TADB Yawanufaisha Wakulima 527,291


5
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe.  Dkt. Mary Mwanjelwa akieleza mikakati ya Serikali katika kuinua sekta ya kilimo hapa nchini wakati wa kipindi cha maswali na majibu leo Bungeni Jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Kilimo, Dkt. Mary Mwanjelwa
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Hadi kufikia Julai, 2018 Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) imewanufaisha jumla ya wakulima 527,291 kwa kuwapa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 48.67.
Takwimu hizo zimetolewa leo na Naibu Waziri wa Kilimo, Dkt. Mary Mwanjelwa alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Magomeni, Mhe. Jamal Kassim Ali lililohoji juu ya mikakati ya Serikali ya kuwasaidia wakulima kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo.
Naibu Waziri Dkt. Mwanjelwa amesema serikali inatambua changamoto za upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya shughuli za kilimo zinazotokana na taasisi nyingi za fedha kuweka masharti magumu hususan kwa waombaji kutoka sekta ya kilimo ndio maana Benki hiyo inajitahidi kutafuta vyanzo vipya vya mtaji ili kuimarisha uwezo wa benki kuwahudumia wakulima.
“Ili kuwaendeleza wakulima, Serikali itaendelea kuiongezea mtaji Benki ya TADB na kuhamasisha uanzishwaji na usimamizi wa Vyama vya Ushirika ili kuwezesha upatikanaji wa mikopo nafuu kwa wakulima, hadi kufikia Julai 2018 jumla ya wakulima 527,291 katika mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe, Morogoro, Tanga, Manyara, Kagera, Arusha, Zanzibar na mikoa ya Kanda ya Ziwa walipatiwa mikopo,” alisema Dkt. Mwanjelwa.
Ameongeza kuwa Serikali imeweka mikakati mbalimbali ikiwemo ya kuipatia benki ya kilimo mkopo wa gharama nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika wa shilingi bilioni 103, kufadhili miradi ya ubunifu vijijini pamoja na kuratibu utoaji wa dhamana kwa mikopo itakayotolewa  na mabenki na taasisi nyingine za fedha.
Aidha, Naibu Waziri wa Kilimo amefafanua juu ya uongezaji wa matawi ya benki hiyo nchini ambapo katika Mwaka wa Fedha 2018/19, Serikali imepanga kuanzisha Ofisi sita za kanda zikiwemo za Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Magharibi lakini Kanda za Kusini, Kaskazini na Zanzibar zitafunguliwa baadae.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni