Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akijibu maswali katika kikao cha Bunge leo Jijini Dodoma.
Na Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
Serikali imeeleza kuwa inazingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo, Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala (ccm), Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano na mwaka mmoja, pamoja na Mwongozo wa Bajeti kugawa rasilimali fedha na watu katika kukabiliana na changamoto za umaskini nchini.
Hayo yameelezwa Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) alipokuwa akijibu maswali ya Mbunge wa Kasulu Mjini Mhe. Daniel Nicodemus Nsanzugwanko (CCM), aliyetaka kujua mbinu za Serikali katika kuhakikisha mikoa maskini nchini inapata rasilimali fedha na watu ili iweze kuondokana na hali hiyo ya umaskini.
Dkt. Kijaji alisema kuwa mgawanyo wa rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo huenda sambamba na mgawanyo wa rasilimali watu kwa ajili ya utekelezaji, usimamizi, uperembaji na kutoa huduma kulingana na aina ya miradi.
Aidha Mhe. Nsanzugwanko alihoji hatua zilizochukuliwa na Serikali katika Mkoa wa Kigoma ili kujenga ulinganifu katika maendeleo.
Akijibu swali hilo Dkt. Kijaji alisema Serikali imebainisha maeneo na miradi ya kimkakati kwa ajili ya utekelezaji ili kufungua fursa za kiuchumi mkoani huo.
Alieleza kuwa miongoni mwa maeneo ya kimkakati yaliyobainishwa na kuanza kutekelezwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17-2020/21 ni pamoja na mradi wa upanuzi na ujenzi wa Uwanja wa Ndege Kigoma.
“Miradi mingine ni mradi wa uzalishaji wa umeme wa maji katika maporomoko ya mto Malagarasi MW 44.7, kuanzisha na kuendeleza eneo huru la uwekezaji Kigoma, mradi wa gridi ya Kaskazini Magharibi kv400 na ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha kimataifa”, alisema Dkt. Kijaji.
Katika swali jingine, Mhe. Nswanzugwanko alitaka kujua kwa nini Serikali isitenge shilingi bilioni 5 kila mwaka kwa kila mkoa ili kuondoa tishio la mikoa hiyo kuachwa nyuma kimaendeleo.
Mhe. Dkt. Kijaji alieleza kuwa kwa sasa Serikali haina sera wala mwongozo wa kutenga shilingi bilioni 5 kila mwaka kwa kila mkoa ili kukabiliana na changamoto za umasikini.
Alifafanua kuwa hoja ya kutenga shilingi bilioni 5 kwa kila mkoa kila mwaka ni lazima ifungamanishwe na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni