Kundi la waandishi kumi wa habari kutoka nchini Israel wakiwa katika hifadhi ya Taifa ya Gombe hivi karibuni kwa ajili ya kurekodi vivutio mbalimbali vya utalii vinavyopatikana katika hifadhi hiyo kwa ajili ya kuvitangaza nchini kwao ikiwa ni mkakati wa Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Bodi ya Utalii Tanzania kwa kushirikiana na Hifadhi za Taifa (TANAPA). Kwa sasa soko la utalii la mashariki ya kati limeanza kufunguka kwa kasi ambapo hivi karibuni Waziri Mkuu Mstaafu wa Israel Ehud Barak ametembelea hifadhi za Ngorongoro na Serengeti.
HAMZA TEMBA - WMU
Kundi la wanahabari kumi
akiwemo muigizaji mmoja na maofisa wa kampuni ya utalii ya Safari kutoka nchini
Israel limetembelea hifadhi ya Taifa ya Gombe iliyopo mkoani Kigoma na kufurahia
vivutio lukuki vya utalii vinavyopatikana katika hifadhi hiyo na kuahidi
kuvitangaza watakaporudi nchini kwao ikiwa ni mkakati wa Wizara ya Maliasili na
Utalii kupitia TANAPA na Bodi ya Utalii kutangaza vivutio hivyo nchini humo.
Akizungumza hivi karibuni mara
baada ya kukamilika kwa ziara hiyo ya siku mbili, Kiongozi wa kundi hilo, Ronit
Hershkovitz alisema ziara hiyo imekuwa na mafanikio makubwa ambapo wamefurahia
kuona vivutio vya kipekee katika hifadhi hiyo na kuahidi kuwa mabalozi wazuri
wa vivutio hivyo nchini Israel.
Timu
maalum ya wanahabari kutoka nchini Israel ikiwa na wajumbe kumi
ilipowasili katika uwanja wa ndege wa Kigoma tayari kwa ajili ya ziara
ya kitalii ya siku mbili katika hifadhi ya Taifa ya Gombe. Ziaza hiyo
iliandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Bodi ya Utalii
Tanzania (TTB) kwa kushirikiana na Shirika ya Hifadhi za Taifa Tanzani
(TANAPA) kwa ajili ya kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania nchini
Israel ikiwa ni mkakati maamlum wa kukamata soko la Mashariki ya Kati.
Kutoka kulia wanaongoza msafara huo ni Meneja Mawasiliano TANAPA,
Paschal Shelutete na Meneja Mahusiano wa TTB, Geofrey Tengeneza.
“Ni furaha kubwa kuwa hapa
Gombe, tumeona makundi ya Sokwe na fukwe nzuri za Ziwa Tanganyika, tuko hapa
kwa ajili ya kwenda kueleza kivutio hiki na vivutio vingine vya Tanzania nchini
Israel, Waisrael wanaipenda Tanzania na wanapenda kutembelea Tanzania, tumeona
ongezeko kubwa la watalii katika miaka ya hivi karibuni kutoka Israel baada ya
kazi ngumu ya muda mrefu, sasa tuna furaha kuona watalii wengi wanaongezeka na
tungependa kuona pia Watanzania wengi wakitembelea Israel,” Alisema Ronit.
Aliongeza kuwa, “Tunaenda
kueleza taarifa hizi kwenye mitandao ya kijamii, magazeti, televisheni na
popote tutakapoweza, lakini kubwa zaidi ni kuwaeleza marafiki zetu ana kwa ana
uzuri wa Tanzania kwasababu tunaipenda Tanzania, nakupenda sana”.
Wanahabari
kutoka Israel wakipanda kwenye boti kwa ajili kunza safari kuelekea
hifadhi ya Taifa ya Gombe. Msafara huo ulikuwa na wanahabari kutoka
vyombo maarufu nchini humo ikiwemo kituo cha Televisheni cha Channel 2,
Jarida la Atmosphere, Jarida la National Geographic, Jaria la wiki la
Yediot Acharanot -7 Yamim na waandishi wawili wa mitandao ya kijamii.
Wengine ni maofisa wawili wa kampuni ya Utalii ya Safari ya nchini
humo.
Walfson Noa, ambaye ni
Mwandishi wa Mitandao ya Kijamii na Meneja Masoko wa Kampuni ya Utalii ya
Safari ya Israel alisema, “Tulifanya matembezi kuwaona Sokwe wanaovutia sana huku
wakiishi katika mazingira yao ya asili, hili ziwa ni la maajabu sana (Ziwa
Tanganyika), hata nyani nao walikuwa wakijaribu kuingia kwenye mahema yetu ni
jambo la kuvutia, katika mtizamo wa kimasoko hili ni eneo ambalo nitawashauri
wateja wangu watembelee, ni kitu ambacho watu wanatakiwa kukifahamu, kugundua
siri ya uzuri wa hifadhi ya Taifa ya Gombe”
Kwa upande wake Meneja wa
Mawasiliano wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania, Paschal Shelutete ambaye
alikuwa kiongozi wa msafara huo akishirikiana na Meneja Mawasiliano TTB,
Geofrey Tengeneza, Meneja Mawasiliano wa TFS, Glory Mziray na Afisa Mawasiliano
wa Wizara ya Maliasili, Hamza Temba alisema ujio wa wanahabari hao utaleta
chachu ya kuongezeka kwa watalii wengi kutoka Israel pamoja na kupanua soko la
utalii kwa hifadhi za mikoa ya magharibi mwa Tanzania ikiwemo hifadhi ya Gombe.
Mhifadhi
wa hifadhi ya Taifa ya Gombe, Elihuruma Wilson (kushoto) akitoa maelezo
mafupi kwa wanahabari kutoka nchini Israel kuhusu hifadhi hiyo kabla ya
kuanza ziara ya kutembelea vivutio vilivyopo. Alieleza kuwa hifadhi
hiyo ina vivutio vingi wakiwemo Sokwe zaidi 100, Nyani, Kima, maporomoko ya maji, ndege aina mbalimbali na fukwe nzuri za kuogelea za ziwa Tanganyika.
“Tumekuja na kundi hili la wanahabari
ambao wameamua kama mlivowasikia kwa dhati kabisa kwamba watakaporudi nyumbani
watatumia mitandao ya kijamii, radio mbalimbali, Televisheni lakini kubwa zaidi
magazeti, wataandaa makala na vipindi mbalimbali hivyo tunaamini kwa dhati
kabisa watakaporudi nyumbani na kuzifanyia kazi taarifa zote walizozipata
katika hifadhi ya Taifa ya Gombe ama kwa hakika tutashuhudia ongezeko kubwa la
watalii kutoka nchini Israel katika siku chache zijazo,” Alisema Shelutete.
Aliongeza kuwa, “Ni wajibu
wa kila Mtanzania kuhakikisha rasilimali hizi za hifadhi zinazopatikana katika
hifadhi za taifa zinaendelea kutunzwa kwa ajili ya kizazi hiki na vizazi
vijavyo, watalii hawaji kuangalia ng’ombe kwenye hifadhi zetu, nasisitiza kuwa mifugo
haikubaliki kwenye hifadhi zetu”.
Msafara huo ulikuwa na
wanahabari kutoka vyombo maarufu nchini humo ikiwemo kituo cha Televisheni cha Channel
2, Jarida la Atmosphere, Jarida la National Geographic, Jaria la wiki la Yediot
Acharanot -7 Yamim na waandishi wawili wa mitandao ya kijamii. Wengine ni
maofisa wawili wa kampuni ya Utalii ya Safari ya nchini humo.
Hifadhi ya Taifa ya Gombe ilianzishwa
mwaka 1968 kwa ajili ya tafiti za kisayansi, hususani katika kuwalinda na
kuwahifadhi wanyamapori adimu wa jamii ya Sokwe Mtu (chimpanzees) ambao wapo
hatarini kutoweka. Hifadhi hii inaelezwa kuwa na Sokwe wasiopungua mia moja
ambao huishi kwa makundi na kuwa kivutio kikubwa na adimu katika hifadhi hiyo ambayo
ina ukubwa wa kilomita za mraba 52.
Msafara
wa Wanahabari wa Israel wakiwa kwenye boti tayari kwa safari ya
kuelekea hifadhi ya Taifa ya Gombe ambapo kutoka Kigoma mjini hadi
kwenye hifadhi hiyo ni mwendo wa saa moja na nusu hadi masaa mawili.
Meneja
Mawasiliano wa Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Paschal Shelutete
(kulia), Meneja Mahusiano wa Bodi ya Utalii Tanzania (Geofrey Tengeneza)
na Meneja Mawasiliano wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (Glory
Mziray) wakiongoza msafara wa wanahabari wa Israel kutembelea Hifadhi ya
Taifa ya Gombe.
Timu
ya wanahabari wa Israel wakianza safari ya kuingia ndani ya msitu wa
hifadhi ya Taifa ya Gombe kwa ajili ya kuona makundi mbalimbali ya
Sokwe. Lengo
kuu la ziara hiyo iliyoandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii
kupitia Bodi ya Utalii na TANAPA ni kutangaza vivutio vya utalii vya
Tanzania nchini Israel.
Wanahabari
kutoka Israel wakipata maelezo kutoka kwa mhifadhi wa hifadhi ya Taifa
ya Gombe kuhusu utarartibu wa kuzingatia wawapo ndani ya hifadhi hiyo
ikiwemo kutokupiga kelele na kuepuka matumizi ya mwanga wa kamera (Flash
Lights).
Mmoja
ya wanahabari wa Israel, Gerald Eddie wa Jarida la National Geographic
akiwa katika harakati za kupata taswira mwanana ya picha za Sokwe ndani
hifadhi ya Taifa ya Gombe.
Wanahabari wa Israel wakiwa ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Gombe.
Sokwe
akirukia matawi ya miti akiwa na mtoto wake ndani ya hifadhi ya Taifa
ya Gombe wakati wa ziara ya wanahabari wa Israel kwenye hifadhi hiyo.
Taswira mwanana ya Sokwe Mtu ndani ya hifadhi ya Taifa ya Gombe wakati wa ziara hiyo.
Mtoto
wa Sokwe akila matunda yanayopatikana katika hifadhi ya Taifa ya Gombe
wakati wa ziara ya wanahabari wa Israel katika hifadhi hiyo. Lengo kuu
la ziara hiyo iliyoandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia
Bodi ya Utalii na TANAPA ni kutangaza vivutio vilivyopo Tanzania nchini
Israel.
Sokwe
akiwa kapumzika kwenye maeneo yake ya kujidai ndani ya hifadhi ya Taifa
ya Gombe wakati wa zaira ya wanahabari wa Israel katika hifadhi hiyo.
Wanahabari hao walifurahia kuwaona sokwe hao wanaoelezewa na wanasayansi
kuwa wanakaribiana na binaadamu kwa takribani asilimia 80.
Meneja
Mawasiliano wa Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Paschal Shelutete
(wa pili kulia) akionesha kifaa maalum cha kupigia picha za angani
(drone) kilichorushwa na mmoja wa mwanahabari ambaye ni mpigapicha
kutoka Israel katika fukwe za Ziwa Tanganyika pembezoni mwa hifadhi ya
Taifa ya Gombe wakati wa zaiara ya wanahabari hao hifadhini hapo.
Kifaa
hicho maalum cha kupiga picha za angani kijulikancho kama 'drone'
kikiwa angani kupata taswira pana ya hifadhi ya Taifa ya Gombe.
Wanahabari
hao wakipiga picha za mwanahabari mwenzao na nyani wanaopatikana katika
hifadhi ya Taifa ya Gombe katika fukwe za Ziwa Tanganyika.
Mwanahabari
maarufu nchini Israel, Dana Spector, wa Jarida la Yediot Acharonot
(kushoto) akiigiliza mkao wa nyani katika hifadhi ya Taifa ya Gombe
wakati wa ziara hiyo. Matukio hayo yataonekana katika jarida hilo nchini
Israel kwa ajili kutangaza vivutio vya Tanzania. Anayepiga picha ni
Meneja Mawasiliano wa Shirika la Hifadhi za Taifa, Paschal Shelutete.
Mpiga picha wa Jarida la National Geographic la nchini Israel, Gerald
Eddie akipiga picha nyani wanaopatikana katika hifadhi ya Taifa ya
Gombe ambao pia ni kivutio cha utalii katika hifadhi hiyo kwa ajili ya
kuvitangaza katika jarida hilo.
Nyani
akiwa kambeba mtoto wake katika hifadhi ya Taifa ya Gombe tukio ambalo
pia sehemu ya vivutio vinavyopatikana katika hifadhi hiyo.
Wanahabari
hao hawakutaka kupitwa na tukio lolote katika ziara yao hiyo, hapo
wakipiga picha boti ambayo hufanya safari za kawaida kwa wananchi wa
vijiji vya mwambao wa ziwa Tanganyika na Manispaa ya Kigoma.
Mwanahabari
maarufu nchini Israel, Dana Spector, wa Jarida la Yediot Acharonot (wa
pili kushoto) na Mtangazaji maarufu wa Radio na Televisheni nchini
humo, Ran Sarig wakiigiliza mkao wa nyani dume na jike katika fukwe za
ziwa Tanganyika kwenye hifadhi ya Taifa ya Gombe.
Mwanahabari
maarufu nchini Israel, Dana Spector, wa Jarida la Yediot Acharonot (wa
pili kushoto) na Mtangazaji maarufu wa Radio na Televisheni nchini
humo, Ran Sarig wakifurahia matukio mbali mbali yaliyokuwa yakifanywa na
nyani wa hifadhi ya Taifa ya Gombe.
Wanahabari
hao pia walipata fursa ya kuogolea katika fukwe za kitalii za ziwa
Tanganyika pembezoni mwa Hifadhi hiyo ya Taifa ya Gombe, Fukwe hiyo ni
kivutio kikubwa cha utalii katika hifadhi ya Taifa ya Gombe.
Wanahabari
hao wakiwa wanaogelea katika fukwe za kuvutia za ziwa Tanganyika kwenye
hifadhi ya Taifa ya Gombe huku wakipiga picha za tukio hilo kwa ajili
kutangaza kivutio hicho nchini Israel.
Wanahabari
hao pia walipata fursa kutembelea jamii ya kijiji cha Mwamgongo ambacho
kinapakana na hifadhi ya Taifa ya Gombe, hapo wakimpiga picha mtoto
aliyekuwa na mpira wa makaratasi ambao ni sehemu ya utalii wa
kiutamaduni.
Mwandishi
wa habari kutoka Israel ambaye ni mpiga picha wa kituo cha Televisheni
cha Chanel 2, Roni Dahabari Kuban akiwapiga picha watoto katika kijiji
cha Mwamgongo jirani na hifadhi ya Taifa ya Gombe.
Mtangazaji
maarufu wa Radio na Televisheni nchini Israel, Ran Sarig akifungwa
shuka aliyoinunua na wananchi wa Kigoma katika ziara hiyo. Shuka hizo
zinazofumwa kwa mikono ni maarufu Mkoani Kigoma na sehemu ya utalii wa
Kiutamaduni unaopatikana katika Mkoa huo.
Mtangazaji
maarufu wa Radio na Televisheni nchini Israel, Ran Sarig akipiga picha
ya "Selfie" na baadhi ya watoto wa kijiji cha Mwamgongo kilichopo jirani
na hifadhi ya Taifa ya Gombe wakati wa ziara hiyo.
Wanahabari
hao walipotembelea kijiji cha Mwamgongo kilichopo jirani na hifadhi
hiyo ya Taifa ya Gombe walipata kujionea na kushiriki katika ngoma za
asili ambazo pia ni sehemu ya utalii wa kiutamaduni.
Mwanahabari
maarufu nchini Israel, Dana Spector, wa Jarida la Yediot Acharonot
akijaribu kuwasiliana na wanakikundi cha ngoma za asili wa kijiji cha
Mwamgongo kinachopakana na hifadhi ya Taifa ya Gombe na kushudia kazi
zao za mikono na ngoma ambazo ni sehemu ya utalii wa kiutamaduni.
Mwandishi
wa habari wa mitandao ya kijamii nchini Israel, Walfson Noa akifurahia
michezo na jamii ya watoto wa kijiji cha Mwamgongo wakati wa ziara hiyo.
Watalii
wa ndani nao pia walikuwemo kufurahia vivutio vya utalii
vinavyopatikana katika hifadhi hiyo na kutoa wito kwa watanzania wengi
zaidi kuvitembelea. Meneja wa Shirika la Hifadhi za Taifa, Paschal
Shelutete (wa pili kushoto waliosimama) akiongoza mahojiano na watalii
hao wa ndani.
Picha
ya pamoja ya wanahabari wa Israel, wahifadhi wa hifadhi ya Taifa ya
Gombe na waongoza msafara huo ambao ni Meneja Mawasiliano wa TANAPA,
Paschal Shelutete (wa pili kulia), Meneja Mahusiano wa TTB, Geofrey
Tengeneza (katikati waliosimama), Meneja Mawasiliano TFS, Glory Mziray
(wa tatu kulia) na Afisa Mawasiliano wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Hamza Temba (wa nne kulia).
Baada
ya kutembelea hifadhi ya Taifa ya Gombe msafara wa wanahabari hao
ulipanda boti kwa ajili ya safari ya kurudi Kigoma Mjini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni