SHILINGI MILIONI 600 KUJENGA KITUO CHA AFYA KALAMBA-KONDOA

  Na.Benny Mwaipaja, Kondoa

ZAIDI ya wakazi elfu 30 wa kata mbili za Kalamba na Haubi wilayani Kondoa mkoani Dodoma wanatarajia kuondokana na adha ya kukosa huduma ya afya karibu na maeneo yao baada ya Serikali kutoa zaidi ya shilingi milioni mia 6 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya kitakachengwa katika kitongoji cha Itongwi, kijiji cha Kalamba kata ya Kalamba.


Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji, ametembelea eneo hilo na kushuhudia wananchi wenye ari wakiwa wamejitolea nguvu zao kusafisha eneo ambalo kituo hiko kitajengwa ili kuwaondolea adha ya muda mrefu ya kufuata huduma za afya Kondoa mjini umbali wa zaidi ya kilometa 100.

Wakazi wa Kata za Kalamba na Haubi wilayani Kondoa mkoani Dodoma walijitokeza wakiwa na majembe, miundu, mapanga na mashoka kusafisha eneo la mradi wa ujenzi wa kituo cha afya Kalamba kitakacho toa huduma ya mama na Mtoto, ambapo tayari, mawe, mchanga na kokoto vimekwisha pelekwa katika eneo la ujenzi.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dokta Ashatu Kijaji ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kondoa Vijijini, amepongeza jitihada za wananchi hao kwa kujitolea nguvu zao kushiriki ujenzi wa kituo hicho cha afya ambacho majengo yake yatagharimu shilingi milioni 400.

Aidha, Dkt. Kijaji amesifu uamuzi wa baadhi ya wanakijiji cha Kalamba wa kutoa maeneo yao zaidi ya ekari 6 bila kudai fidia ili kuwezesha kuanza kwa ujenzi wa mradi huo unaotarajiwa kukamilika ndani ya miezi mitatu ijayo.

Amesema kuwa kitendo hicho kinafaa kuigwa na watanzania wengine katika maeneo ambayo miradi ya kijamii inapita ili kuipunguzia serikali gharama za miradi na hivyo kuharakisha maendeleo ya wananchi.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma Dkt. Ikaji Rashid, alisema kuwa kituo hicho cha afya kitakuwa na majengo sita yakiwemo wodi ya wazazi, jengo la upasuaji wa dharula wa mama wajawazito, jengo la kuhifadhia maiti na jengo la wagonjwa wa nje.

"Akina mama wajawazito watakao hitajika kufanyiwa upasuaji baada ya kubainika kuwa na changamoto ya uzazi watapatiwa huduma hapa hapa hivyo hakutakuwa na haja ya kukimbizwa mjini Kondoa hivyo wataepuka gharama na kuepuka kujifungulia majumbani" Alisisitiza Dkt. Rashid.

Alisema kuwa Serikali imetoa pia fedha kiasi cha shilingi milioni 220 kwa ajili ya kununua vifaa vitakavyotumika kutolea tiba baada ya ujenzi wa kituo hicho cha afya kukamilika.

Wakizungumza katika ziara hiyo ya kukagua eneo la ujenzi wa kituo hicho kipya cha afya Kalamba, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kondoa Bi. Hija Bakari Suru na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilayani Kondoa Alhaji Othman Gora wamewataka wakazi wa kata hizo mbili kujitolea kufanyakazi ili mradi huo ukamilike kwa wakati.

Aidha, walisisitiza umuhimu wa kamati ya ujenzi kufanyakazi kwa bidii na kwa uadilifu ili malengo ya muda mrefu ya wananchi wa kata hizo la kupata huduma karibu na maeneo yao yaweze kufikiwa.
Wakazi wa wa Kijiji cha Kalamba Wilayani Kondoa Mkoani Dodoma wakipokea kwa shangwe maelezo ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango na Mbunge wa Kondoa Vijijini Dkt. Ashatu Kijaji (hayupo pichani) alipokua akieleza mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya utakaogharimu Sh. Milioni 600 alipo kwenda kukagua maendeleo ya Mradi huo.
Wazee wa Kijiji cha Kalamba Wilayani Kondoa Mkoani Dodoma wakimsikiliza kwa Makini Naibu Waziri wa Fedha na Mipango na Mbunge wa Kondoa Vijijini Dkt. Ashatu Kijaji (hayupo pichani) alipokua akieleza umuhimu wa kuwapeleka shule watoto wao na kushiriki katika miradi ya maendeleo, alipotembelea Kijiji hicho kukagua mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya utakaogharimu Sh. Milioni 600.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kalamba Bw. Mahamudu Issa Katengo, akieleza namna wanakijiji walivyopokea kwa furaha Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Afya baada ya muda mrefu kuhangaika kutafuta matibabu mbali na eneo hilo wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango na Mbunge wa Kondoa Vijijini Dkt. Ashatu Kijaji (katikati) alipokwenda kukagua mradi wa ujenzi wa Kituo hicho.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Dkt. Ikaji Rashid (kulia) akiwaeleza mchakato uliosababisha kuweka Kituo cha Afya katika Kijiji cha Kalamba ambapo alisema ni kutokana na utayari wa Wakazi hao kujitolea ardhi bure kwa maendeleo yao wakati wa Ziara ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango na Mbunge wa Kondoa Vijijini Dkt. Ashatu Kijaji (katikati)alipokwenda kukagua miradi ya Maendeleo katika kata ya Kalamba. 
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kondoa Mkoani Dodoma Alhaji Othman Gora akizungumza na Wakazi wa Kata za Kalamba na Haubi namna Chama chake kilivyoridhika jinsi Serikali inavyotekeleza kwa umakini Ilani ya Uchaguzi.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, ambaye pia ni Mbunge wa Kondoa Vijijini, akiwaeleza wakazi wa Kata za Kalamba na Haubi kuhusu ujenzi wa Kituo cha Afya kalamba kitakachohudumia zaidi ya wakazi elfu 30 wa kata hizo ujenzi wake utakapokamilika miezi mitatu ijayo.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma Alhaji Othman Gora (kulia) na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa Bi. Hija Bakari Suru wakifuatilia kwa makini maelekezo ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji (hayupo pichani) alipotembelea na kukagua eneo la ujenzi wa kituo kipya cha afya cha Kalamba.
Mkazi wa Kijiji cha Kalamba Bw. Athuman Abdala, akiishukuru Serikali kwa kutoa fedha zaidi ya shilingi milioni 600 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Kalamba pamoja na ununuzi wa vifaa tiba, kitakachotoa huduma ya mama na mtoto kwa wakazi wa kata za Kalamba na Haubi hivyo kuwaondolea kero ya muda mrefu ya kufuata huduma ya afya mjini Kondoa.
Wakazi wa Kata za Kalamba na Haubi wakimpongeza naibu Waziri wa Fedha na Mipango na Mbunge wa Kondoa Vijijini, Dkt. Ashatu Kijaji (kushoto) kwa kusimamia maendeleo ya jimbo lake na kuhamasisha maendeleo, alipofanya ziara ya kukagua eneo la ujenzi wa kituo cha afya Kalamba katika Halmashauri ya wilaya ya Kondoa.


(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni