Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akisalimiana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla
wakati alipowasili kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja kuzindua Maadhisho ya
Wiki ya Mazingira, Mei 31, 2018. Wapili kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa
Pwani, Mhandisi Evarest Ndikilo.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akisalimiana na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Dar es salaam, Kate Kamba
wakati alipowasili kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam
kuzindua Wiki ya Mazingira, Mei 31, 2018. Wapili kushoto ni Waziri wa
Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla na watatu kushoto ni Mkuu
wa Mkoa wa Pwani , Mhandisi Evarest Ndikilo.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Space
Engineering Limited, Bw. Philip Mtui kuhusu mkaa uliotengenezwa kutokana
na takataka na kufungashwa kwenye kiroba tayari kwa kuuzwa wakati
alipotembelea banda la Kampuni hiyo kabla ya kuzindua Wiki ya Mazingira
kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam, Mei 31, 2018.
katikati ni Mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi, Evarest Ndikilo.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Space
Engineering Limited, Bw. Philip Mtui kuhusu mkaa uliotengenezwa kutoka
na takataka na kufungashwa kwenye kiroba tayari kwa kuuzwa wakati
alipotembelea banda la Kampuni hiyo kabla ya kuzindua Wiki ya Mazingira
kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam, Mei 31, 2018. Kulia
kwake ni Mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi, Evarest Ndikilo na kushoto ni
Meneja Mauzo wa kampuni hiyo, Neema Matemba.
Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa
akipata Maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Edosama
Hardware Limited, Edward Maduhu kuhusu bidhaa mbalimbali zinazotokana na
miti ambazo zinatengenezwa na kampuni hiyo wakati alipotembelea mabada
ya maonyesho kabla ya kuzindua Wiki ya Mazingira kwenye Viwanja vya
Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam Mei 31, 2018. Kulia ni Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba na
kushoto ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Dar es salaam, Kate Kamba.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akipata Maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Edosama
Hardware Limited, Edward Maduhu kuhusu bidhaa mbalimbali zinazotokana na
miti ambazo zinatengenezwa na kampuni hiyo wakati alipotembelea mabada
ya maonyesho kabla ya kuzindua Wiki ya Mazingira kwenye Viwanja vya
Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam Mei 31, 2018. Kulia ni Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akimsikiliza Bibi Nimwagile Mwaijumba wakati alipotembelea banda la
Kituo cha Utengenezaji magari cha Nyumbu na kujionea mashine ya
kutengeneza mkaa bora kwa kutumia takataka iliyobuniwa na kutengenezwa
na kituo hicho. Waziri Mkuu alitembelea mabanda ya maonyesho kabla ya
kuzindua Wiki ya Mazingira kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es
salaam, Mei 31, 2018. Watatu kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa
Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba na wapili kulia ni Mkuu wa
Mkoa wa Opwani Mhandisi, Evarest Ndikilo.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akimsikiliza Mkurugenzi wa Kampuni ya JHS , David Mwendapole wakati
alipotoa maelezo kuhusu majiko makubwa yanayotumia gesi kidogo katika
maonyesho ya Wiki ya Mazingira kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar
es salaam, Mei 31, 2018. Wanne kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akizungumza wakati alipozindua Wiki ya Mazingira kwenye Viwanja vya
Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam Mei 31, 2018.
Baadhi ya wananchi waliohudhuria
katika maadhimisho ya wiki ya Mazingira wakimsikiliza Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa wakati alipowahutubia kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja
jijini Dar es salaam, Mei 31, 2018.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akiagana na viongozi baada ya kuzindua Wiki ya Mazingira kwenye Viwanja
vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam, Mei 30, 2018. Kutoka kushoto ni
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarest Ndikilo, Waziri wa Maliasili na
Utalii, Dkt. Hamis Kigwangala, Mwenyekiti wa CC wa Mkoa wa Dar es alaam,
Kate Kamba,Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kisare Matiku Makori na kulia ni
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January
Makamba. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
………………
*Aagiza viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam wabadilike
*Ataka wasimamie wananchi waachane na matumizi ya mkaa
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
ameziagiza Wizara, mashirika na taasisi zote za Serikali na binafsi
zianze kutumia nishati mbadala ili kuondoa kabisa matumizi ya kuni na
mkaa.
“Wizara, taasisi na mashirika yote
ya Serikali na binafsi pamoja na vikundi vya uzalishaji wanaotumia
nishati ya kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia au shughuli za uzalishaji
waanze kutumia nishati mbadala ili matumizi ya mkaa yaishe na
ikiwezekana yatoweke kabisa,” amesema.
Ametoa agizo hilo leo
(Alhamisi, Mei 31, 2018) wakati akizungumza na mamia ya wananchi na
viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam walioshiriki uzinduzi wa maadhimisho
ya Siku ya Mazingira Duniani kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar
es Salaam. Kaulimbiu ya mwaka huu ni: “Mkaa ni Gharama: Tumia Nishati
Mbadala.”
Waziri Mkuu amesema teknolojia
bora ya uzalishaji wa mkaa mbadala ambayo ameiona kwenye maonesho hayo,
ikuzwe na kusambazwa kote nchini ili kuwawezesha wananchi walio wengi
waachane na matumizi ya mkaa wa kawaida na badala yake watumie
mkaa-mbadala kwa lengo la kuhifadhi misitu na kupunguza uharibifu wa
mazingira.
Ili kufanikisha matumizi ya
teknolojia hiyo, Waziri Mkuu amesema vibali vya ujenzi wa majengo
makubwa na taasisi kama shule, vyuo, hospitali navyo pia vianze
kuzingatia ufungaji wa mifumo ya nishati ya gesi kwa ajili ya matumizi
ya kupikia ili kurahisisha upatikanaji na matumizi ya nishati mbadala
katika taasisi na majengo makubwa.
“Wahandisi na wachoraji ramani za
majengo waweke njia za kupitisha kwenye michoro yao ili ujenzi wa nyumba
na majengo haya ukikamilika, watumiaji waweze kutumia teknolojia hiyo,”
amesema.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema
Mkoa wa Dar es Salaam ni lazima ubadilike na uachane na matumizi ya
mkaa. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, mkoa huo unatumia tani 500,000 za
mkaa kwa mwaka.
“Viongozi wa mkoa na wilaya
ondokeni hapa na hili kama ajenda ya mkoa wa Dar es Salaam, mkaifanyie
kazi na Wizara pia ifuatilie mmetekeleza kwa kiasi gani. Jitihada
zilizofanywa na Jiji la Dar es Salaam kupitia kwa Mstahiki Meya, za
kuanza kuwapa mtaji wajasiriamali hawa wanaotengeneza teknolojia mpya ni
lazima ziigwe na nyie kwenye Manispaa zenu.”
“Meya ametoa fursa na
amewaanzishia, na ninyi sasa endeleeni. Tengenezeni bajeti kupitia
Mabaraza ya Madiwani na muwaunge mkono wajasiriamali wanaotengeneza haya
majiko kwa kuwapa teknolojia hii kwenye maeneo yenu. Wanaotengeneza
mashine za mkaa mbadala, wawezeshwe watengeneze mashine nyingi zaidi na
zije kila Manispaa, ili kila Manispaa ianze kutumia teknonolojia hiyo
kupikia,” alisisitiza.
Amewaagiza Wakuu wa Wilaya na
Wakurugenzi wa Manispaa za Jiji la Dar es Salaam wafuatilie kwa karibu
usambazaji wa teknolojia hiyo.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi
Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Yusuf Makamba
amesema hali ya mazingira hapa nchini ni mbaya licha ya kuwa haionekani
kwa haraka na watu waishio mijini.
“Hali ya mazingira nchini mwetu ni
mbaya sana na inawezekana watu wanaoishi Dar es Salaam hawaioni kwa
haraka kwa sababu mahitaji yao yote wanayapata sokoni na madukani,”
alisema.
“Wenzetu wa mikoani na vijijii
wanaotegemea mvua na udongo wenye rutuba wanataabika kwa sababu kipato
chao kinaathirika kutokana na uharibifu wa mazingira,” alisema.
Alisema mazingira yanafungamana na
utalii, kilimo, ufugaji, nishati, maji na kwamba maendeleo ya nchi pia
yamefungamana moja kwa moja na mazingira. “Asilimia 90 ya Watanzania
wanatumia kuni na mkaa kupikia lakini asilimia 70 ya mkaa wote
unaozalishwa nchini Tanzania, unatumika jijini Dar es Salaam,” alisema.
Waziri Makamba alisema taasisi za
Serikali kama vyuo, magereza, hospitali na shule zinaongoza kwa matumizi
ya kuni na mkaa na hivyo kuchangia uharibifu mkubwa wa mazingira.
Akitoa mfano, alisema Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kina wanafunzi wapatao 30,000 na kinalazimika kuandaa milo mitatu kila siku.
“Chuo hiki kina migahawa tisa,
kule nyuma kumejaa magogo ya kuni. Kuna mgahawa mmoja mdogo unatumia
magunia 17 ya mkaa kwa siku, sasa huo mkubwa unatumia magunia mangapi?”
alihoji.
Maadhimisho hayo yaliyozinduliwa
leo, yataendelea hadi Juni 5, mwaka huu ambayo ni siku ya kilele. Pia
wiki nzima kutakuwa na makongamano, midahalo na mjadala wa kitaifa.