WIZARA YA MALIASILI NA UTALII INAVYOIMARISHA SEKTA YA UHIFADHI NA UTALII NCHINI


Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiwaongoza Maafisa wa Wanyamapori 87 wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania– TAWA, Shirika la Hifadhi za Taifa – TANAPA na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro kupiga gwaride la ukakamavu muda mfupi baada ya kuwatunuku vyeti vya kuhitimu mafunzo ya Jeshi Usu hivi karibuni katika kituo cha Mlele mkoani Katavi.

........................................................
Wakati huu tunapoadhimisha miaka 54 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ni takriban miaka miwili sasa na miezi kadhaa tangu Serikali ya awamu ya tano, inayoongozwa na Mhe. Rais, Dk. John Pombe Joseph Magufuli iingie madarakani.

Itakumbukwa kuwa katika hotuba yake ya kwanza ya kulihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa mjini Dodoma, Mhe. Rais Magufuli alitoa vipaombele kadhaa vya kutekelezwa na wizara zake huku Wizara ya Maliasili na Utalii akiipa vipaombele vikuu vitatu ambavyo ni kukabiliana na ujangili, kutatua migogoro ya mipaka kwenye maeneo ya hifadhi na kuongeza ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Wizara ya Maliasili imeendelea kutekeleza vipaombele hivyo pamoja na jukumu lake la msingi la kuhifadhi na kusimamia matumizi endelevu ya rasilimali za maliasili na malikale, na kuendeleza Utalii kwa faida ya kizazi cha sasa na kizazi kijacho.

Ujangili

Wizara imefanikiwa kuanzisha mikakati mbalimbali ya kukabiliana na ujangili na biashara haramu ya wanyamapori ambayo imeanza kuzaa matunda.

Mikakati hiyo ni pamoja na kuanzishwa kwa Kikosi Kazi Maalum cha Kudhibiti Uhalifu wa Misitu na Wanyamapori nchini ambacho kilianzishwa mwezi Julai, 2016 sambamba na kuimarishwa kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) ambayo ilianza majukumu yake rasmi tarehe 1 Julai, 2016.

Mikakati mingine ni mabadiliko ya mfumo wa utendaji kutoka ule wa kiraia kwenda wa Jeshi Usu, matumizi ya teknolojia ya ndege zisizokuwa na rubani (drones) kwa ajili ya doria, ushirikishwaji wa wananchi kwenye uhifadhi na matumizi ya mbwa maalum wa kunusa ili kutambua nyara katika viwanja vya ndege na bandari.

Kupitia mikakati hiyo, mwaka 2016/2017 Wizara kupitia taasisi zake iliendesha doria mbalimbali ndani na nje ya maeneo yaliyohifadhiwa na kufanikiwa kukamata watuhumiwa 7,085 kwa makosa mbalimbali. Aidha, meno ya tembo 129 na vipande 95 vyenye uzito wa jumla ya kilo 810.03 vilikamatwa.

Vielelezo kadhaa pia vilikamatwa ikiwemo silaha za kivita 48, silaha za kiraia 150, risasi 1,058, magobore 406, silaha za jadi 22,307 na roda 120,538.

Jumla ya kesi 2,097 zilifunguliwa katika mahakama mbalimbali na kesi 802 zilimalizika. Watuhumiwa 472 katika kesi 262 walifungwa jela jumla ya miezi 42,153 na watuhumiwa 79 katika kesi 43 waliachiwa huru huku watuhumiwa wengine 469 katika kesi 276 wakilipa faini ya jumla ya shilingi  milioni 452.1.

Katika kuelekea kwenye Mfumo wa Jeshi Usu, Wizara imeendesha mafunzo kwa watumishi 661 kuhusu ukakamavu, uongozi na ukusanyaji wa taarifa za kiintelijensia kuhusu Ujangili. Watumishi walioshiriki mafunzo hayo ni 139 kutoka TAWA, 388 kutoka TANAPA, 117 kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro na 17 kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania. 

Kutokana na jitihada hizi hali ya ujangili imepungua kwa kiasi kikubwa. Kwa mfano, katika Pori la Akiba Selous idadi ya Tembo waliouwawa imepungua kutoka tembo 17 mwaka 2015/16 hadi tembo 7 mwaka 2016/17.

Hata hivyo, katika siku za hivi karibuni, wanyamapori hasa tembo wameanza kuonekana katika maeneo mbalimbali ambayo kwa kipindi kirefu hawakuwa wakionekana, mfano hivi karibuni tembo kadhaa walionekana katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Aprili 18 mwaka huu, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na Balozi wa Uingereza hapa nchini, Sarah Cooke ofisini kwake mjini Dodoma, alinukuliwa akisema kuwa ujangili hapa nchini umepungua kwa zaidi ya asilimia 50.

Alisema katika kipindi cha miezi sita iliyopita hadi kufikia mwezi huu wa Aprili hakuna mauaji mapya ya wanyamapori yaliyoripotiwa kuhusiana na ujangili na kwamba nyara zinazokamatwa hivi sasa ni masalia ya zamani ambayo yanatafutiwa masoko. 

Alisema mafanikio hayo yametokana na juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama sambamba na kuwashirikisha wananchi kwa kuimarisha ulinzi na doria za mara kwa mara za kiitelijensia katika maeneo ya hifadhi.

Utalii

Katika kuongeza idadi ya watalii nchini, Wizara imeendelea kutekeleza shughuli mbali mbali ikiwa ni pamoja na kuimarisha ulinzi kwenye maeneo ya hifadhi, kuboresha miundo mbinu kwenye maeneo ya vivutio, kuanzisha huduma mpya za utalii pamoja na utangazaji.

Juhudi hizo zimewezesha ongezeko la watalii wa kimataifa kutoka 1,284,279 mwaka 2016 hadi kufikia 1,327,143 mwaka 2017 sawa na ongezeko la asilimia 3.2.

Aidha, mapato yanayotokana na utalii yameongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 2.1 mwaka 2016 hadi Dola za Marekani bilioni 2.2 mwaka 2017.

Sekta hii ya utalii imetoa ajira takriban 500,000 za moja kwa moja na ajira nyingine milioni moja zisizo za moja kwa moja kwa mwaka.

Sekta hii pia inachangia takriban asilimia 17.5 ya Pato la Taifa na wastani wa asilimia 25 ya fedha zote za kigeni.

Aidha, Wizara imedhamiria kupanua wigo wa vivutio vya utalii nchini kwa kufungua utalii wa Kanda ya Kusini ili kuongeza idadi ya watalii na mapato ya Serikali. 

Kupitia dhamira hiyo Serikali imesaini mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia wa Dola za Marekani milioni 150, sawa na takriban shilingi bilioni 340 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa Kusimamia Maliasili na Kuendeleza Utalii wa Ukanda wa Kusini –REGROW.

Mradi huu ambao maandalizi yake yalianza mwezi Novemba 2014 ulizinduliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan tarehe 12 Februari, 2018 katika viwanja vya Kihesa Kilolo Mjini Iringa huku Kauli Mbiu yake ikiwa “Utalii kwa Maendeleo Endelevu- Karibu Kusini”.

Mama Samia alisema lengo la mradi huo ni kuongeza mchango wa sekta ya maliasili na utalii katika uchumi wa taifa kwa kuboresha vivutio vya utalii, miundombinu, usimamizi wa vivutio na kuongeza faida za kiuchumi kwa jamii zinazoishi jirani na maeneo ya hifadhi katika ukanda huo wa kusini.

Katika kuongeza jitihada za kutangaza utalii ndani na nje ya nchi, Wizara imeendelea kuongeza bajeti ya utangazaji ambapo Bodi ya Utalii Tanzania kwa mwaka wa fedha 2017/18 imeongezewa bajeti kufikia shilingi bilioni 6.6 ikilinganishwa na shilingi bilioni 4.1 mwaka 2016/2017 na bilioni 4.3 mwaka 2015/16.

Aidha, katika kufungua masoko mapya ya utalii nje ya nchi, Wizara inaangazia masoko mapya katika nchi za China, Israel, Urusi, Australia na nchi nyingine za Skandinavia.

Wananchi wanavyonufaika na uhifadhi 

Wizara ya Maliasili inaendelea na juhudi za kuhakikisha wananchi wanaoishi jirani na maeneo ya hifadhi wananufaika na rasilimali zilizopo. Kupitia Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori, jamii zinanufaika kwa kupata ajira, kitoweo, elimu, miradi ya kijamii na kuongeza kipato.

Hadi hivi sasa jumla ya Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori 38 zimeanzishwa. Aidha, wananchi wanaoishi jirani na misitu wananufaika kupitia miradi ya ufugaji nyuki ambapo kupitia uwezeshaji wa Mfuko wa Misitu Tanzania miradi 254 ya kuboresha kipato cha jamii zinazoishi pembezoni mwa misitu imetekelezwa.

Miradi hiyo ni ya ufugaji nyuki ambapo vikundi vya ufugaji nyuki 399 na watu binafsi 27 wamewezeshwa kupata mizinga ipatayo 11,730.

Udhibiti wa migogoro baina ya wananchi na hifadhi

Katika kudhibiti migogoro ya mipaka kati ya wananchi na maeneo jirani na hifadhi, Wizara kwa kushirikiana na Taasisi za Serikali na Wadau imeendelea kuhakiki mipaka yote ya maeneo ya hifadhi na kuweka alama za kudumu na mabango ya tahadhari.

Hadi kufikia mwezi Mei, 2017 vigingi 14,755 vimesimikwa sawa na asilimia 62.4 ya vigingi 23,638 vinavyohitajika katika Hifadhi za Misitu, Mapori ya Akiba, Hifadhi za Taifa na Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro.

Aidha, kupitia program ya Panda Miti Kibiashara, Wizara imewezesha vijiji 48 kuandaa Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi katika Wilaya za Ludewa, Madaba, Makete, Mufindi, Njombe Mjini, Njombe Vijijini, Kilolo na Nyasa.

Mikakati mipya chini ya Waziri wa Maliasili, Dk. Hamisi Kigwangalla

Aidha chini ya Uongozi Mpya wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla ipo baadhi ya mikakati yake mipya inayolenga kutoa uelekeo mpya wa kuimarisha sekta Maliasili na Utalii nchini.

Dk. Kigwangalla anaeleza mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kuanzisha kwa mwezi maalum wa Urithi wa Mtanzania (Tanzania Heritage Month) ambao utaadhimishwa mwezi Septemba kila mwaka, kuanzishwa kwa Makumbusho ya Marais Wastaafu waliotawala Tanzania mjini Dodoma na Kuboresha na kuendeleza utalii wa fukwe kwa kuanzisha Mamlaka ya Fukwe.

Mikakati mingine ni pamoja na kujenga makumbusho ya meno ya tembo katika miji ya Dar es Salaam, Dodoma, Arusha na Iringa pamoja na kutambua barabara iliyokuwa ikitumika katika biashara ya utumwa wakati wa ukoloni ili iweze kutumika kiutalii.

Akizungumzia migogoro ya mipaka iliyopo baina ya wananchi na maeneo ya hifadhi, Dk. Kigwangalla amesema Serikali itatatua migogoro hiyo kwa kushirikisha wananchi sambamba na kuwasaidia kutatua changamoto za msingi ambazo ni kuimarisha maeneo ya malisho ya mifugo, upatikanaji wa maji kwa ajili ya wananchi na mifugo, mpango bora wa matumizi ya ardhi na uendelezaji wa kilimo na ufugaji.

Kwa upande wa vitalu vya uwindaji wa kitalii, Dk. Kigwangalla amesema Serikali itafanya mabadiliko katika mfumo wa ugawaji vitalu vya uwindaji wa kitalii kutoka mfumo unaotumika hivi sasa wa Kamati “Administrative Allocation” na kutumia mfumo wa mnada “Auction”.

Lengo ikiwa ni kuongeza uwazi na kuruhusu nguvu ya soko kuamua bei ambapo mapato ya Serikali nayo yatatarajiwa kuongezeka maradufu. Ili kutekeleza hilo, sheria na kanuni zinafanyiwa marekebisho.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni