BAADHI YA MADUKA YA WAFANYABIASHARA MNARANI -LOLIONDO KIBAHA YAFUNGWA KWA KUSHINDWA KULIPA KODI


IMG-20180905-WA0011
Baadhi ya maduka ya wafanyabiashara katika soko la Mnarani, Loliondo halmashauri ya Mji wa Kibaha Pwani yakiwa yamefungwa kutokana na kushindwa kulipa kodi.
Picha na Mwamvua Mwinyi
……………………..
NA MWAMVUA MWINYI,KIBAHA
MADUKA ya baadhi ya wafanyabiashara wa soko la Mnarani ,Loliondo ,halmashauri ya Mji wa Kibaha ,Pwani ,yamefungwa kwa siku tatu baada ya kushindwa kulipia kodi kwa zaidi ya mwaka sasa.
Kufuatia kufungwa kwa maduka hayo ,wameiomba ofisi ya mkuu wa mkoa huo iingilie kati suala hilo kwani wanatakiwa kulipa sh.8,000 kwa mita za mraba kiasi ambacho ni kikubwa kwao.
Mfanyabiashara aliyefungiwa duka lake ,Henry Makundi alisema wamehamishiwa kutoka Maili Moja stendi na kupewa maeneo Loliondo ili wajenge maduka na fedha zao watafidia kwenye kodi.  
Alieleza, walikuwa wanataka kuwe na mafungu matatu ya malipo moja ya tatu mkurugenzi na moja ya tatu mfanyabiashara na moja ya tatu iwe ya mfanyabiashara kama wawekezaji moja ya tatu iwe kama faida.
Makundi alielezea ,halmashauri inataka asilimia 50 na mfanyabiashara 50 ili kurudisha gharama jambo ambalo hawakubaliani nalo.
Nae mwenyekiti wa soko hilo ,Ramadhan Maulid alishangaa kuona maduka yanafungwa .
Alisema kwamba,kulikuwa na makubaliano walipe mita za mraba 4,000 huku akiwepo mkurugenzi na mbunge wa mji huo hivyo wanashangaa kuambiwa walipie sh 8,000.
Maulid alifafanua, kutokana na hali hiyo wanaendelea na mazungumzo na katibu tawala wa mkoa ili kuangalia namna ya kulishughulikia suala hilo .
Akijibu hoja za wafanyabiashara hao mkurugenzi wa halmashauri ya Mji wa Kibaha Jeniffer Omolo alisema ,walikubaliana kuwa wafanyabiashara wajenge maduka kwa gharama ya sh .milioni tano na halmashauri walitoa ardhi lakini hawajalipa kodi zaidi ya mwaka sasa.
Kwa mujibu wake ,wamegundua wengi wanaofanya biashara ni wapangaji na sio waliojenga maduka ambayo wanapangisha kuanzia sh.300,000 hadi sh.400,000 kwa mwezi.
Jennifer alibainisha ,kwa mwaka wanapata kati ya sh.milioni 3.6 – milioni 4.8 kwa miaka miwili anakuwa amerejesha gharama zake za ujenzi .
Mkurugenzi huyo aliwataka ,wale ambao gharama zimezidi ya waliyokubaliana waende ofisini kwake kwa ajili ya mazungumzo.
Jennifer alielekeza ,wafanyabiashara ambao hawajalipa kodi kulipa kwani kutolipa kodi ni kinyume cha sheria , ili waepukane na usumbufu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni