UN WAINGIA MAKUBALIANO NA SERIKALI KUTANGAZA MPANGO WA MAENDELEO


UMOJA wa Mataifa umeingia makubaliano ya kuimarisha upatikanaji na usambazaji wa habari za maendeleo na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na chama cha Maafisa Mawasiliano Serikalini (TAGCO).

Makubaliano hayo yamelenga kuimarisha upatikanaji na utoaji habari wa pamoja kuhusu mpango wa maendeleo wa miaka mitano wa serikali na malengo ya maendeleo endelevu ya dunia.

Kwa mujibu Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa Bw. Alvaro Rodriguez makubaliano hayo yatachagiza kupatikana kwa habari kuhusiana na utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu unaokwenda sambamba na mpango wa maendeleo wa miaka mitano wa Tanzania.

Akizungumzia malengo hayo kwa maofisa wa mawasiliano wa serikali wanaokutana mjini Arusha kwa semina ya wiki moja iliyoandaliwa kwa pamoja kati ya TAGCO na Wizara ya Habari na kufadhiliwa na Umoja wa Mataifa, alisisitiza kuwa malengo hayo yanahitaji kuwasilishwa kwa wananchi na pia kupigiwa chapuo.

Aliwataka maofisa mawasiliano hao wa serikali kufanyakazi ya uragibishi na pia kuwasiliana ana kwa ana na jamii kuhusu masuala mtambuka kama kuhifadhi mazingira,kuondoa tatizo la ukeketaji (FGM) na kupambana na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto katika kufanikisha mpango wa maendeleo wa kitaifa na ule wa dunia.

Kwa upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi Mkuu wa Maelezo Dk. Hassan Abbas alisema kwamba kwa sasa wizara ya habari iko katika mchakato wa kuandaa makubaliano na Umoja wa Mataifa yatakayogusa masuala ya mawasiliano katika utekelezaji wa mpango wa pili wa miaka mitano wa maendeleo m na malengo ya maendeleo endelevu ya dunia.

Aidha alisema semina hiyo itawapatia mafunzo mengi maofisa hao ikiwa ni pamoja na kutembelea maeneo yenye miradi iliyopata mafanikio na kujenga athari chanya kwa jamii.

Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Bw. Alvaro Rodriguez akiwasilisha mada kuhusu malengo ya maendeleo ya milenia na uhusiano wake na mpango wa maendeleo wa miaka mitano wakati wa mkutano wa 14 wa Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini unaoendelea Jijini Arusha.
Ofisa Habari wa taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa Takukuru akiuliza namna ambavyo mapambano dhidi ya rushwa yanavyoweza kuwa sehemu ya utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu.
Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Bw. Alvaro Rodriguez (kushoto) na Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bi Suzan Mlawi (kulia) wakifuatilia mada kuhusu malengo ya maendeleo ya milenia na uhusiano wake na mpango wa maendeleo wa miaka mitano wakati wa mkutano wa 14 wa Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini unaoendelea Jijini Arusha.
Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi Mkuu wa Maelezo Dk. Hassan Abbas akizungumza na waandishi wa habari nje wakati wa mkutano wa 14 wa Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini unaoendelea Jijini Arusha.
Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini wakifuatilia mada kuhusu malengo ya maendeleo ya milenia na uhusiano wake na mpango wa maendeleo wa miaka mitano ikiwasilishwa na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Bw. Alvaro Rodriguez hayupo pichani katika mkutano huo wa 14 unaoendelea jijini Arusha.
Sehemu ya washiriki wakati wa mkutano wa 14 wa Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini unaoendelea Jijini Arusha.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni