANYIKA ZANZIBAR

Muakilishi wa Jimbo la Mpendae Said Mohd Dimwa wapili kushoto akifuatana na Viongozi mbalimbali pamoja na wananchi katika Maandamano ya maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani yaliofanyika katika Ofisi ya Jumuiya ya watu wenye maradhi yasioambukiza (ZNCDA)Mpendae Wilaya ya Mjini Unguja
Maandamano yalioongozwa na Bend ya Chipukizi yakielekea katika Ofisi ya Jumuia ya watu wenye maradhi yasioambukiza katika maadhimisho ya Siku ya moyo Duniani 29/09/2017.Mpendae Wilaya ya Mjini Unguja
Vikundi mbalimbali vya mazoezi vikishajiisha suala zima la ufanyaji mazoezi ili kulinda afya na maradhi mbalimbali, katika siku ya maadhimisho ya Siku ya moyo Duniani 29/09/2017.Mpendae Wilaya ya Mjini Unguja.
Makamo mwenyekiti wa ZNCDA Ali Zubeir Juma akitoa hotuba ya makaribisho kwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Siku ya moyo Duniani 29/09/2017.Mpendae Wilaya ya Mjini Unguja.
Mgeni rasmi katika maadimisho ya siku ya Moyo Duniani Mwakilishi wa Jimbo la Mpendae Said Mohd Dimwa akitoa hotuba kuhusiana na kujikinga na maradhi mbalimbali yanayotokana na Ulaji,Unywaji wa Pombe na Uvutaji wa Tumbaku katika maadhimisho hayo yliofanyika katika Ofisi ya Jumuiya ya watu wenye maradhi yasioambukiza (ZNCDA)Mpendae Wilaya ya Mjini Unguja.
Wananchi mbalimbali waliojitokeza kupimwa afya zao katika maadhimisho ya Siku ya moyo Duniani 29/09/2017.Mpendae Wilaya ya Mjini Unguja.PICHA NA YUSSUF SIMAI/MAELEZO ZANZIBAR.

MAKAMU WA RAIS, MHE. SAMIA SULUHU HASSAN KUZINDUA MAKUMBUSHO MAPYA YA OLDUVAI NA ONESHO LA CHIMBUKO LA MWANADAMU

Morogoro, Septemba 28, 2017.

Serikali ya Tanzania kupitia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya imekamilisha ujenzi wa Makumbusho mapya ya Olduvai ambayo yanaonesha Chimbuko la Binadamu (The Cradle of Humankind) katika Bara la Afrika.
Makumbusho hayo mapya pamoja na Onesho la Chimbuko la Binadamu, yatafunguliwa rasmi na  Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan tarehe 03 Oktoba, 2017 katika eneo la Olduvai, ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.
Onesho hilo ni matokeo ya utafiti wa muda mrefu uliofanyika katika Bonde la Olduvai na Laetoli katika Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha. Wananchi, viongozi mbalimbali wa kitaifa na Mabalozi wanatarajiwa kuhudhuria kwenye hafla hiyo.
Idadi kubwa ya vioneshwa katika Makumbusho hiyo, vilipatikana katika bonde la Olduvai na Laetoli nchini Tanzania kupitia utafiti wa kisayansi wa muda mrefu na vilikuwa vimehifadhiwa katika Makumbusho ya Taifa, Jijini Dar es Salaam. Vioneshwa hivi ni pamoja na masalia ya zamadamu, zana za mawe na masalia ya wanyama walioishi takribani miaka milioni 4 iliyopita.
Makumbusho hayo yamepangwa kuonesha sehemu kuu nne zinazowiana.  Sehemu ya kwanza inahusu ushahidi wa nyayo za zamadamu zilizongunduliwa huko Laetoli mwaka 1978 na mtafiti Dr. Mary D. Leakey.  Nyayo hizi ziliachwa na zamadamu anayeiitwa Australopithecus afarensis na ndio ushaidi usiopingika wa zamadamu kutembea wima kwa miguu miwili takribani miaka milioni 3.6 iliyopita.
Sehemu ya pili inahusu hadithi ya kusisimua ya kuwa binadamu (Genus Homo); ambapo kutakuwa na masalia ya zamadamu wanaoitwa Zinjanthropus au Paranthropus boisei na Homo habilis, zana za mawe za mwanzo zilizotumika (Oldowan) katika kujipatia chakula na ushahidi wa kale wa ulaji wa nyama katika historia ya mabadiliko ya binadamu, takribani miaka million 2 iliyopita.
Sehemu ya tatu inahusu maisha ya jamii ya Homo erectus.  Jamii hii ilikuwa inafanana zaidi na binadamu wa sasa kuliko jamii zilizotangulia. Kutakuwa na masalia zamadamu Homo erectus, zana za mawe (Acheulian) na ushahidi wa ulaji wa wanyama wakubwa kama vile Nyati na tembo katika historia ya mabadiliko ya binadamu, takribani miaka million 1.7 iliyopita.
Sehemu ya nne inaonesha kipindi cha mwanzo cha binadamu wa sasa (Homo sapiens) walioanza kutokea hapa Afrika miaka laki 2 iliyopita. Sehemu hii pia itaonesha mila na utamaduni wa makabila mbalimbali kama vile Wahadzabe, wamasai na Datoga.  Kutakuwa na mavazi ya asili ya jamii hizo, zana za kuwinda na vifaa mbalimbali wanavyovitumia katika maisha yao ya kila siku.
Wizara ya Maliasili na Utalii inawakaribisha wananchi wote kuhudhuria ufunguzi huo ambapo watapata pia fursa ya kutembelea vivutio vingine vilivyopo ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro ili kujifunza na kufurahia urithi huu wa asili na kiutamaduni wa Taifa letu.
Imetolewa na;

Prof. Jumanne Maghembe
Waziri wa Maliasili na Utalii
Waziri wa Maliasili, Prof. Jumanne Maghembe akizungumza na waandishi wa habari jana mkoani Morogoro kuhusu uzinduzi wa Makumbusho Mapya ya Olduvai na Onesho la Chimbuko la Mwanadamu ambayo yatazinduliwa tarehe 03 Oktoba, 2017 na Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika eneo la Olduvai wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha. 

 Waziri wa Maliasili, Prof. Jumanne Maghembe akizungumza na waandishi wa habari jana mkoani Morogoro kuhusu uzinduzi wa Makumbusho Mapya ya Olduvai na Onesho la Chimbuko la Mwanadamu ambayo yatazinduliwa tarehe 03 Oktoba, 2017 na Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika eneo la Olduvai wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha. (Picha na Hamza Temba - WMU).

CHINA YAIPATIA TANZANIA MSAADA WA SH. BILIONI 29.4 KWA AJILI YA MIRADI YA MAENDELEO

IMG_0669
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James (wa pili kulia) na Kaimu Balozi wa China Nchini Tanzania, Mhe. Gou Haodong (wa tatu kushoto) wakisaini makubaliano ya msaada wa Sh. bilioni 29.4 kwa ajili ya miradi ya Ujenzi wa Chuo cha VETA Mkoani Kagera, Utalii wa Kijilojia na Ukarabati wa Uwanja wa Taifa, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.
IMG_0685
Kaimu Balozi wa China Nchini Tanzania, Mhe. Gou Haodong (kushoto) na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James (kulia) wakibadilishana hati ya makubaliano ya msaada wa Sh. bilioni 29.4 kwa ajili ya miradi ya Ujenzi wa Chuo cha Ufundi (VETA), Mkoani Kagera, Utalii wa Kijiolojia na Ukarabati wa Uwanja wa Taifa, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.
IMG_0696
Kaimu Balozi wa China Nchini Tanzania, Mhe. Gou Haodong (kushoto) na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James (kulia) wakiwaonesha waandishi wa habari (hawapo pichani) hati ya makubaliano ya msaada wa Sh. bilioni 29.4 uliotolewa na Serikali ya China kwa ajili ya miradi ya Ujenzi wa Chuo cha Ufundi (VETA) Mkoani Kagera, Utalii wa Kijiolojia na Ukarabati wa Uwanja wa Taifa, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.
IMG_0700
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi Amina Khamis Shaaban (kushoto) na Kamishna wa Fedha za Nje wa Wizara hiyo Bw. John Rubuga (kulia) wakishuhudia utiliwaji saini makubaliano ya msaada wa Sh. bilioni 29.4 uliotolewa na China kwa ajili ya miradi ya Ujenzi wa Chuo cha Ufundi (VETA) Mkoani Kagera, Utalii wa Miamba na Ukarabati wa Uwanja wa Taifa, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.
IMG_0789
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James (katikati), Kaimu Balozi wa China Nchini Tanzania, Mhe. Gou Haodong (wa pili kulia) na Maafisa waandamizi kutoka Tanzania na China wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kusainiwa makubaliano ya msaada wa Sh. bilioni 29.4 uliotolewa na Serikali ya China kwa ajili ya miradi mbalimbali katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.

Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikali Wizara ya Fedha na Mipango

Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam

SERIKALI ya China imeipatia Tanzania msaada wa Shilingi bilioni 29.4 kwa ajili ya kusaidia sekta ya elimu ya ufundi stadi, utalii wa kijiolojia na kukarabati wa Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.

Makubaliano ya msaada huo yametiwa saini Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James, kwa niaba ya Serikali, na Kaimu Balozi wa China hapa nchini, Mhe. Gou Haodong.

Bw. Doto James alisema kuwa kiasi cha Shilingi bilioni 22.4 cha msaada huo kitatumika kujenga Chuo cha Ufundi Stadi-VETA wilayani Ngara mkoani Kagera, ambacho kitakapo kamilika kitadahili zaidi ya wanafunzi 400.

“Fedha hizo zitatumika kujenga vyumba 19 vya madarasa, ujenzi wa karakana 9 za kutolea mafunzo ya elektroniki, ufundi bomba, useremala, ufundi uashi na upakaji rangi” alisema Bw. James

Alieleza kuwa kiasi hicho pia kitatumika kujenga majengo ya utawala, mabweni, nyumba za walimu na miundombinu mingine itakayosaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia kwenye chuo hicho.

“Tunaamini kwamba msaada huo utakuwa sehemu ya kusaidia jitihada za Serikali za kujenga uwezo wa wataalamu wake watakaochangia kukuza sekta ya uzalishaji na hatimaye kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana nchini” alisema Bw. James

Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James alibainisha kuwa katika makubaliano ya msaada huo, Jamhuri ya watu wa China, itatoa kiasi cha shilingi bilioni 6.7 kwa ajili ya kuukarabati Uwanja wa Taifa wa Michezo wa Dar es Salaam.

“Katika makubaliano yetu ya msaada wa kuendeleza Uwanja wa Taifa wenye uwezo wa kuingiza watu 60,000, China itatoa msaada wa kiufundi na vifaa vya kisasa vya michezo na utaalamu katika usimamizi na ukarabati wa uwanja” Alifafanua Bw. James

Bw. Doto James alisema kuwa kiasi kingine cha shilingi milioni 300 kitatumika kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu wa kuanzishwa kwa aina mpya ya utalii ujulikanao kama utalii wa kijiolojia “Geopark Project” katika Hifadhi ya Taifa Ngorongoro, mkoani Arusha.

Alisema lengo la utafiti huo ni kuhakikisha kuwa Tanzania inanufaika na maajabu mbalimbali ya kitalii yaliyopo nchini ambayo hayajatumika kikamilifu kuvutia watalii watakaoongeza pato la Taifa

“Tanzania ina kila sababu ya kujifunza kutoka katika Hifadhi ya Kimataifa ya Jiolojia ya Jiaozuo ya Yuntaishan ya China, iliyoanzishwa mwaka 2000 ambayo inaongeza asilimia 37.2 ya watalii kila mwaka na huchangia asilimia 12 ya pato la Taifa la nchi hiyo” aliongeza Bw. Doto James.

Aliishukuru China kwa ushirikiano wake wa dhati na Tanzania tangu miaka ya 1960 na kwamba mpaka sasa nchi hiyo imeendelea kuipiga jeki Serikali katika ujenzi wa miradi mbalimbali ukiwemo upanuzi wa Chuo cha Polisi Moshi, Ujenzi wa Maktaba mpya katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na ujenzi wa Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Kwa upande wake Kaimu Balozi wa China hapa nchini, Mhe. Gou Haodong, amesema kuwa nchi yake inatarajia kwamba ujenzi wa Chuo Cha Ufundi VETA huko Ngara mkoani Kagera utaanza haraka kama ilivyopangwa.

Kuhusu masauala ya utalii wa kijiolojia katika Hifadhi ya Taifa Ngorongoro, alisema Tanzania ina bahati ya kuwa na vivutio vingi vya utalii lakini haijavutia idadi kubwa ya watalii kutoka China kuja kuvitembelea.

“Zaidi ya watalii milioni moja kutoka China wanatembelea nchi mbalimbali dunia lakini kati ya hao, Tanzania inapokea watalii elfu 20 tu kila mwaka kutoka China, lakini kwa kuanzisha mradi huu, watalii wengi kutoka China watavutiwa kuja nchini kufurahia utalii wa miamba, mandhari nzuri, urithi wa dunia, na kutembelea hifadhi za Taifa” aliongeza Mhe. Haodong

Akizungumzia masuala ya uchumi, Balozi huyo alisema kuwa hivi sasa China imekuwa mwekezaji mkubwa zaidi nchini Tanzania kwa kuwekeza kiasi cha Dola za Marekani bilioni 1.77 na kukuza ajira nchini.

Ameitaja baadhi ya miradi mikubwa iliyowekezwa kuwa ni pamoja na mradi wa miundombinu ya mtandao (Tanzania ICT Broadband backbone), Bomba la gesi la kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, mradi wa kuboresha miundombinu ya Bandari, barabara na madaraja.

Hafla hiyo imehudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo, ambaye alisema kuwa msaada wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi VETA mkoani Kagera kitaongeza watalaamu watakaosaidia kuendeleza sekta ya viwanda nchini.

WATANZANIA WANG'ARA SHINDANO LA MWANDISHI BORA WA SAYANSI NA KILIMO AFRIKA

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti ya Uganda na Mjumbe wa Bodi ya ASARECA, Dr. Ambrose Agona (kushoto), akimkabidhi cheti Mwandishi wa Star Tv Dino Mgunda kuwa mshindi wa pili kwa waandishi wa Televisheni kwenye shindano hilo lililofanyika jana nchini Uganda.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti ya Uganda na Mjumbe wa Bodi ya ASARECA, Dr. Ambrose Agona, akimkabidhi cheti Mwandishi wa Tanzania Koleta Makulwa kutoka Radio Free Afrika ambaye alipata tuzo na kuwashinda wenzake ambao walikuwa wanashindana katika eneo la Radio.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti ya Uganda na Mjumbe wa Bodi ya ASARECA, Dr. Ambrose Agona, akimkabidhi cheti Mwandishi wa Tanzania wa gazeti la Guardian, Gerald Kitabu ambae alishinda tuzo ya umahiri wa habari za sayansi katika eneo la magazeti huku akiwaashinda waandishi wengine kutoka nchi zingine saba za Afrika.
                                                                               Keki ikikatwa katika hafla hiyo

                                                                                    Na Dotto Mwaibale

Mwandishi wa gazeti la Guardian, Gerald Kitabu ameshinda tuzo ya umahiri wa habari za sayansi katika eneo la magazeti huku akiwaashinda waandishi wengine kutoka nchi zingine saba za Afrika.

Kitabu alikuwa anachuana na waandishi kutoka nchi za Nigeria, Burkina Faso, Ghana, Ethiopia, Kenya, Tanzania na Uganda. Shindano hilo lilifanyika jana katika Hoteli ya Speke Resort Munyonyo iliyoko nje kidogo ya jiji la Kampala.
 
Kwa ushindi huo, Kitabu ambaye ni mshindi wa jumla wa shindano la Tanzania, alijinyakulia kitita cha dola za marekani 1,500 pamoja na simu aina ya iPhone 7+ yenye thamani za dola za Marekani 1,200.  
Mwandishi mwingine wa Tanzania aliyepata tuzo ni Koleta Makulwa kutoka Radio Free Afrika ambaye aliwashinda waandishi wengine ambao walikuwa wanashindana katika eneo la Radio. ambapo Tanzania ilizidi kung'ara baada ya Mwandishi wa Star Tv Dino Mgunda kuwa mshindi wa pili katika waandishi wa televisheni.

Koleta aliondoka na kitita cha dola za Marekani 1,500, simu aina ya iPhone 7+ ya thamani ya dola za marekani 1,200 wakati Dino Mgunda alipata zawadi ya dola za marekani 1,000 na simu ya iPhone7+ ya thamani ya dola za marekani 1,000.

Katika shindano hilo jumla ya waandishi 20 waliwakilisha nchi hizo. waandishi hao ni wale ambao walikuwa washindi katika shindano la nchi mahalia, shindano ambalo lilifanyika mwanzoni mwa wiki hii katika nchi hizo ikiwemo tanzania.

Shindano hilo liliandaliwa na Jukwaa la wazi la Bioteknolojia za Kilimo (OFAB) ambalo linahamasisha matumizi ya bioteknolojia katika kilimo ili kuwezesha nchi za Afrika ziweze kujitosheleza kwa chakula.
 
Mshindi wa jumla katika shindano hilo la jana ni mtangazaji wa kituo cha TVC, Omolara Afolayan kutoka Nigeria. Washindi waliteuliwa na jopo la majai watano.

JAFO: WATENDAJI MSILETE LELEMAMA USIMAMIZI MIRADI YA MAENDELEO

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na wananchi mara baada ya kukagua Kituo cha Afya Kintinku wilayani Manyoni, Wengine ni Mkuu wa Wilaya ya Manyoni ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu na Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki (CCM) Mhe Daniel Mtuka
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akiwa na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Manyoni ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu wakikagua chumba cha kuhifadhia maiti katika kituo cha Afya Kintinku wilayani Manyoni.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akitembelea na kukagua mradi wa maji Kintinku/Lusilile wilayani Manyoni
Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Manyoni ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu akimshukuru Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo kwa ukaguzi wa miradi ya maendeleo.
  Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akikagua mradi wa maji Kintinku/Lusilile wilayani Manyoni
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akikagua chumba cha dawa katika Kituo cha Afya Kintinku wilayani Manyoni, Mwingine ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Manyoni ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu

Na Mathias Canal, Singida

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, (Tamisemi) Mhe Seleman S. Jaffo (Mb) amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni Mkoani Singida kuanza haraka Mradi wa Ujenzi wa Chumba Cha upasuaji, na Ujenzi wa wodi ya kisasa.
 

Naibu Waziri Jaffo ametoa maagizo hayo wakati alipokuwa akizungumza na watumishi wa kituo Cha afya Kintinku mara Baada ya kutembele na kujionea uduni wa upatikanaji wa Huduma katika kituo hicho.

Alisema Mradi huo utaambatana na Ujenzi wa maabara kwa ajili ya vipimo kwa wagonjwa, Ujenzi wa eneo la kuchomea taka na Ukarabati wa eneo la kuhifadhia maiti.

Jafo ameonyesha kukerwa na ucheleweshwaji wa kuanza Ujenzi huo licha ya serikali kupeleka fedha kiasi cha shilingi milioni 500 katika mwaka wa fedha 2017/2018 zitakazotosha kukamilisha Ujenzi wote.

Alisema katika awamu ya Pili zitatolewa fedha kiasi cha shilingi milioni 220 zitakazotumika kununua vifaa vyote katika Chumba Cha upasuaji na vifaa tiba kwa ujumla.

Naibu Waziri Jafo alisema kitendo Cha kuchelewa kuanza Ujenzi huo kinachelewesha kuwapatia huduma bora wananchi ambayo inahubiriwa na serikali ya awamu tano inayoongozwa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli.

"Haiwezekani Rais anatoa fedha kwa ajili ya kuboresha sekta mbalimbali nchini ikiwemo sekta ya Afya halafu kuna watu wachache wanashindwa kusimama vizuri fedha Hizo Jambo ambalo linapelekea serikali kulaumiwa na wananchi" Alisema Jaffo

Katika hatua nyingine Mhe Jaffo alimuagiza mhandisi wa Maji Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni Vijijini Eng Gasto Mbondo kutekeleza mpango wa shughuli za utoaji wa Huduma ya maji kupitia Mradi wa kisima Cha Kintinku/Lusilile kilichopo Kijiji Cha Mbwasa (Mbwasa Well Field) kwani eneo Hilo linaonekana kuwa na maji ya kutosha.

Akikagua mradi huo Mhe Jaffo alisema tatizo kubwa kwa wananchi Ni pamoja na changamoto sugu ya upatikanaji Huduma za maji hususani vijijini na kukamilika kwa mradi huo utapunguza umbali na muda wanaotumia wananchi kutafuta maji.

Awali Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni Eng Gasto Mbondo akisoma taarifa ya utekelezaji wa shughuli za utoaji wa Huduma ya maji alisema kuwa Mradi huo wa maji wa Kintinku/Lusilile utakapokamilika unatarajia kuhudumia watu wapatao 45,417 kwa kuongeza 19.2% kutoka 42.1% iliyopo mpaka 61.3% na utakuwa na Vituo 81 vya kuchotea maji (DPs).
  

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu Alisema kuwa utekelezaji wa miradi hiyo utasimamiwa kwa karibu na ofisi yake ili kuongeza Hamasa na tija.

Pia alisema katika Mradi wa Ujenzi wa majengo kwa ajili ya kituo Cha Afya Kintinku asilimia kubwa ya mafundi watatoka katika Wilaya ya Manyoni ili kutoa ajira kwa wananchi husika.

BBC TANZANIA WATEMBELEA WADAU WAKE

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi Kasiga akiwa katika mazungumzo na Mkuu wa BBC, Idhaa ya Kiswahili kwa upande wa Tanzania, Bw. John Solombi leo katika Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje. Timu ya BBC imeanza ziara kuwatembelea wadau wake wakubwa katika masuala ya kupashana habari na wameanza kwa kuitembelea Wizara ya Mambo ya Nje na baadaye walielekea kwa msemaji wa Jeshi la Polisi nchini. Katika mazungumzo hayo, wawili hao walikubaliana kufanya kazi kwa karibu kwa maslahi ya kuuelimisha na kuuhabarisha umma.                        Bw. Solombi akisisitiza jambo katika mazungumzo hayo. Mazungumzo yanaendelea. Katika picha anaonekana Bw. Aboubkar Famau, Mtangazaji wa BBC na Mkuu wa Kitengo cha Uratibu wa Vipindi, akichangia jambo katika mazungumzo hayo. Kulia kwake ni Bw. Ally Kondo, Afisa Mawasiliano wa Wizara ya Mambo ya Nje na aliyekaa peke yake ni Bi. Halima Nyanza, Mtangazaji wa BBC.                                                                                                      Picha ya pamoja Timu ya BBC baada ya kukutana na Kitengo cha Mawasiliano ilipata fursa ya kusalimiana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Suzan Kolimba (Mb). Pichani anaoenekana Mhe. Naibu Waziri akiwapa neno la shukrani Team ya BBC kwa uamuzi wao wa kuichagua Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuwa mdau wa kwanza kutembelewa.Mhe. Naibu Waziri akiwa katika picha ya pamoja na Team ya BBC na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali cha Wizara ya Mambo ya Nje

PROF. MAGHEMBE AFUNGUA MAONESHO YA UTALII

 Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Prof. Jumanne Maghembe (kushoto), aliyefungua rasmi maonesho ya Utalii ya Karibu Kusini, akikaribishwa na Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Iringa kilichopo Kata ya Nduli kwenye banda la maonesho la Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), yanayofanyika kwenye viwanja vya Kichangani..
Mbunge wa Iringa, Mchungaji Peter Msigwa (kushoto) akisalimiwa na Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Iringa kilichopo Kata ya Nduli, Bi. Hana Kibopile alipotembelea banda la maonesho ya Utalii ya Karibu Kusini la Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA).

BULEMBO ATANGAZA KUNG’ATUKA KUGOMBEA UENYEKITI JUMUIA YA WAZAZI

Mwenyekiti wa Jumuia ya Wazazi Tanzania Alhaj Abdallah Bulembo akizungumza na waandishi wa habari leo, Makao Makuu ya Jumuia hiyo jijini Dar es Salaam, kutangaza uamuazi wake wa kutogombea katika Jumuia hiyo.
———————————–
NA BASHIR NKOROMO
Mwenyekiti wa Jumuia ya Wazazi Tanzania, Alhaji Abdallah Bulembo mchana huu ametangaza kujiondoa katika kugombea nafasi ya Uenyekiti wa Jumuia hiyo katika Uchaguzi Mkuu wa ndani ya Chama unaofanyika mwaka huu.

Bulembo ambaye alikuwa ameshachukua fomu kuwania Uenyekiti wa Jumuia ya Wazazi, Taifa, kwa awamu ya pili ametangaza uamuzi huo, mbele ya waandishi wa habari aliowaita Ofisini kwake Makamo Makuu ya Jumuia hiyo jijini Dar es Salaam.
“Mwanzoni kabisa nilitangaza kutogombea, lakini kwa shinikizo la wazee maarufu ndani ya Chama akiwemo Mzee Malecela (John Malecela), na wengineo niliamua kuchukua fomu, lakini sasa leo bila kuomba ushauri kwa yeyote nimeamua kutangaza kuwa sigombei tena”.
“Uamuzi huu nimeufikia baada ya kuona kwamba katika kinyang’anyiro hiki kwenye nafasi ya Uenyekiti tulijitokeza wagombea 49. Sasa nina uhakika baada ya kujitoa mimi katika 48 waliobaki lazima atapatikana Mwana CCM ambaye viatu vyangu vitamtosha”, alisema Bulembo.
Amesema ameamua kujitoa kugombea siyo kwa shinikizo lolote kwa kuwa kwa mujibu wa kanuni za Uchaguzi ndani ya Chama hakuna sehemu yoyote inayomzuia kuwania uongozi.
Builembon amesema, anafurahi kwamba Jumuia ya Wazazi anaiacha ikiwa bora kuliko alivyoikuta, akisema, hivi sasa hadhi ya shule za jumuia hiyo imepanda kitaaluma, na pia Jumuia imeweza kulipa asilimia 68 ya madeni aliyokuta ikidaiwa.

PROF. MAGHEMBE ATOA SIKU 40 KWA WALIOLIMA NDANI YA HIFADHI YA TAIFA YA ARUSHA WAONDOKE KWA HIARI, LAA SIVYO….

Na HAMZA TEMBA – WMU
———————————————————–
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne
Maghembe ameliagiza Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kupitia
Hifadhi ya Taifa ya Arusha kuhakikisha kuwa wananchi wote waliolima ndani ya
eneo la hifadhi hiyo kinyume cha sheria wanaondoa mazao yao pamoja na kusitisha
kabisa shughuli zozote za kibinadamu ndani ya hifadhi hiyo.  
Prof. Maghembe ametoa agizo hilo jana wakati akiwa
kwenye ziara yake ya kikazi ya siku moja katika hifadhi hiyo iliyopo wilaya ya
Arumeru mkoani Arusha kwa ajili ya kukagua shughuli mbalimbali zinazofanywa na
hifadhi hiyo ikiwemo maeneo yenye mgogoro kwa ajili ya kuyatafutia ufumbuzi.
“Naagiza, kuanzia leo ni marufuku mtu yeyote
kuonekana akilima katika eneo hili, wekeni askari hapa, atakayeonekana piga
pingu, hatuwezi kushuhudia watu wanalima ndani ya hifadhi tukae kimya, ni
lazima tuchukue hatua. Watangaziwe na wapewe muda wa kuondoa mazao yao, ndani
ya siku 30 au 40 wawe wameshaondoka”, alisisitiza Prof. Maghembe baada ya
kukagua eneo hilo.
Awali akiwasilisha taarifa ya hifadhi hiyo kwa
Waziri Maghembe, Mhifadhi Mkuu wa hifadhi hiyo, Steria Ndaga alisema eneo hilo
ambalo pia linajulikana kama shamba namba 40 na 41 limekuwa na mgogoro tangu
mwaka 1990 baada wananchi wa Kijiji cha Olkung’wado kuvamia eneo hilo huku
wakitoa hoja kadhaa ikiwemo madai kuwa shamba hilo ni maeneo yao ya asili
waliyokuwa wakimiliki tangu zamani.
Alisema hoja nyingine wanazozitoa ni kuwa walipewa
mashamba hayo na Serikali wakati wa operesheni ya uanzishwaji wa vijiji mwaka
1975 na 1976, Aidha, hoja nyingine ni kuwa hawakushirikishwa kwenye mchakato
wakati wa ugawaji wa mashamba hayo na kwamba TANAPA pia haina hati miliki ya
mashamba hayo.
Ngada alisema hoja zote hizo zilikinzana na ukweli
ya kwamba shamba hilo lilimilikishwa kwa TANAPA tangu mwaka 1980 baada ya
kutolewa tangazo kwa wadau wanaoweza kuliendeleza kufuatia muwekezaji wa awali,
James Preston Mallory kushindwa kuliendeleza na hivyo kufutiwa hati miliki na
Mhe. Rais mnamo mwaka 1979.
“Wadau mbalimbali waliomba umiliki wake ikiwemo
Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro na Halmashauri ya Kijiji cha
Olkung’wado, lakini Kamati ya Ushauri ya Ardhi ya Mkoa wa Arusha ikaishauri
Serikali mashamba hayo yamilikiwe na TANAPA na hivyo tukaandikiwa barua rasmi
ya kukubaliwa kupewa shamba na Idara ya Ardhi Mkoa” alisema Ndaga.
Alisema TANAPA ilinunua eneo hilo lenye ukubwa wa
ekari 966 kwa lengo la kupanua hifadhi ya Taifa ya Arusha ambapo baada kupewa
shamba hilo, iliagizwa kulipa fidia ya mali zilizokuwepo, mwaka 1983 tathmini
ikafanyika na malipo yakalipwa Serikalini hatimaye TANAPA ikapewa barua ya
kumiliki ardhi mwaka 1988. Alisema kwa upande wa Kijiji hicho
cha Olkung’wado hakuna nyaraka yeyote inayoonesha shamba hilo kupewa
kijiji hicho. 
Mhifadhi huyo alisema baada ya mgogoro wa muda
mrefu, wataalam wa TANAPA walifanya survey katika shamba hilo ili kubaini
maeneo yaliyo na shughuli nyingi za kibinadamu na yale yenye umuhimu zaidi
kiikolojia, mapendekezo yalitolewa kuwa maeneo yenye shughuli nyingi za
kibinadamu yaachwe kwa wananchi na yale yenye umuhimu kiikolojia yaendelee
kuhifadhiwa, Bodi ya TANAPA iliridhia ekari 366 zipewe wananchi na ekari 600
ziendelee kuhifadhiwa.
“Baada ya kikao cha wadau wa uhifadhi
kilichoitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru tarehe 11 Mei, 2017 ambacho
kilijumuisha Madiwani, mwakilishi wa Mbunge, katibu tarafa, watendaji wa kata,
wenyeviti na watendaji wa vijiji, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya na
wataalam wa halmashauri, ilifikiwa maazimio ambapo wajumbe waliridhia maamuzi
ya Bodi ya Wadhamini ya TANAPA kuwapa wananchi ekari 366 ya shamba hilo na
kubakiwa na ekari 600” alisema Ndaga.
Aliongeza “Kikao hicho pia kiliridhia TANAPA kuweka
vigingi vya mpaka katika shamba hilo ambapo tarehe 14 Mei, mwaka huu, 2017
zoezi hilo lilianza na jumla ya vigingi 26 viliwekwa”.
Alisema hata hivyo kumekuwepo na taarifa kuwa baadhi
ya wanakijiji wa Kitongoji cha Momella walifungua kesi mahakamani wakidai
wakidai kuwa kijiji cha Olkung’wado kimenyang’anywa ardhi yao na TANAPA, hata
hivyo Serikali hiyo ya Kijiji imekana kwa maandishi kuhisika na ufunguzi wa
kesi hiyo wakidai imefunguliwa na mtu binafsi na sio Serikali ya Kijiji hicho.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Dkt.
Alan Kijazi alimuhakikishia Waziri Maghembe kuwa maagizo yote aliyoyatoa ya
kusitisha shughuli za kibinadamu ndani ya eneo hilo yatafanyiwa kazi na atapewa
mrejesho wa utekelezaji wake.



Hifadhi ya Taifa ya Arusha ilianzishwa mwaka 1960 wakati huo ikiitwa Ngurdoto na ina ukubwa wa kilomita za mraba 322. Hifadhi hiyo ni maarufu kwa utalii wa magari, kutembea kwa miguu, kupanda milima (mlima Meru), utalii wa farasi, mitumbwi ya kuogelea, baiskeli na wa utalii wa kutumia farasi. Katika mwaka wa fedha uliopita 2016/2017 hifadhi hiyo ilivunja rekodi ya ukusanyaji wa mapato kwa asilimia 12 ambapo ilikusanya Shilingi bil. 5.4.
Waziri wa Maliasili, Prof. Jumanne Maghembe (kushoto) akiingia
kwenye ofisi kuu ya Hifadhi ya Taifa ya Arusha jana Mkoani Arusha katika ziara
yake ya kikazi ya siku moja katika hifadhi hiyo iliyolenga kukagua shughuli za
uhifadhi hususan maeneo yenye migogoro kwa ajili ya kuitafutia ufumbuzi. Kushoto
kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Dkt. Alan Kijazi.
 Waziri wa Maliasili, Prof. Jumanne Maghembe (kushoto) akisalimiana
na Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Arusha, Steria Ndaga alipowasili katika
ofisi kuu ya hifadhi hiyo jana Mkoani Arusha kwa ajili ya ziara ya kikazi ya
siku moja iliyolenga kukagua shughuli za uhifadhi hususan maeneo yenye migogoro
kwa ajili ya kuitafutia ufumbuzi. 
 Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Arusha, Steria
Ndaga (wa pili kulia) akiwasilisha taarifa ya hifadhi hiyo kwa Waziri wa
Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe wakati wa ziara yake ya kikazi ya
siku moja katika hifadhi hiyo jana ambayo ililenga kukagua shughuli za uhifadhi
hususan maeneo yenye migogoro kwa ajili ya kuitafutia ufumbuzi.
Prof. Maghembe akizungumza kwenye kikao hicho.
Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Dkt. Alan Kijazi (kushoto)
akizungumza kutambulisha viongozi wa Hifadhi ya Taifa ya Arusha kwa Waziri wa
Maliasili, Prof. Jumanne Maghembe (kulia) wakati wa ziara yake ya kikazi ya
siku moja katika hifadhi hiyo jana Mkoani Arusha ambapo ililenga kukagua
shughuli za uhifadhi hususan maeneo yenye migogoro kwa ajili ya kuitafutia ufumbuzi. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (kushoto) na wajumbe wa kikao hicho wakifuatilia taarifa kuhusu Hifadhi ya Taifa ya Arusha ambayo iliwasilishwa na Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi hiyo, Steria Ndaga.
 Waziri wa Maliasili, Prof. Jumanne Maghembe (kushoto) akiongea
na viongozi wa TANAPA kuhusu eneo lililolimwa na wananchi ndani ya Hifadhi ya
Taifa ya Arusha kinyume cha sheria wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja katika
hifadhi hiyo iliyolenga kukagua shughuli za uhifadhi hususan maeneo yenye migogoro
kwa ajili ya kuitafutia ufumbuzi, aliagiza wananchi hao waondolewe ndani ya
siku 40. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Dkt. Alan Kijazi na Mhifadhi
Mkuu wa hifadhi hiyo, Steria Ndaga (kulia). 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (wa
pili kulia) akisikiliza ufafanuzi wa jambo kutoka kwa Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi
ya Taifa ya Arusha, Steria Ndaga (kushoto) wakati wa ziara yake ya kikazi ya
siku moja katika hifadhi hiyo jana ambayo ililenga kukagua shughuli za uhifadhi
hususan maeneo yenye migogoro kwa ajili ya kuitafutia ufumbuzi. 
 Baadhi ya wanyamapori (Twiga na Pundamilia) wakionekana wakijivinjari ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Arusha wakati wa ziara ya kikazi ya siku moja ya Waziri wa Maliasili, Prof. Jumanne Maghembe katika hifadhi hiyo jana ambayo ililenga kukagua shughuli za uhifadhi hususan maeneo yenye migogoro kwa ajili ya kuitafutia ufumbuzi. 

SERIKALI ITAHAKIKISHA MIRADI YA UMEME, MBAGALA, KURASINI NA KIGAMBONI INAKAMILIKA-DKT. KALEMANI

 Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani, (wakwanza kulia), Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania, (TANESCO), Mhandisi Dkt. Tito Mwinuka, (wakwanza kushoto), na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo anayeshughulikia Miradi, Mhandisi Khalid James, (watatu kushoto), wakimsikiliza Meneja Mradi wa TEDAP, Mhandisi Emmanuel Manirabona, (aliyenyoosha mkono), wakati Naibu Waziri na uongpozi wa TANESCO, ulipotembelea mradi wa TEDAP wa Gongolamboto jijini Dar es Salaam, Septemba 18, 2017. Mradi huo unahusu upanuzi na uendelezaji wa mradi wa kusafirisha umeme wa 132kv.

NA K-VIS BLOG/Khalfan Said

SERIKALI kupitia Shirika la Umeme Tanzania, (TANESCO), imeahidi kusimamia miradi ya umeme Kituo cha Tipper-Kigamboni,  Mbagala na Kurasini ili kuhakikisha inakamilika kwa haraka na kwa wakati na hatimaye wananchi wa maeneo hayo wanaondokana na adha ya kukatika kwa umeme mara kwa mara.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani, mwishoni mwa ziara yake ya kufuatilia uboreshaji wa vituo vya kupoza na kusambaza umeme pamoja na ujenzi wa kituo kipya cha kufua na kusambaza umeme huko Kimbiji  wilayani Kigamboni jijini Dar es Salaam Septemba 18, 2017.

Waziri pia amekagua ujenzi wa mradi wa maendeleo ya upanuzi na upatikanaji nishati (TEDAP), wa kusafirisha umeme wa 132kv ulioko Gongolamboto nje kidogo ya jiji.

“Wananchi wanataka umeme, hawahitaji kujua  nguzo za umeme zimepatikana wapi, au upembuzi yakinifu utakamilika lini, nimeagiza baada ya siku tano kuanzia leo (Septemba 18), fanyeni kazi usiku na mchana walau vituo viwili vya kupoza na kusambaza umeme viwe vimekamilika ili wananchi wa Mbagala na Kigamboni wapate umeme wa kutosha.” Alisema Dkt. 

Kalemani mbele ya Mbunge wa Kigamboni Dkt. Faustine Ndungulile, Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Mhe. Hashim Mgandila na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi, Dkt. Tito Mwinuka na viongizi wengine wa Tanesco.

Dkt. Kalemani alisema, miradi hiyo imechukua muda mrefu, na kwamba hakuna muda zaidi utakaoongezwa kuikamilisha.Serikali kupitia TANESCO, inatekeleza miradi mitano ya kuongeza kiasi cha umeme kwenye maeneo ya Mbagala na maeeno kadhaa ya wilaya ya Temeke, Kurasini na Kigamboni ili kukabiliana na ongezeko la kasi la watu na shughuli za kiuchumi katika maeneo hayo.
Aidha Naibu Waziri aliipongeza TANESCO, kwa kutekeleza agizo lake la kuhakikisha wakazi 3,500 wa Kigamboni waliolipia ili kuunganishiwa umeme, wawe wameunganishiwa ifikapo Septemba 15, 2017 ikiwa ni pamoja na kupeleka nguzo za umeme zaidi ya 1,000 maagizo ambayo yametekelezwa.

Hata hivyo naibu Waziri alimueleza Mheshimiwa Mbunge wa Kigamboni na Mkuu wa Wilaya hiyo kuwa tiba mahsusi ya upungufu wa umeme kwenye wilaya hiyo ni kukamilika kwa ujenzi wa kituo kipya cha kupoza na kusambaza umeme cha Kimbiji.

“Tiba kubwa ya matatizo ya umeme kwa watu wa Kigamboni, na Mbagala ni hapa Kimbiji(kituo kipya), vile vituo vingine vitapunguza tu matatizo lakini naomba Mheshimiwa Mbunge, uwafikishie ujumbe wananchi kuwa Serikali ya awamu ya Tano inayo dhamira ya kweli ya kuhakikisha inawapatia umeme wa uhakika sio tu wananchi wa Kigamboni bali watanzania wote kwa ujumla.” Alifafanua Dkt. Kalemani.

Naibu Waziri ameshuhudia hatua mbalimbali za ukamilishaji wa miradi hiyo zikiwa zimefikiwa ambapo katika kituo maeneo yote aliyotembelea.
Kuhusu ujenzi wa kituo kipya cha Kimbiji, Dkt. Kalemani amemuagiza Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANSCO, Mhandisi Dkt. Tito Mwinuka, kuwaleta mafundi wa TANESCO wealiotekeleza kwa muda mfupi ujenzi wa mradi wa kituo cha kupoza na ksuambaza umeme kule Mtwara ili waje kuongeza nguvu.
Mbunge wa Kigamboni Mhe. Dkt. Faustine Ndungulile, (kushoto), akizungumza mbele ya Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani ambaye alifuatana naye kwenye ziara hiyo.
Sakafu ya kufungia transfoma mpya ya umeme wa 15mva kituo cha Tipper-Kigamboni, ikijengwa Septemba 18, 2017
Mshine mpya kwenye kituo cha Mbagala
Kituo cha Kurasini ambacho nacho kitakuwa tayari baada ya siku tano.
Dkt. Kalemani, (katikati), Dkt. Ndungulile (wapili kushoto) na Dkt. Mwinuka, (wakwanza kushoto), wakiwa na Meneja wa Mradi wa TADEP, Mhandisi Emmanuel Manirabona, (kulia), baada ya kujionea moja ya mashine mpya ikiwa bado imefunikwa ili kuzuia vumbi kwenye kituo cha Kurasini.
Fundi akiwa kazini kwenye kituo cha Kurasini.
Naibu Waziri Dkt. Kalemani, na Mbunge wa Kigamboni Dkt. Ndungulile, wakiwa na furaha baada ya kutembelea kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Mbagala, ambacho ujenzi wake umekamilika
Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Mhe. Hashim Mgandila, akizungumza mwishoni mwa ziara ya Naibu Waziri, Dkt. Kalemani huko Kimbiji.
Naibu Waziri Dkt. Kalemani na Mhandisi Khalid James.
Msafara wa Naibu Waziri ukiwa kwenye eneo la mradi wa TEDAP. Gongolombaoto.
Mkandarasi anayejenga mradi wa TEDAP, Gongolamboto, akizunguzma.
Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, anayeshughulikia usambazaji umeme na huduma kwa wateja mama Joyce Ngahyoma, akielezea hatua zilizochukuliwa na TANESCO katika kuhakikisha wateja 3,500 wa TANESCO Kigamboni waliolipia gharama za kuunganishiwa umeme, wanapatiwa huduma hiyo ikiwa ni pamoja na kupelekwa kwa nguzo zaidi ya 1,000 kwenye eneo la Kigamboni. Anayemsikiliza ni Naibu Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani.
Kituo cha Mbagala
Dkt. Kalemani, (kushoto), akimsikiliza Meneja wa TANESCO Mkoa wa Temeke, Mhandisi Jahulula akielezea hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Tipper-Kigamboni.
Dkt. Kalemani, (wapili kushoto), akizungumza jambo na Mhandisi Dkt. Tito Mwinuka, walipowasili eneo la Kimbiji ambako kunatarajiwa kujengwa kituo kipya cha kupoza na kusambaza umeme kitakachohudumia wakazi wa Kigamboni, Kurasini na Mbagala. Wakwanza kushoto ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO nayeshughulikia Miradi, Mhandisi Khalid James.