
Shirika 
 la Nyumba la Taifa (NHC) limeanza kubomoa jengo la iliyokuwa Klabu 
Bilicanas na ofisi za Free Media inayomiliki gazeti la Tanzania Daima 
zinazomilikiwa na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na 
Maendeleo (Chadema) Taifa, Freeman Mbowe, lililopo makutano ya barabara 
ya Mkwepu na Indira Gandhi lenye kitalu namba 725-726/24 na hati namba 
C. T No. 186018/15 and C. T No. 186018/10.
Ubomoaji
 huo ulioanza jana unafanyika wakati Mbowe ameingia katika mgogoro na 
NHC baada ya kampuni ya udalali ya Poster and General Traders kumtolea 
vyombo nje mwanzoni mwa Septemba, mwaka jana kwa kudaiwa Sh bilioni 1.2 
ambayo ni deni la pango ya miaka 20.
Mwanzoni
 mwa Septemba, mwaka jana NHC kwa kushirikiana na Kampuni ya Poster and 
General Traders, ilifika katika jengo hilo kwa maelekezo ya kutoa  
thamani mbalimbali zilizokuwa katika ofisi za jengo hilo na kumpa Mbowe 
siku 14  kulipa deni analodaiwa na kuweza kugomboa mali hizo.
Mpango
 huo ulisimamiwa na Meneja wa Ukusanyaji Madeni wa NHC, Japhet 
Mwanasenga na alisema Mbowe alikuwa na muda wa wiki mbili kwa wakati huo
 kulipa fedha hizo kabla ya vifaa vyake kupigwa mnada.
Mwanasenga
 alisema taratibu zote zilifuatwa kabla ya kumwondoa mteja huyo ikiwamo 
notisi na kwamba vifaa hivyo vitashikiliwa kwa muda huo na endapo 
akishindwa kulipa jengo hilo atapangishwa mtu mwingine.
Alisema
 shirika hilo linahitaji fedha kwa ajili ya ujenzi na uendelezaji wa 
majengo yake hivyo mteja anayedaiwa ajiandae kuondolewa wakati wowote 
huku baadhi ya watu wakilihusisha tukio la Mbowe kuondolewa katika ofisi
 hizo na masuala ya siasa.
Hata hivyo, Mwanasenga, alisema uamuzi wa kumwondoa katika ofisi hizo hauna uhusiano na masuala ya siasa.
Kutokana
 na hali hiyo, Mbowe kupitia Mawakili wake, John Malya na Peter 
Kibatala, walifungua shauri la kupinga kuondolewa katika jengo hilo 
Mahakama Kuu ya Tanzania na kutaka kurudishwa katika jengo hilo.
Hata
 hivyo, maombi hayo yalitupiliwa mbali Oktoba 17, mwaka jana na Jaji 
Sivangilwa Mwangesi na kusema kuwa mahakama hiyo imechukua uamuzi huo 
baada ya kujiridhisha na hoja kuu tatu kuwa hakuna mkataba wa ubia 
uliopo baina ya NHC na Mbowe Hotels Limited na kuwa uhusiano pekee 
uliosalia ni wa mpangaji na mpangishaji.
Pia
 Jaji Mwangesi alisema mahakama imejiridhisha kuwa NHC imefuata taratibu
 zote katika kuiondoa Mbowe Hotels Limited kwa kutoa ilani ya siku 30 na
 baadaye siku 14 kabla ya kumtoa mteja wao huyo.
Kuhusu
 kusajiliwa au kutosajiliwa kama dalali rasmi wa mahakama wa kuendesha 
mchakato wa kumhamisha Mbowe katika jengo hilo, alisema hiyo nayo 
haikuwa hoja yenye mashiko na kwamba waombaji walitakiwa kuwasiliana na 
Msajili wa Mabaraza ya Ardhi.
Katika
 shauri hilo, NHC iliongozwa na Wakili Kiongozi, Aloyce Sekule na 
Ipilinga Panya na mawakili wake wengine waliojikita katika kujibu hoja 
zilizokuwa zikitolewa na wateja wao.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni