Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli akihutubia mamia ya wananchi Wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga wakati wa dhifa ya uzinduzi wa barabara ya Isaka-Ushirombo yenye urefu wa Kilomita 132, Leo 10 Machi 2018. Picha Zote Na Mathias Canal-Wazo Huru Blog
Sehemu ya mamia ya wananchi Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga wakimsikiliza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli wakati wa sherehe za uzinduzi wa barabara ya Isaka-Ushirombo yenye urefu wa Kilomita 132, Leo 10 Machi 2018.
Na Mathias Canal, Kahama-Geita
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli Leo 10 Machi 2018 amezindua barabara ya Isaka-Ushirombo yenye urefu wa Kilomita 132 iliyojengwa na kukamilika kwa kiwango cha lami.
Katika sherehe za ufunguzi wa barabara hiyo katika Eneo la Nyasubi, Kahama Mjini Mhe Rais Magufuli amesema kuwa Barabara hiyo ni chachu ya ukuaji wa uchumi na kiungo cha Mikoa ya Shinyanga, Geita na Kagera pia ni sehemu ya kurahisisha na kuimarisha mahusiano chanya ya kibiashara baina ya nchi za Uganda, Rwanda na Burundi.
Rais Magufuli amewataka wafanyabiashara nchini kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya dawa kwani serikali inatumia zaidi ya shilingi Bilioni 269 kununua dawa nje ya nchi hivyo endapo watajenga viwanda hivyo vya dawa serikali itawanufaisha wafanyabiashara wa ndani ya nchi kwa kununua bidhaa hizo.
Kama alivyojipambanua katika kuwatetea wanyonge Mhe Rais Magufuli ameagiza kutohamishwa wananchi waliovamia eneo la ardhi ya Wizara ya Elimu, wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (MWAMVA), na kusema kuwa wananchi hao ndio waliompigia kura na hatimaye kuwa Rais wa nchi hivyo hawapaswi kunyanyaswa.
Aidha, aliwataka wananchi wengine kutoendelea na ujenzi wa nyumba za makazi katika Mtaa wa Igomelo, Kata ya Malunga ili eneo lililosalia la hekari 40 ndilo litumike kujenga chuo hicho.
Katika hatua nyingine Rais Magufuli amewashukuru wabunge wa Mkoa wa Shinyanga kwa kushirikiana na wabunge wengine wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitisha sheria ya madini ya mwaka 2010 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2017 ambayo inataka kuwa na uchumi fungamanishi kwa wananchi kupitia rasilimali zao.
Aidha, serikali imekuwa ikikusanya mapato mengi kupitia sekta ya madini ambapo mwaka 2014/2015 ilikusanya jumla ya shilingi Bilioni 168.09, mwaka 2015/2016 ilikusanya zaidi ya Bilioni 205, mwaka 2016/2017 ikikusanya jumla ya Shilingi Bilioni 213.365
Katika hatua nyingine Diwani wa Kata ya Bugalama (CHADEMA), Katibu mwenezi Kanda ya ziwa (CHADEMA) na wanachama wengine 50 wamejivua uanachama wa Chadema mbele ya Rais Magufuli na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi huku wakisema kuwa wameridhishwa na utendaji wake katika kuwatumikia watanzania.
Mradi wa ukarabati wa barabara hiyo ya Isaka-Ushirombo yenye urefu wa Kilomita 132 iliyojengwa na kukamilika kwa kiwango cha lami ni sehemu ya barabara kutoka Isaka hadi Lusumo yenye kilomita 1334 iliyokuwa imejengwa mwaka 1980 na mwanzoni mwaka 1990 hivyo imetumika kwa kipindi cha miaka 20 bila kufanyiwa marekebisho.
Dhifa ya uzinduzi wa barabara hiyo umehudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe Zainab Telack, Naibu Waziri wa Ujenzi, uchukuzi na mawasiliano, Mhe Elius John Kuandikwa (Mb), Naibu waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko (Mb), Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Joseph Nyamhanga na Mtendaji Mkuu wa Tanroads Mhandisi Patrick Mfugale, na Wabunge wa Mkoa wa Shinyanga.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni