Na. Mahmoud Ahmad, Dodoma.
Mamlaka ya usimamizi wa Bima nchini (TIRA) imetoa onyo kali kwa watu wanaowatapeli wananchi kwa kuwauzia bima za kugushi na hivyo kuwasababishia hasara na kuikosesha Serikali mapato,Matapeli hao ambao wengi wao hawana leseni za kufanya biashara ya Bima wametakiwa kuacha mara moja wizi huo kwani mkono wa sheria unawasaka ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao.
Akizungumza wakati wa zoezi la ukaguzi wa bima katika Vyombo vya moto lililofanyika Mjini Dodoma ,Bibi Stella Guli Rutaguza amesema jumla ya magari 586 yalifanyiwa ukaguzi, ambapo wamebaini magari 25, pikipiki za miguu mitatu 5(bajaj) pikipiki za miguu miwili 2 yakiwa na Bima za kugushi huku magari mengine 19 yakiwa hayana bima.
Rutaguza amesema kuwa wamefaminikiwa kuwakamata watu Wawili ambao wanatuhumiwa kujihusisha na kuuza bima za kugushi kwa wananchi na tayari wako mikononi mwa Jeshi la Polisi kwa hatua zaidi za kisheria.
Bibi Stella Rutaguza amesema zoezi la kuwasaka watu wanaouza bima feki kwa na kuwaibia wananchi na Serikali ni endelevu hapa Dodoma na Nchi nzima kwa ujumla.
"Tunataka kukomesha tabia hii chafu kwenye Soko la Bima", hivyo tunawataka vishoka wa Bima popote walipo watafute kazi halali ya kufanya maana Mamlaka ya Usimamizi wa Bima haitawafumbia macho na mkono wa sheria hawataukwepa", alisema Rutaguza.
Amewataka wananchi kuchukua tahadhari ya kutokuibiwa na matapeli hawa wa Bima kwa kununua Bima kwenye ofisi zilizosajiliwa na kupewa Leseni na Serikali kwa ajili ya kufanya biashara ya Bima na kuacha kununua Bima kiholela mitaani kwa watu wasiofahamika.
"Kuna wananchi wananunua bima faki kwa kutokujua na kuibiwa na watu hawa wasio waaminifu lakini pia tunafahamu kuwa kuna baadhi ya wananchi wananunua bima feki kwa hiari yao wenyewe kwa sababu bima hizo zinauzwa bei ya chini sana kuliko bima halali, Tukibaini kuwa ulinunua bima feki kwa hiari yako basi wote wawili mnunuzi na muuzaji mtaakuwa na hatia ya kupanga njama za wizi na utapeli wa kuiibia Serikali mapato Yake Sheria itawashughulikia wote." alisisitiza.
Amesema kuwa Mteja wa Bima au mtu yeyote anaweza kuhakiki bima aliyonunua kama ni halali au ni feki kwa kutumia njia ya mfumo wa TIRAMIS. Mfumo huu umetengenezwa na Mamlaka kwa ajili ya kudhibiti wezi wa mapato ya Bima za vyombo vya moto kwa Serikali,
Makampuni ya Bima na pia kumrahisishia Mwananchi kuepuka kuibiwa fedha zake.
Meneja huyo wa kanda ya kati Stella Rutaguza pia ametoa rai kwa wafanyabiashara wa bima kufuata sheria na miongozo ya ufanyaji biashara hiyo kama ilivyoainishwa kwenye sheria ya Bima namba 10 ya mwaka 2009 na hivyo kuepusha usumbufu kwa Wananchi wakati wanapotakiwa kupata fidia ya bima.
Amesema kuwa mfanyabiashara yeyote atakayebainika kukiuka taratibu za utendaji na kusababisha usumbufu usio wa lazima kwa wananchi hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake ikiwa ni pamoja na Mamlaka kumfutia leseni yake.
Afisa Mwandamizi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Nchini (TIRA) kanda ya kati ,Adamu Maneno (katikati)akihakiki stika ya bima kama ni halali au feki stendi ya Hiace jamatini Dodoma,kulia kwake ni PC Majenga,kushoto kwake ni Liberath wakala wa bima mkoani hapo.Picha na Vero Ignatus Blog.
Afisa mwandamizi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Kanda ya Kati Rojas Msagati (katikati)akiwa anahakiki moja ya gari katika stendi ya jamatini Dodoma ,kulia.kwake ni WP 4079CPL Karitas.
Haule Reward, Meneja Dodoma Jubilee Insurance .
Muonekano wa Stendi ya hiace Jamatini Dodoma.Picha na Vero Ignatus Blog.
Askari wa kikosi cha usalama barabarani G.8922PC.Bashiru wa kwanza kushoto,pamoja na H.5987PC Majenga walishirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Kanda ya kati katika zoezi la ukaguzi wa bima kanda ya kati.
Baadhi ya vyombo vya moto vilivyokamatwa vikiwa katika kituo cha Polisi Dodoma.Picha na Vero Ignatus Blog
NAMNA YA KUHAKIKI BIMA YAKO YA GARI:
*************************1. Kwa kutumia ujumbe wa simu: Nenda kwenye uwanja wa kutuma ujumbe mfupi, andika neno Stika, acha nafasi, andika namba ya Stika ya Bima, Tuma kwenda namba 15200.
2. Kwa kutumia mfumo wa TIRAMIS.
Pakua (download) TIRAMIS kwenye simu yako, Bonyeza (click) neno Tiramis, utakuja Uwanja wa TIRAMIS kwenye simu yako ambapo utaona Maneno yanayokueleza hakiki hati ya bima ( validate insurance covernote) na Maneno mengine yanasema hakiki Stika ya Bima (validate insurance sticker) Kuhakiki hati ya Bima unahakiki kwa kutumia namba ya gari lako.
Unachotakiwa kufanya ni kubonyeza hapo kwenye validate insurance cover, utaandika namba yako ya gari halafu utabonyeza neno hakiki (validate) baada ya hapo utapata Maelezo ya Bima ya gari unayohakiki.
Unaweza pia Kuhakiki kwa kutumia stika ya Bima yako. Unachotakiwa kufanya ni kubonyeza neno validate insurance sticker(hakiki Stika ya bima),andika namba yako ya Stika halafu bonyeza neno validate(hakiki). Baada ya hapo utapata majibu yanayokueleza kuhusu hiyo Stika ya Bima. Majibu utakayopata kwenye Kuhakiki bima kupitia namba ya gari na Kuhakiki kupitia namba ya Stika ya Bima yote yanafanana kama. Majibu yanakuwa na Maelezo yafuatayo:-
1. Utaambiwa uhai wa bima hiyo.
2.Bima imekatwa kwa Kampuni gani.
3. Namba ya gari. iliyokatiwa bima hiyo.
4.Aina ya Bima kwa mfano ni Comprehensive au thirdparty.
5.Namba ya Stika.
6. Aina ya Stika kwa mfano, ni private,public service, n.k.
7. Bima ni halali mpaka tarehe ngapi.
MUHIMU: Ukiona majibu unayoyapata unapohakiki bima yako ni tofauti na Maelezo ya Bima unayohakiki kwa mfano tofauti ya namba ya gari,Kampuni ya Bima iliyokatiwa bima hiyo, namba ya stika, muda wa kuisha bima hiyo n.k. wasiliana na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima kwa ajili ya kuchukua hatua za haraka ili kukuepusha kupata hasara.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni