Na Veronica Kazimoto,Zanzibar
Wastani
wa ukusanyaji wa mapato katika kipindi cha miezi 10 ya Mwaka wa Fedha
2017/18 katika Jumuiya ya Afrika Mashariki umeongezeka hadi kufikia
asilimia 16 ukilinganisha na asilimia 14 katika kipindi kama hicho cha
2016/17.
Hayo
yamesemwa na Kamishina Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw.
Charles Kichere baada ya kumaliza Kikao cha 44 cha Makamishna Wakuu wa
Mamlaka za Mapato za Jumuiya hiyo kilichofanyika tarehe 29 hadi 30 Mei,
2018 katika Ukumbi wa Benki Kuu, Zanzibar ambacho TRA ilikuwa mwenyeji.
"Katika
kikao hiki tulichomaliza leo, tumejadili mambo mbalimbali ikiwa ni
pamoja na mafanikio tuliyoyapata ambayo ni kuongezeka kwa ukusanyaji wa
mapato katika Jumuiya yetu kutoka asilimia 14 kwa Mwaka wa Fedha wa
2016/17 hadi kufikia asilimia16 katika kipindi kama hicho cha Mwaka huu
wa Fedha wa 2017/18", alisema Kichere.
Kichere
alieleza kuwa, pamoja na mafanikio hayo, kikao hicho kimejadili na
kukubaliana masuala mbalimbali yakiwemo kuimarisha utozaji kodi kwa watu
binafsi na wafanyabiashara wadogo na kuweka mipango mahususi ya kutoza
kodi stahiki kutoka kwa wafanyabiashara hao.
"Pia,
tumekubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano katika Mamlaka za Mapato
za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ajili ya kupeana taarifa na
kuonyeshana mianya ya ukwepaji kodi ili kudhibiti na kukomesha hali
hiyo," alibainisha Kichere.
Makubaliano
mengine ni pamoja na kuweka mikakati mahususi ya kushughulikia masuala
ya uadilifu kwa kuwa, Mamlaka za Mapato za Afrika Mashariki kama ilivyo
kwenye taasisi nyingine za Serikali ndani ya Jumuiya, kumekuwa na
changamoto hiyo ya uadilifu. Hivyo, Makamishna Wakuu hao wamekubaliana
kuongeza ufanisi katika kukagua mwenendo wa maisha wa watumishi wa
Mamlaka zao ikiwa ni pamoja na kuwashitaki wale wote ambao si waadilifu
kama sehemu ya kupambana na rushwa.
"Ndugu
waandishi wa habari, pamoja na kupambana na rushwa, tumekubaliana pia
kupunguza gharama za mifumo ya TEHAMA kwa kuwajengea uwezo watumishi wa
ndani ya Mamlaka ili kupunguza gharama ambazo zinatumika kuwalipa
watalaam kutoka katika mataifa mengine," aliongeza Kichere.
Kwa
upande wa Makamishna Wakuu wa Jumuia hiyo ya Afrika Mashariki,
wakizungumza kila mmoja kwa wakati wake, wote wamekubali kuzingatia
makubaliano hayo kwa ajili ya kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa
mapato ndani ya nchi zao.
Kabla
ya mkutano huo, Makamishna Wakuu hao wa taasisi za kodi katika Jumuiya
ya Afrika Mashariki walikutana na Wawakilishi wa Shirika la Misaada la
nchini Japan (JICA) kutathmin miradi wanayofadhili kwa lengo la
uboreshaji shughuli za forodha ndani ya Jumuiya.
Katika
mkutano huo, Shirika la JICA lilipongezwa kwa kurahisisha uondoshaji wa
mizigo na kuhudumia abiria wanaosafiri kupitia mipaka ya nchi za
Jumuiya hiyo kutoka saa 8 za awali hadi saa 2 na nusu kwa sasa hususani
katika Kituo cha Huduma za Pamoja cha Rusumo ambacho kilijengwa kwa
msaada wa JICA.
Kituo
hicho ni moja kati ya vituo 7 vya Huduma za Pamoja Mipakani
vilivyojengwa kwa ufadhili wa wadau mbalimbali wa Maendeleo. Sambamba na
pongezi hizo, Shirika hilo limeombwa kusaidia ufadhili wa uunganishaji
mifumo ya TEHAMA na uwezeshaji wa mawakala wa forodha ili kupata ufanisi
zaidi.
Kikao
cha 44 cha Makamishna Wakuu hao, kimehudhuliwa na watendaji wapato 80
kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB),
Mamlaka ya Mapato Kenya (KRA), Mamlaka ya Mapato Rwanda (RRA), Mamlaka
ya Mapato ya Uganda (URA) Mamlaka ya Mapato Burundi (OBR), Mamlaka ya
Mapato ya Jamhuri ya Sudani Kusini pamoja na Mwakilishi kutoka
Sekritariat ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kikao kijacho kinatarajia
kufanyika mwezi Novemba, 2018 nchini Kenya.
Kamishna
Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Charles Kichere (katikati)
akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza Kikao cha 44
cha Makamishna Wakuu wa Mamlaka za Mapato za Jumuiya ya Afrika Mashariki
kilichofanyika tarehe 29 hadi 30 Mei, 2018 katika Ukumbi wa Benki Kuu,
Zanzibar ambapo TRA ilikuwa mwenyeji. Kushoto ni Mhe. Audace Niyonzima
wa Mamlaka ya Mapato Burundi na kulia ni Bi. Doris Akol, Kamishna Mkuu
wa Mamlaka ya Mapato ya Uganda (URA).
Mwenyekiti
wa Kamati ya Watalaam wa Mamlaka za Mapato za Jumuiya ya Afrika
Mahariki Bi. Martine Nibasumba kutoka Mamlaka ya Mapato Burundi (OBR)
akiwasilisha ripoti ya kamati hiyo kwa Makamishna Wakuu (hawapo pichani)
wakati wa Kikao cha 44 cha Makamishna Wakuu wa Mamlaka za Mapato za
Jumuiya hiyo kilichofanyika tarehe 29 hadi 30 Mei, 2018 katika Ukumbi wa
Benki Kuu, Zanzibar ambapo TRA ilikuwa mwenyeji.
Kamishna
Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Charles Kichere (katikati)
akiwa katika picha ya pamoja na Makamishna Wakuu wenzake na baadhi ya
wajumbe wa Kikao cha 44 cha Makamishna Wakuu wa Mamlaka za Mapato za
Jumuiya ya Afrika Mashariki kilichofanyika tarehe 29 hadi 30 Mei, 2018
katika Ukumbi wa Benki Kuu, Zanzibar ambapo TRA ilikuwa mwenyeji.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni