Morogoro, Septemba 28, 2017.
Serikali
ya Tanzania kupitia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa kushirikiana
na Umoja wa Ulaya imekamilisha ujenzi wa Makumbusho mapya ya Olduvai
ambayo yanaonesha Chimbuko la Binadamu (The Cradle of Humankind) katika Bara la Afrika.
Makumbusho
hayo mapya pamoja na Onesho la Chimbuko la Binadamu, yatafunguliwa
rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa
Samia Suluhu Hassan tarehe 03 Oktoba, 2017 katika eneo la Olduvai, ndani
ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.
Onesho
hilo ni matokeo ya utafiti wa muda mrefu uliofanyika katika Bonde la
Olduvai na Laetoli katika Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha. Wananchi,
viongozi mbalimbali wa kitaifa na Mabalozi wanatarajiwa kuhudhuria
kwenye hafla hiyo.
Idadi
kubwa ya vioneshwa katika Makumbusho hiyo, vilipatikana katika bonde la
Olduvai na Laetoli nchini Tanzania kupitia utafiti wa kisayansi wa muda
mrefu na vilikuwa vimehifadhiwa katika Makumbusho ya Taifa, Jijini Dar
es Salaam. Vioneshwa hivi ni pamoja na masalia ya zamadamu, zana za mawe
na masalia ya wanyama walioishi takribani miaka milioni 4 iliyopita.
Makumbusho hayo yamepangwa
kuonesha sehemu kuu nne zinazowiana. Sehemu ya kwanza inahusu ushahidi
wa nyayo za zamadamu zilizongunduliwa huko Laetoli mwaka 1978 na
mtafiti Dr. Mary D. Leakey. Nyayo hizi ziliachwa na zamadamu anayeiitwa
Australopithecus afarensis na ndio ushaidi usiopingika wa zamadamu
kutembea wima kwa miguu miwili takribani miaka milioni 3.6 iliyopita.
Sehemu
ya pili inahusu hadithi ya kusisimua ya kuwa binadamu (Genus Homo);
ambapo kutakuwa na masalia ya zamadamu wanaoitwa Zinjanthropus au
Paranthropus boisei na Homo habilis, zana za mawe za mwanzo zilizotumika
(Oldowan) katika kujipatia chakula na ushahidi wa kale wa ulaji wa
nyama katika historia ya mabadiliko ya binadamu, takribani miaka million
2 iliyopita.
Sehemu
ya tatu inahusu maisha ya jamii ya Homo erectus. Jamii hii ilikuwa
inafanana zaidi na binadamu wa sasa kuliko jamii zilizotangulia.
Kutakuwa na masalia zamadamu Homo erectus, zana za mawe (Acheulian) na
ushahidi wa ulaji wa wanyama wakubwa kama vile Nyati na tembo katika
historia ya mabadiliko ya binadamu, takribani miaka million 1.7
iliyopita.
Sehemu
ya nne inaonesha kipindi cha mwanzo cha binadamu wa sasa (Homo sapiens)
walioanza kutokea hapa Afrika miaka laki 2 iliyopita. Sehemu hii pia
itaonesha mila na utamaduni wa makabila mbalimbali kama vile Wahadzabe,
wamasai na Datoga. Kutakuwa na mavazi ya asili ya jamii hizo, zana za
kuwinda na vifaa mbalimbali wanavyovitumia katika maisha yao ya kila
siku.
Wizara
ya Maliasili na Utalii inawakaribisha wananchi wote kuhudhuria ufunguzi
huo ambapo watapata pia fursa ya kutembelea vivutio vingine vilivyopo
ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro ili kujifunza na kufurahia urithi huu wa
asili na kiutamaduni wa Taifa letu.
Imetolewa na;
Prof. Jumanne Maghembe
Waziri wa Maliasili na Utalii
Prof. Jumanne Maghembe
Waziri wa Maliasili na Utalii
Waziri
wa Maliasili, Prof. Jumanne Maghembe akizungumza na waandishi wa habari
jana mkoani Morogoro kuhusu uzinduzi wa Makumbusho Mapya ya Olduvai na
Onesho la Chimbuko la Mwanadamu ambayo yatazinduliwa tarehe 03 Oktoba,
2017 na Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika eneo la Olduvai
wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha.
Waziri
wa Maliasili, Prof. Jumanne Maghembe akizungumza na waandishi wa habari
jana mkoani Morogoro kuhusu uzinduzi wa Makumbusho Mapya ya Olduvai na
Onesho la Chimbuko la Mwanadamu ambayo yatazinduliwa tarehe 03 Oktoba,
2017 na Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika eneo la Olduvai
wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha. (Picha na Hamza Temba - WMU).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni