Inna lillah wainna Illah rajiun.Poleni wana Ujiji poleni wana Kigoma poleni wana CCM na poleni Watanzania.
Ilikuwa alfajiri ya leo saa 12.37 asubuhi nilipopokea simu kutoka rafiki na ndugu yangu Ahmed Maaruf Byemba almaarufu Yaounde. Alianza na kauli niliyoanza nayo hapo juu.
Nikajua yametimia kwani ndugu yangu huyo anamuuguza mdogo wake kule Dodoma hivyo nikaelewa mgonjwa wake amefariki. Haikuwa hivyo bali alikuwa ananifahamisha kuwa Dk. Aman Walid Kaburou hatunae tena.
Niliduwa japo sikushangaa kwani taarifa za ugonjwa nilikuwanazo na hata taarifa za kupekekwa Muhimbili kutokea hospitali ya Maweni Kigoma nilikuwanazo na ndio maana sikushangaa. Ila niliduwaa kutokana na ninavyomfahamu Dk Kaburou. Nina historia nae.
Baada ya kupata maelezo toka kwa ndugu Yaounde nakuondokana na mduwao uliokuwa umenipata niliendelea kupata simu kuhusiana na kufariki kwa Dk Kabourou kutoka kwa ndugu wengine, hususan wana Ujiji.
Kifo cha Dk Aman Walid Kabourou kimenirejesha kifikra zaidi ya miaka 68 tokea sasa tukiwa watoto hadi kipindi cha kuanza elimu ya msingi. Mimi nilikisoma Ujiji Government Town School na Aman akiwa Kipampa Lower Primary School.
Sote tulikutana Kipampa Middle School mwaka 1962.Tulisoma hapo kwa miaka minne hadi tulipohitimu darasa la nane mwaka 1965 na kujiunga na elimu ya sekondari pale Livingstone College mwaka 1966.
Kifo cha Dk Kabourou kimenikumbusha mikimiki ya pale Livingstone hadi kusababisha kukatiza masomo tukiwa tumehitimu kidato cha tatu tu. Hapa leo sio mahala pa kuelezea hiyo mikimiki bali kumuomboleza Dk Aman Kabourou.
Baada ya kutoka shule hiyo 1968, mimi nilielekea Dar es Salaam kutafuta maisha ambapo mwezi Mei 1969 nilipata ajira ya muda Shirika la Reli la Afrika Mashariki(EARC) wakati nasubiri kwenda Nairobi, Kenya kuchukua mafunzo ya Ufundi Mitambo ngazi ya cheti mwaka uliofuata. Jambo lililofanikiwa kwa msaada wa Mhandisi Juma Omari Lweno aliyekuwa Mhandisi Mitambo (Mkoa wa Tanzania). Ikumbukwe nilikuwa nimeishia kidato cha tatu hivyo mafunzo hayo yalinichukua miaka minne ikijumuisha miaka miwili ya mafunzo kwa vitendo.
Wakati mimi nashughulika na ajira na mafunzo, Aman alibaki Ujiji akimsaidia baba yake katika biashara ya nguo za mitumba. Hapa ni vyema kutambua kuwa enzi zile nguo za mitumba zilikuwa zinaingizwa Tanzania kutokea Burundi pamoja na kwamba ilikuwa inapitishiwa bandari ya Dar es Salaam. Kwa ufupi nchini Tanzania miaka ya katikati ya 1960s hadi ile ya 1980s nguo za mitumba zilikuwa zinauzwa kiuficho.
Mwaka 1972 nilirejea Dar es Salaam kwa ajili ya muhula wa kwanza wa mazoezi kwa vitendo. Kwa urahisi wa kuwa jirani na karakana (Kituo Cha Reli, Dar es Salaam) nilipanga chumba Mtaa wa Aggrey, nyumba Na 97 ambayo ndugu Bakhresa baadae aliinunua na hivi sasa ni moja ya ofisi au maeneo ya shughuli zake.
Wakati nikiishi hapo na kama kumbukumbu zangu zinaniongoza vizuri, mwishoni mwa mwezi Machi, 1972 ndugu Aman aliamua kuachana na biashara ya mitumba akaja Dar es Salaam tukaishi pamoja (chumba hicho hicho kimoja). Lengo lake likiwa kutaka kujiendeleza kielimu.
Alipokuja kujiunga nami pale Aggrey, ndugu Aman alinikuta nahudhuria masomo ya jioni kwenye Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, Lumumba (kwenye jengo kilpoanzia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam). Pale niliamua kusoma mambo matatu ambayo ni masomo ya "O Leval" ambayo nilikatizwa shuleni nakufanya mtihani wa "London GCE" ambao nilifanyia Nairobi huku nikiebdelea na masomo ya Reli. Pia nilikuwa najifunza "Creative Writing" iliyonisaidia katika masomo ya stashada (Diploma ya Uandishi wa Habari ambayo nilihitimu Novemba 1976. Kadhalika nilijifunza Kifaransa lugha ambayo nilijifunza hadi Chuo Kikuu.
Ndugu Aman alifurahishwa sana aliponikuta najiendekeza kielimu. Nakumbuka aliwahi kuniambia kwamba ni lazima tujielimishe ili tuthibitishe kuwa kule Livingstone College hatukwenda kwa bahati mbaya na kwa yeyote aliyetufitini ajiulize kwa nini alifanya hivyo.
Ndugu Aman alilenga kusoma nje ya nchi. Hivyo kila siku asubuhi hadi saa mbili usiku (Jumatatu hadi Ijumaa) alishinda Maktaba ya Taifa akijisomea mambo mbali mbali ya utashi wake. Ni huko Maktaba ya Taifa ndiko kulikopatikana njia yakuelekea kupata shahada ya Uzamivu (Ph D).
Akiwa "mwanafunzi" wa maktaba alikutana na Wamarekani Weusi ambao walimuomba awafundishe Kiswahili;na katika kutekeleza hilo waliweza kumpatia wepesi wakwenda kuishi Marekani kupitia Ethiopia na Italia.
Ndugu Aman aliondoka nchini Oktoba,1972.
Kabla hajaondoka aliniusia haya "MZEE MSAMBYA (pamoja na umri wetu mdogo na wa ujana miaka ile alipenda kuniwakilisha kwa heshima ya Mzee na amekuwa akinichukulia hivyo maisha yake yote) INABIDI TUPATE ELIMU KWA NAMNA YEYOTE ILI NASISI TUWE SEHEMU YA UONGOZI WA NCHI YETU.
Na imekuwa hivyo maana sote tumekuwa wabunge (yeye Kigoma-Ujiji) mimi Kigoma Kusini.Dk Kabourou aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Chadema(Taifa)na hivi karibuni alikuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kigoma. Kwa upande wangu nimewahi kuwa Naibu Waziri (Nishati & Madini) na takriban miaka miwili nyuma nilikuwa Mkuu wa Wilaya. Hizo ni nafasi za uongozi kama alivyobashiri Ndugu Aman Walid Kabourou.
Nikiri kuwa kuishi kwangu pamoja nae ule mwaka 1972 kulikuwa chachu ya baadhi ya mafanikio yangu.
Ndugu Aman baada ya kuhitimu shahada ya Uzamivu (Ph D) alifanyakazi Marekani kwa muda mfupi na mnamo mwaka 1993 mwishoni alirejea nyumbani na kushiriki harakati za siasa na kuwa Mbunge kwa takriban miaka 10 kuanzia 1995.
Kurejea kwa Dk Kabourou nchini na kujiunga na siasa kuliweza kuwa chachu kwa vijana si tu wa Kigoma bali nchini kote.
Kwa Kigoma Dk Kabourou atakumbukwa kwa jinsi alivyokuwa mvuto kwenye mikutano yake ama ya kampeni au ya kawaida. Mvuto huo uliwezesha akapewa jina RUKUGA ambao ni moja kati ya pepo kali zivumazo ndani ya Ziwa Tanganyika na ambazo wavuvi na wenye vyombo vya ussfiri majini huzigwaya sana.
Dk Kabourou atakunbukwa kwa kufufua mkusanyiko wa vijana waogeleaji kwenye mchezo maarufu wa AIFOLA.
Kumuelezea Ndugu Amani Walid Kabourou sio kwepesi kama inavyoweza kudhaniwa na kwa mimi ambae tunayo historia ya kipekee baina yetu.
Itoshe nihitimishe kwa yafuatayo kuwa binafsi nimesononeshwa kwakutopata wasaa wakushiriki mazishi yake,lakini hii imetokana na afya yangu kutokuwa nzuri.Hata hvyo. Nichukue fursa hii kumpa pole mjane pamoja na watoto wote wakiwemo Vyema,Walid Aman Walid Kabourou Jr na wengine wote.
Aidha niwafariji ndugu jamaa na wote walioguswa na kuondoka kwa mpendwa wetu. Kikubwa tumuombee safari yake ya mwisho iwe nyepesi na ALLAH amsamehe makosa yake na kwa wana Kigoma tutafakari namna bora ya kumuenzi ndugu yetu.
Wala tusiseme RUKUGA amepoa na kwamba amekuwa AIFOLA MWENDA SALAMA.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni