Vigogo
watatu ambao ni wakurugenzi katika Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania
(Tanesco), makao makuu Dar es Salaam, wameshushwa vyeo huku mmoja
akiamua kuacha kazi mwenyewe.
Hatua
hiyo imekuja siku nne tangu Rais Dk. John Magufuli atengue uteuzi wa
aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Mhandisi Felchesmi
Mramba.
Mramba
alitenguliwa uteuzi wake siku chache baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa
Huduma za Nishati na Maji (Ewura), kutangaza kuridhia ombi la Tanesco la
kupandisha bei ya umeme kwa asilimia 8.5 kutoka 18 waliyoomba.
Wakurugenzi hao wamesimamishwa jana kupisha uchunguzi, huku chanzo cha kusimamishwa kwao kikiwa hakijaelezwa.
Taarifa
kutoka ndani ya Tanesco ambayo ilithibitishwa na Kaimu Mkurugenzi mpya
wa shirika hilo, Dk. Tito Mwinuka kwa simu jana, ilieleza kusimamishwa
kwa vigogo hao ambao walikuwa wasaidizi wa karibu wa Mramba katika
utendaji.
“Ni
kweli wamesimamishwa, lakini kwa kuwa sikuwa ofisini ngoja niisome
vizuri taarifa iliyopo mezani kisha niwatumie taarifa iliyokuwa sahihi
kuhusiana na hilo.
“Hapa
nilipo nipo ofisini na ofisa habari wangu (hakumtaja jina) tunaandaa
taarifa ya pamoja, kwa maana kila mmoja anapiga simu kutaka taarifa,
hivyo siwezi kuzitoa nusu nusu,’’ alisema Dk. Mwinuka.
Taarifa
zinaeleza kwamba wakurugenzi watatu wameshushwa vyeo na kuhamishiwa
katika Chuo cha Mafunzo cha Tanesco (TSS) kwa madai kuwa shirika
linaboresha ufanisi wake.
Walioshushwa
vyeo ni pamoja na Declan Mhaiki ambaye alikuwa Naibu Mkurugenzi
Mtendaji aliyekuwa anashughulikia usambazaji wa umeme.
Hata
uamuzi huo unachukuliwa inaelezwa kuwa Mhaiki alikuwa kwenye msiba wa
kaka yake mkoani Ruvuma, marehemu Kapteni Keenan Mhaiki.
Kapteni Mhaiki aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA), alifariki dunia mapema wiki hii.
Wengine
walioshushwa vyeo na kuhamishwa ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji Uzalishaji
na Huduma kwa Mteja, Mhandisi Sophia Mgonja na Naibu Mkurugenzi
Mtendaji Uzalishaji Umeme, Nazir Kachwamba.
Wakati
hao wakipigwa na panga hilo, Mkurugenzi wa Idara ya Rasilimali Watu,
Watson Mwakyusa, aliamua kuandika barua kuacha kazi mwenyewe.
Januari
Mosi mwaka huu, Rais Magufuli alimteua Dk. Mwinuka kuwa Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, baada ya kumng’oa aliyekuwa mkurugenzi
wa shirika hilo, Mhandisi Mramba.
Kabla ya uteuzi huo, Dk. Mwinuka alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Akiwa
mjini Bukoba kwenye ibada ya Mwaka Mpya, Rais Magufuli alisema amekerwa
na kusikitishwa na vitendo vya baadhi ya watumishi wa umma kujitokeza
hadharani na kutangaza au kuzungumzia mambo ya kitaifa kama uamuzi wa
Serikali bila kushirikisha viongozi wao wa ngazi za juu.
Kutokana na hali hiyo, alisema watendaji hao ni miongoni mwa majipu yanayostahili kutumbuliwa.
Hatua ya kutumbuliwa kwa Mramba ilikuja siku moja baada ya Ewura kutangaza kuridhia ombi la Tanesco la kupandisha bei ya umeme.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni