MSAFARA wa Rais John Magufuli uliokuwa ukielekea wilayani Ukerewe mkoani Mwanza, umepata ajali katika kijiji cha Kasuguti, kata ya Kisorya, wilayani Bunda mkoani Mara, leo Septemba 4, 2018 baada ya magari manne kugongana katika eneo ambalo barabara ilikuwa ikijengwa.
Taarifa za awali zinadai kuwa waandishi wawili wa habari wamejeruhiwa baada ya gari walimokuwa kupinduka.
Kwa mujibu wa Mkuu Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Mara, R.T.O Steven, akizungumza na Global TV Online, pamoja na kuthibitisha kutokea kwa ajli hiyo, miongoni mwa magari yaliyopata ajali, mojawapo ni la waandishi wa habari na jingine ni la Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Amesema chanzo cha ajali hiyo ni vumbi lilikuwa limetapakaa barabarani kutokana na msafara huo hivyo madereva kushindwa kuona vizuri njia lakini hakuna madhara makubwa licha ya gari moja kubondeka ubavuni baada ya kupinduka.
Ameongeza kuwa magari yote yameshafika eneo ambalo Rais Magufuli amekwenda kufanya ziara na hakuna taarifa ya mtu aliyepelekwa hospitali kwa kuumia.
Taarifa nyingine kutoka eneo la tukio zinadai kwamba gari jingine lililopata ajali ni la Chama Cha Mapinduzi (CCM) la mkoa huo.
Majeruhi wa ajli hiyo ni watu wawili ambao ni Neema Emmanuel, waandishi wa Gazeti la Nipashe ambaye ameumia kichwani na Tunu Heriman ambaye alipata mshituko tu lakini kwa sasa wote wanaendelea vizuri
CREDIT:Global TV Online
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni