Kamati za mashindano Handeni Kwetu Cup zaaswa kutimiza wajibu wao


VIONGOZI wa mpira wa miguu katika kata mbalimbali wilayani Handeni, mkoani Tanga, wameaswa kuhakikisha kwamba wanatimiza wajibu wao wa kuratibu na kuyasimamia mashindano ya Ligi ya Handeni Kwetu Cup kwenye Kata zao ili mashindano hayo yawe na tija na kupatikana washindi kwa wakati kama ilivyokusudiwa.

Ushauri huo umetolewa na muasisi wa mashindano hayo, Kambi Mbwana, alipokuwa akizungumza na gazeti hili wilayani hapa, akisema kuwa kuna baadhi ya Kata zimekuwa zikisua sua kutokana na viongozi waliochaguliwa kutojua umuhimu wa uwajibikaji na kutimiza wajibu kwa maslahi mapana ya mpira wa miguu kwa kupitia mashindano hayo yanayodhaminiwa na bahati nasibu ya Biko 'ijue nguvu ya buku' na Mfuko wa hifadhi ya jamii (NSSF).

Akizungumzia suala hilo, Mbwana alisema kabla ya kuanza mashindano hayo, Chama cha Mpira wa miguu wilayani Handeni mkoani Tanga (HDFA), kilichagua viongozi wake kila kata ili pamoja na kuyaratibu mashindano ya Handeni Kwetu kwenye Kata zao kwa ajili ya kutafuta washindi wawili wa kwenda ngazi ya tarafa, pia viongozi hao wangekuwa na majukumu ya kusimamia na kuendeza mpira kwenye kata zao, viongozi ambao upatikanaji wao ulilazimika kutumika kwa gharama ya muda na fedha.

"Kila mdau wa michezo anapaswa kujua kwenye kata yake kuna viongozi wa mpira waliochaguliwa ili kusimamia ligi hii, hivyo wanapaswa kutimiza wajibu wao ili mashindano yetu yaende vizuri kwa ajili ya kutoka kwenye kata na kuingia kwenye tarafa na baadae ngazi ya wilaya kama matarajio yetu.

" Kumekuwa na ucheleweshaji mkubwa kwa mashindano yetu kwa baadhi ya kata zetu jambo linaloweza kuathiri mfumo mzima wa ligi yetu tuliyoamua kuanzisha kwa minajiri ya kuendeleza vipaji vya vijana wetu katika wilaya ya Handeni, hivyo nawaomba sana viongozi hawa watimize wajibu wao,"Alisema.

Kwa mujibu wa Mbwana, baadhi ya kata ambazo zimechelewa kuanza mashindano hayo ni pamoja na Segera, Sindeni, Kwachaga, Kwamsisi, Kiva, Kwaluguru, Kitumbi, Komkonga na Kwedizinga, wakati kata nyingine zilizosalia zikiwemo za Halmashauri ya Handeni mjini zenyewe zikiwa zinaelekea mwishoni, wakati zipo zile zilizomaliza kupata washindi wa kuelekea kwenye ngazi ya tarafa itakayoanza baada ya kumalizika katika hatua ya kata.

Mashindano ya Handeni Kwetu Cup yalizinduliwa mwezi Machi mwaka huu katika uwanja wa Mabatini, Mkata na kuhudhuliwa na watu mbalimbali kwa hisani ya Biko na NSSF huku waratibu wa mashindano hayo yatakayomalizika mwezi Novemba mwaka huu wakifungua milango kwa wadhamini wengine ili kuwezesha ligi hiyo ya aina yake ifanyike kwa mafanikio makubwa.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni