NEC yaanza kutekeleza mpango wa Elimu ya Mpiga Kura kupitia Redio

Hussein Makame, NEC 

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetoa wito kwa wananchi walioko kwenye halmashauri mbalimbali nchini, kuitumia vyema fursa ya utoaji wa elimu ya mpiga kura kupitia redio za kijamii kwenye halmashauri zao ili kuondoa manung’uniko kwenye chaguzi.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume hiyo Bw. Kailima Ramadhani wakati akizungumzia mpango wa kutoa elimu ya mpiga kura nchi nzima ulioanza kutekelezwa Mei 8 mwaka huu hii katika mikoa kumi nchini.
Alisema kupitia mpango huo wananchi wanaosikiliza redio za kijamii kwenye halmashauri nchini, watapata fursa ya kujifunza elimu ya mpiga kura na kuelewa masuala yote muhimu yanayohusu mfumo mzima wa kupiga kura. 

“Tumepanga mpango, Tume itasambaa nchi nzima kuzungumzia elimu ya mpiga kura kwenye redio za kijamii zilizoko kwenye halmashauri zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.” alisema Bw. Kailima.

Alisisitiza kwa kutoa wito kwa wananchi walioko maeneo ambayo Tume itakwenda kutoa elimu ya mpiga kura, wasikilize na kuuliza maswali ili waweze kuelewa.

“Hii ni fursa kwa wananchi ambayo muda mrefu hawajawahi kuipata, hivyo nawaomba wafuatilie ili waweze kuelimika zaidi ili yale manung’uniko ya kura yatakuwa yamekwisha na tutakuwa na uchaguzi mzuri zaidi ya ile ambayo tumeifanya.” Alifafanua Bw. Kailima.

Utekelezaji wa mpango huo umegawanyika katika makundi matatu ambapo kundi la kwanza limeanza kutoa elimu hiyo elimu hiyo kwenye mikoa ya Kagera,Mwanza, Kilimanjaro, Morogoro, Mbeya na Dodoma.

Mikoa mingine itakayojumuishwa kwenye kundi hilo ni Ruvuma, Mara, Pwani na Mtwara ambapo elimu hiyo itatolewa kuanzia tarehe 8 Mei hadi tarehe 20 Mei mwaka 2017.

Kundi la pili linatarajiwa kutoa elimu hiyo kuanzia tarehe 24 Mei hadi tarehe 7 Juni mwaka huu katika mikoa ya Geita, Tanga, Singida, Shinyanga, Lindi, Arusha, Tabora, Kigoma, Iringa, Manyara, Rukwa, Katavi, Songwe, Njombe na Simiyu.

Bw. Kailima alisema kuwa utoaji wa elimu hiyo utajikita kwenye mada kuu ya Elimu ya Mpiga Kura iliyogawanywa kwenye vipindi vitano, itakaytoolewa kwenye redio hizo kulingana mada husika na wananchi kuuliza maswali na kujibiwa na wawasilishaji wa mada hizo kutoka Tume.

“Ni mada ambayo imejumuisha masuala yote muhumu yatakayofanya mpiga kura yeyote au mdau yeyote wa uchaguzi kuisoma au kuisikiliza na akaelewa mfumo mzima wa masuala ya kupiga kura” alisema.

Mbali na kutoa elimu ya mpiga kura kupitia vituo vya redio za kijamii katika halmashauri nchi nzima, Tume pia inatoa elimu hiyo kwa njia ya magazeti na vyombo vingine vya habari na mitandao ya kijamii, kushiriki kwenye mikutano na maonesho mbalimbali nchini.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Bw. Kailima Ramadhani akitoa elimu ya mpiga kura kupitia redio A FM ya mkoani Dodoma leo Mei 9 mwaka huu huku akifuatiliwa kwa makini na watangazaji wa redio hiyo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni