TUMENUFAIKA NA MKUTANO WA FOCAC-MAJALIWA




































WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Tanzania imepata mafanikio makubwa kutokana na kushiriki kwake katika Mkutano wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC).

Amesema kikao hicho kimekuwa na tija kwa Tanzania kutokana na maeneo ya vipaumbele yaliyojadiliwa katika mkutano huo hususani masuala ya uwekezaji kwenye sekta ya viwanda.

Waziri Mkuu aliyasema hayo jana (Jumatano, Septemba 05, 2018) alipokutana na waandishi wa habari katika kikao cha majumuisho ya ziara yake ya kikazi China ambako alikwenda kumuwakilisha Rais Dkt. John Magufuli kwenye mkutano wa FOCAC. 

Alisema maeneo yaliyopewa kipaumbele katika mkutano huo ni masuala ya usalama wa nchi, maendeleo ya kiuchumi hususani uboreshaji wa sekta ya viwanda, elimu, kilimo, afya, elimu na teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA).

“Kikao hiki kimekuwa na tija kwa Tanzania kwa sababu maeneo yote yaliyojadiliwa ni muhimu kwetu. Tumeanza kuona idadi nzuri ya wawekezaji kutoka China na ni matokeo ya mpango uliowekwa katika kikao cha kwanza cha FOCAC kilichofanyika Afrika Kusini.”

Waziri Mkuu alisema maeneo mengine yaliyopewa kipaumbele ni pamoja na sekta ya madini, mifugo na uvuvi, ambazo nazo zimewekewa mikakati ya namna ya kuziboresha ili ili ziweze kuchangia ukuzaji wa uchumi katika mataifa hayo.

Kadhalika, Waziri Mkuu alisema kikao hiko pia kilijadili namna ya kuboresha sekta ya utalii kwa kuvutia watalii kutoka za Afrika na nje ya bara hilo ikiwemo na China, hivyo Tanzania inatakiwa kutumia fursa fursa zilizopo kuvutia watalii kutoka nchi mbalimbali.

Alisema ushirikiano huo unaanza mara moja na China imetenga dola bilini 60 za Marekani kwa ajili ya kusaidia Afrika ili ziweze kuboresha maeneo hayo yaliyoainishwa. Tanzania inatakiwa kutumia vizuri fursa hiyo.

Pia Waziri Mkuu alisema atakaporejea nchini ataitisha kikao cha kazi cha Mawaziri na kutoa maelekezo kwa mawaziri wote ambao sekta zao zimeguswa kwenye mpango wa FOCAC ili waweze kuandaa utaratibu mzuri wa namna tukavyonufaika na fedha hizo.

“Watanzania tushirikiane kwa pamoja na watendaji katika wizara zote ili tuweze kujipanga vizuri. Wataalamu katika kila sekta waweke mpango kazi utakaokwenda kuhitaji fedha hizo kwa ajili ya kuimarisha sekta husika ili maeneo yote yapate tija.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amempongeza Rais wa China, Xi Jinpingkwa kuitambua Tanzania kama moja kati ya nchi rafiki wa muda mrefu wa China na kuipa kipaumbele kwenye mkakati wa kuwekeza kwenye viwanda.

Alisema wawekezaji wengi kutoka China wamedhamiria kuja Tanzania kujenga viwanda na kuviendesha kwa kutumia teknolojia ya kisasa zaidi ili viweze kuzalisha kwa uhakika na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo. 

Waziri Mkuu alisema tayari Tanzania ilishafanikiwa katika mkakati wa kuboresha mazao makuu matano ya biashara ambayo ni korosho, chai, kahawa, pamba na tumbaku na sasa imejipanga kuboresha mazao ya mbegu za kuzalisha mafuta na ameitaka mikoa husika ifuatilie mazao hao ambayo ni michikichi, alizeti na ufuta.

Mkutano huo wa FOCAC wa siku mbili ulifunguliwa Jumatatu, Septemba 03, 2018 jijini Beijing China na Rais wa China, Xi Jinping. Ulihudhuriwa na viongozi wakuu wa nchi 53 kutoka Afrika.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, SEPTEMBA 06, 2018.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni