MAKAMU MKUU wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. Rwekaza Mukandala amewataka vijana wanaohitimu kidato cha sita nchini wawe makini na wasikubali kusombwa na mawimbi ya dunia.
Ametoa wito huo jana (Jumamosi, Mei 14, 2017) wakati akizungumza na wahitimu 237 wa kidato cha sita wa shule ya sekondari ya St. Joseph Cathedral kwenye mahafali ya sita ya shule hiyo yaliyofanyika shuleni hapo, jijini Dar es Salaam.
Prof. Mukandala alisema: “Kwa hatua mliyofikia kila mmoja anapaswa atafakari kwa kina wito wake kimaisha. Kuweni makini, msisukumwe na mawimbi ya dunia na kujikuta mmepoteza ndoto zenu,” alisisitiza.
“Kuhitimu kidato cha sita si jambo dogo. Ni hatua ya kuwaongiza kujiandaa na utu uzima ikiwemo kujiunga na elimu ya vyuo vya juu na kuingia kwenye ndoa. Ni muda wa kutathmini yale uliyopitia na kutafakari maisha yako ya baadaye. Ni fursa ya kutoa shukrani kwa Mungu, kwa wazazi na walimu ambao walifanya kazi kwa umakini na kujitoa ili mfikie hatua nzuri mliyopo sasa,” alisema.
Alisema kuanzia sasa kila mmoja wao anapaswa kujiamini, kujituma zaidi na kujiona kuwa ana wajibu wa kujiletea maendeleo binafsi. “Mnapaswa kuepuka mwenendo wa kujiona mnyonge, au mtu asiyeweza kutimiza ndoto zake. Jenga tabia ya kuwa makini na maisha yako, jali mazingira yako na maendeleo yako,” alisisitiza.
Aliwataka wahakikishe wanakuchukua hatua mahsusi na kupata taarifa sahihi kuhusu taaluma wanazozitaka. Aliwataka wawe waadilifu na wenye heshima kwa watu wote lakini pia akawaasa juu ya maisha ya kutaka kupata fedha kwa haraka na kujilimbikizia mali.
“Epukeni rushwa na ufisadi. Mnatakiwa kujua kuwa utu, maendeleo na maisha bora havipatikani kwa fedha ingawa nayo ni muhimu katika maisha. Msitegemee kuishi kwa kuzingatia mambo makubwa yanayopimika kwa fedha,” alisema.
Akitoa mfano, Prof. Mukandala alisema: “Msikimbilie kuwa na magari mengi bila kujua nani atayatumia, au kujenga nyumba kubwa bila kujua nani atahitaji nafasi hiyo kubwa. Unanunua simu mbili au tatu bila kufikia athari zake kwa afya na mahusiano yako. Kabla hujachukua hatua ni lazima ujiulize, je unakihitaji kitu hicho? Kuweni makini na matumizi ya fedha badala kujilimbikiza vitu vya anasa,” alisema.
Aliwataka wazazi waendelee kuwalea vema vijana hao kwa sababu bado wanahitaji usimamizi wa wazazi kwa kila hatua wanayosonga mbele. “Tuendelee kuwaunga mkono watoto wetu kwa sababu jukumu letu kama wazazi bado liko palepale,” alisema.
Mapema, akimkaribisha mgeni rasmi kuzungumza na hadhira iliyokuwepo, Mkuu wa Shule ya St. Joseph Cathedral, Sista Theodora Faustine alisema St. wanafunzi waliohitimu jana ni 237 ambao kati yao wavulana ni 140 na wasichana ni 97 waliokuwa wakichukua michepuo ya ECA, EGM, CBG, HGE, HGL, PCM, PCB na PGM.
Alisema anaamini kwamba wahitimu wote watakuwa na sifa za kujiunga na vyuo vikuu mwaka huu kwa sababu shule hiyo imekuwa ni ya kwanza yenye wingi wa ufaulu kuliko shule yoyote mkoani Dar es Salaam. “Tumekuwa tukipata wanafunzi bora kitaifa mara kwa mara na mwaka jana tulipata wanafunzi bora kutoka michepuo ya PCB na ECA,” alisema.
Sista Theodora alisema wamekuwa wakifaulisha wanafunzi zaidi ya 250 kwa mwaka na kwa maana hiyo, wameweza kuandaa vijana 250 kuingia kwenye vyuo vikuu vya ndani na nje ya nchi. Akifafanua kuhusu malengo ya shule, Mkuu huyo wa shule alisema lengo lao ni kutoa elimu bora kwa watoto wa Kitanzania na kuwandaa kuwa wawajibikaji kwa Mungu na kwa Taifa lao.
Kwa upande wake, mwakilishi wa wazazi wenye watoto waliohitimu kwenye mahafali hayo, bw. Eric Shigongo alisema kila mhitimu anayo ndoto yake ambayo anapaswa kufanya kila awezalo kuhakikisha ndoto yake inatimia.
“Unao uwezo wa kuchagua (power of choice) kilicho chema kwa ajili ya maisha yako ya baadaye. Nasisitiza kwa sababu najua kila mmoja wenu ana ndoto yake ya kufika mahali fulani. Hakikisha unatimiza ndoto hiyo, haijalishi utapitia mazingira gani,” alisema.
Alisema kwake yeye anawaona vijana waliohitimu kwamba ni washindi (champions) na aliwaeleza hivyo wiki tatu kabla ya kuanza mitihani yao. Hata hivyo, aliwaasa kwamba wawe tayari kukosa mambo mengine kama kweli wanataka kufanikiwa maishani mwao.
“kama unataka kufanikiwa maishani, huna budi kujinyima mambo mengi ili uweze kupata kile unachokitaka. Najua mmemaliza kidato cha sita lakini safari yenu ya maisha ndiyo kwanza imeanza. Ninaamini wako watu hapa watakaotusaidia kutatua changamoto za nchi hii, wako madaktari hapa, wako wahandisi, wako wafanyabiashara na yuko Rais ajaye wa Tanzania, tena Rais mwanamke kutoka katika kundi hili,” alisema.
Katika mahafali hayo, mwanafunzi Kauthar Said aliibuka mwanafunzi bora na kupewa zawadi ya kompyuta mpakato (laptop) na wanafunzi wa mchepuo wa PCM, walipewa zawadi ya keki na Mkuu wa Shule kwa kuwa ni darasa ambalo halijawahi kuwa na kesi yoyote ya utovu wa nidhamu katika kipindi cha miaka miwili waliyoakaa shuleni hapo.
IMETOLEWA:
JUMAPILI, MEI 14, 2017.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni