Ofisa wa Mamlaka ya Mapato nchini TRA mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Castory Henry akizungumza kwenye kikao na madalali wa madini ya Tanzanite.
Ofisa madini mkazi wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Daudi Ntalima akizungumza kwenye kikao cha madalali wa madini ya Tanzanite.
Mwenyekiti wa Umoja wa madalali wa madini ya Tanzanite wa Mkoa wa Manyara (Magebomita) Ernest Wasonga akizungumza kwenye kikao cha wanachama wao Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro.
Baadhi ya madalali wa madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wakiwa kwenye kikao kilichoitishwa na viongozi wa umoja wa madalali wa mkoa huo (Magebomita).
MADALALI wa madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara wamewalalamikia watathmini wakadiriaji wa madini hayo kwa kukadiria bei ya juu pindi wanapopita nayo kwenye lango la ukuta unaozunguka migodi ya Tanzanite, hivyo kuwasababishia hasara.
Madalali hao walilalamikia tatizo hilo kwenye kikao cha chama cha madalali wa madini ya Tanzanite mkoa wa Manyara, (Magebomita) kilichofanyika ukumbi wa Songambele mji mdogo wa Mirerani.
Mmoja kati ya madalali hao Vincent Peter alisema serikali inapaswa kuweka umakini kwenye hilo kwani madalali wengi wamepata hasara kwa kukadiriwa bei kubwa tofauti na thamani halisi ya madini aliyonayo.
Peter alisema wakadiriaji wanapaswa kukadiria bei halali ili madalali walipe kodi halali ya serikali kwa kuthaminishiwa bei ambayo inapaswa kulipwa tofauti na ilivyo sasa kwani uthaminishaji unafanywa tofauti na bei halisi.
“Hawa wathaminishaji wa madini ya Tanzanite wanakosea mno kwani jiwe lenye thamani ya sh800,000 wanakadiria kwa sh4 milioni, mmewatoa Mbeya kwenye ndizi ndiyo wakaja Mirerani kukadiria madini ya Tanzanite,” alihoji Peter.
Makamu Mwenyekiti wa Magebomita, Sammy Chacha Opong alisema madini ya Tanzanite yanataka utaalamu pindi yakikadiriwa kwani yapo tofauti na madini mengine ya vito hivyo wakadiriaji wanatakiwa kuwa na weledi juu ya hilo.
Opong alisema madalali wengi wamewalalamikia ukadiriaji unaofanywa hivi sasa kwenye lango la kuingia ndani ya ukuta hivyo ni jukumu la serikali kusimamia hilo ili wadau wasizidi kuumia kwa kupata hasara.
“Pamoja na hayo kuna changamoto ya ucheleweshaji wa kutolewa kwa leseni za madalali ambazo zimechukua muda mrefu kupata pindi wanapolipia kwani hulipia mwezi Julai lakini husubiri mno,” alisema.
Hata hivyo, ofisa madini mkazi wa Mirerani, Daudi Ntalima alisema wakadiriaji hao ni wataalamu waliobobea na hupanga bei halisi pindi wanapofanya tathimini ya madini ya Tanzanite ili muuzaji asiende kupata bei ndogo hivyo kupunjwa.
Ntalima alisema endapo dalali akibaini tathimini anayofanyiwa kwenye madini yake ni tofauti na thamani halisi ana haki ya kupinga kwa kuandika barua ili uthaminishaji ufanyike upya.
Ofisa wa mamlaka ya mapato nchini (TRA) wa mji mdogo wa Mirerani, Castory Henry alisema madalali wa madini ya Tanzanite walipo kwenye vikundi vyao wakati wa kufanya biashara hiyo wanaweza kupatiwa leseni.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni