Na Mwandishi wetu
WADAU mbalimbali wamempongeza Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa
kuwa muwazi kwa wananchi wake wakati wanapohitaji misaada mbalimbali
wakati wa majanga.
Wametoa kauli hiyo leo jijini Dar
es salaam wakati wa mahojiano na mwandishi wa habari hizi kueleza kauli
ya hivi karibuni ya Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe ambaye
amekaririwa akidai kuwa kauli za Rais mkoani Kagera ni za hatari.
Wamesema kuwa baadhi ya Watanzania
wamezoea kupewa ahadi ambazo kwa wakati mwingine ni vigumu kutekelezeka
na sasa watu kama Mbowe bado wako kwenye mtazamo huo.
Wameongeza kuwa Rais Magufuli
amekuwa siku zote mkweli, jambo ambalo baadhi ya watu wasiopenda ukweli
wanapotosha kauli zake kwa kutaka kuwachonganisha wananchi na Rais wao
ambaye amekusudia kuwaletea wananchi maendeleo.
Rais Magufuli akiwa Kagera hivi
karibuni alisisitizia msimamo ambao si mpya, umekuwa msimamo wake na wa
Serikali tangu yalipotokea maafa ya tetemeko la ardhi mkoani humo kwamba
Serikali itasaidia lakini haitaweza kumjengea nyumba kila mtu.
“Baadhi ya wanasiasa na viongozi
wamekuwa wakitoa kauli zenye kupotosha na kubeza hotuba ya Rais
Magufuli mkoani Kagera jambo ambalo sio zuri na sio ukomavu wa kiasa”
walisema.
Mhadhiri Mwandamizi Chuo Kikuu
cvha Dar es Salaam, Dkt Bashiru Ally amesema kuwa katika mfumo wa siasa
huru kuna kutofautiana mitazamo kati ya wananchi ,Serikali na viongozi
wa siasa lakini ni wazi kuwa Rais alisimama katika msimamo wa Serikali
yake na uwezo wa kutekeleza ahadi zake.
Alisema kuwa Rais Magufuli alikuwa
na maana nzuri ya kukabiliana na majanga nchini inategemea uwezo wa
nchi na mshikamano wa wananchi na huo ni ukweli ambao wengi hawakupenda
kuusikia.
Dkt. Bashiru Ally alisema kuwa kwa
janga la Kagera kulikuwepo mshikamano wa Serikali katika ngazi zote,
wananchi na wadau mbalimbali walishiriki kwa namna moja ama nyingine
kukabiliana na janga hilo.
“Wito wangu ni kuwataka wanasisa
kujifunza kutokana na majanga badala ya kutoa kauli tatanishi na zenye
kubomoa mshikamano wa wananchi, bali wanatakiwa kukosoa bila kubeza,
kupotosha kwa namna ni ya kungwana,” alisema Dkt Bashiru
Kwa upande wake Dkt. Benson Bana
kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amesema kuwa watu wanatafsiri vibaya
maneno ya Mhe. Rais aliyoyaongea Mkoani Kagera hivi juzi.
“Mheshimiwa ameongea ukweli kwa sababu ni sahihi kuwasaidia watu wengi kwa pamoja kuliko kumsaidia mtu mmoja mmoja,” alisema.
Aliongeza kuwa hakuna haja ya kuwa
na wasiwasi juu ya lugha za Mhe. Rais kwani lugha zake hazina
ubabaishaji ni za kweli na ziko moja kwa moja, hao wanaomuongelea vibaya
ni wale wenye lengo la upinzani tu na sio maendeleo ya Taifa.
Ameongeza kuwa kwa upande wake
pamoja na wananchi wenye mapenzi ya kweli wamemuelewa Mhe. Rais na ndio
maana walikuwa wakimpigia makofi wakati akiongea kule Kagera.
”Mimi nilikuwepo mkoani Kagera na
hotuba za mheshimiwa zote nilizisikiliza kwa makini ndio maana nasema
wanye nia mbaya na Rais ndio wanaoongea mabaya juu yake kwani mbona
alivyoongelea suala la kupunguza umeme hawakusema chochote?” alihoji
Dkt. Bana.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Chama
cha United Democratic Party (UDP) John cheyo amewataka Watanzania
kutotegemea serikali kwa kila kitu pindi wanapopatwa na majanga.
Alisema kuwa lengo la Mheshimiwa
Rais Magufuli ni kutaka Watanzania kujenga utamaduni wa kujitegemea
pindi wanapofikwa na majanga mbalimbali na ndio maana alitaka kujua
juhudi zao kabla ya kuomba msaada wa Serikali.
Profesa Haji Semboja alisema kuwa
kauli ya Rais ilikuwa ni kuwahimiza watu wa Kagera ambao anajua wana
uwezo wa mambo mengi ya kulima mazao mbalimbali kama vile mazao ya
chakula na biashara ikiwemo ndizi na kahawa ambayo yanaweza kuwapatia
chakula cha kutosha wananchi wa mkoa huo.
Naye Kaimu Mkuu wa Chuo cha
Diplomasia nchini Dkt. Bernad Achiula amesema kuwa baadhi ya wananchi
wamepokea hotuba ya Rais John Magufuli kwa mtazamo tofauti, lakini ni
dhahiri hakuna nchi yeyote duniani ambayo inahudumia kila mwananchi
katika majanga ya kiasili yanayotokea.
“Wajibu wa Serikali katika nchi
yeyote ni kujenga na kuboresha miundombinu mbalimbali iliyotokea
ikiwemo barabara, hospitali, shule, malazi ya muda kwa waadhirika,
madawa, miundombinu ya umeme, maji kwa waathirika hatua inayolenga
kuwapa pole waathirika hao.
Alisema kuwa hatua hizo zinalenga
kutoa huduma kwa wananchi wengi kuliko kutoa msaada kwa mtu mmoja mmoja.
Alisema wanaotaka kumlaumu Rais basi wangemlaumu kama angekuwa Serikali
yake haijatoa huduma hizo muhimu.
Alipoulizwa kuhusu kauli hizo za
Mbowe, Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO ambaye pia ndiye Msemaji
Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi alisema lugha ya Rais na Serikali
kwa ujumla kuhusu maafa ya Kagera na mengine yaliyotokea nchini
haijawahi kubadilika wala kutetereka.
“Rais na Serikali yake kwa ujumla
wamekuwa wazi katika hili na itaendelea kuwa wazi kwamba kama Taifa
hatuna raslimali za kumsaidia kila mwathirika wa tetemeko la Kagera kwa
kumfanyia kila kitu.
Serikali ilitibu majeruhi wote
bure, ilisaidia kifuta machozi kwa familia zote zilizopoteza ndugu zao,
ilisaidia waathirika kupata huduma za kibinadamu kama dawa, ushauri wa
kisaikolojia, vyakula na mavazi na maturubai kwa makazi ya muda na
inaendelea kujenga miundombinu kama shule, zahanati na barabara,”
alisema.
Dkt Abbas akasisitiza: “Mbowe
atafute tu ajenda nyingine. Nilikwenda Kagera na kukaa kwa wiki mbili
baada ya tetemeko kutokea ambapo nilibahatika kuzungumza na waathirika
mijini na vijijini; hakuna kati yao popote aliyekuwa anasema Serikali
itamjengea nyumba au kumsaidia kila kitu. Kwa hiyo ujumbe wa Rais
ulieleweka tangu mwanzo na hata sasa.”
Ameongeza kuwa Serikali imesaidia kaya maskini kwa kuwapatia sajuri na mabati kwa ajili ya ujenzi wa nyumba.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni