Baada
ya kupita miaka miwili bila kuchezwa kwa mashindano ya kuwania Kombe la
Chalenji kwa nchi za Afrika Mashariki, michuano hiyo imerejea tena msimu
huu na Tanzania imethibitisha kushiriki.
Nchi wanachama Tanzania Bara, Zanzibar, Uganda, Kenya, Burundi, Rwanda, Somalia, Sudan, Sudan Kusini, Eritrea na Ethiopia.
Kaimu
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Kidao
Wilfred amethibitisha kikosi cha kwanza cha ‘Taifa Stars’ kushiriki na
matarajio ya kufanya vema michuano hiyo itakayofanyika kuanzia Novemba
25, 2017 hadi Desemba 9, mwaka huu.
Kidao
amesema kwamba uteuzi wa timu za kwanza kwa kila nchi mwanachama wa
Baraza la Mpira wa Miguu la Afrika Mashariki ni makubaliano ya viongozi
wa CECAFA waliokutana kwa pamoja huko Sudan, Septemba, mwaka huu.
Kutokana
na makubaliano hayo ya kuita timu za kwanza, michuano hiyo itaathiri
kidogot ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kwa kuwa
wachezaji wengi wanaounda kikosi hicho, wanatoka timu za VPL.
Mtendaji
Mkuu wa Bodi ya Ligi (TPLB), Boniface Wambura amesema: “Tutakaa kama
kamati na kuangalia siku ya Jumatano na Alhamisi baada ya michuano hiyo
na kupanga ratiba ya mechi ambazo zitapanguliwa wakati wa michuano ya
Chalenji.”
Mbali ya
michuano hiyo, Tanzania imethibitisha kushiriki michuano ya Chalenji ya
vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 itakayofanyika Bujumbura nchini
Burundi kuanzia Desemba 12, 2017 hadi Desemba 22, mwaka huu.
Kadhalika,
Tanzania imethibitisha kushiriki michuano ya Chalenji kwa wanawake
ikienda kutetea taji katika michuano itakayofanyika Rwanda mwezi
Desemba, mwaka huu. Tarehe rasmi itatajwa baadaye.
CECAFA
imeamua kurejesha hadhi yake kwani mara baada ya michuano ya Chalenji ya
vijana huko Burundi, mwakani itakuwa ni zamu ya Tanzania ambako
michuano hiyo inatarajiwa kuanza Agosti 11, 2018 hadi Agosti 25,
mwakani.
Wakati
huo huo Kidao amethibitisha Tanzania kuwa wenyeji wa mashindano ya
Vijana ya Chalenji ya CECAFA/CAF kwa vijana chini ya miaka 17 mwakani na
mashindano hayo yatatumika kama sehemu ya kufanya maandalizi Fainali za
Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 17
(AFCON – U17).
Michuano
ya mwakani ina baraka za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa sababu
shirikisho hilo linataka kutumia michuano hiyo ya vijana ya Kanda
mbalimbali za Afrika kupata timu saba katika michuano AFCON – U17 ya
mwaka 2019.
Kanda
hizo ni CECAFA (Afrika Mashariki), COSAFA (Nchi za Kusini mwa Afrika),
WAFU – UFOA (Afrika Magharibi); UNAF (Afrika Kaskazini) na UNIFFAC
(Afrika ya Kati).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni