Na: Mahmoud Ahmad, Dodoma.
Serikali imesema kuwa pamoja na
huduma za bidhaa ya fedha kuamuliwa na nguvu ya soko kwa upande wake
imekuwa ikichua hatua za kisera ili kuhakikisha kuwa riba za mikopo
zinapungua katika soko hapa nchini.
Hayo yameelezwa leo Bungeni Jijini
Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Ashatu Kijaji
alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Konde, Mhe. Khatibu Haji juu ya
Serikali inachukua hatua gani ili benki ziweze kupunguza viwango hivyo
vya riba?
“Baadhi ya hatua zilizochukuliwa
na Serikali kupitia Benki Kuu ni pamoja na kuzitaka benki za biashara
kutumia mfumo wa kuhifadhi na kutoa taarifa za wakopaji (Credit
Reference Bureau System). Aidha, Benki hiyo imekuwa ikitoa mikopo ya
muda mfupi kwa benki za biashara kwa kiwango cha asilimia 6.89,” amesema
Dkt. Kijaji.
Dkt. Kijaji amezitaja hatua
nyingine zilizochukuliwa kuwa ni Benki Kuu kushusha riba (Discount Rate)
kutoka asilimia 16.0 hadi asilimia 9.0 pamoja na kupunguza kiwango cha
chini cha amana kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu na benki za biashara
(Statutory Minimum Reserve Requirememnt (SMR)) kutoka asilimia 10.0 hadi
asilimia 8.0.
Vile vile Serikali imeendelea
kulipa malimbikizo ya madai yaliyohakikiwa kwa lengo la kupunguza
kiwango cha mikopo chechefu na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi.
Aidha, amesema baada ya hatua hizo
za kisera kuchukuliwa na Serikali, baadhi ya benki za biashara hapa
nchini zimeanza kupunguza riba za mikopo.
Ameongeza kuwa, Serikali
itaendelea kuchukua hatua za kisera ili kuhakikisha kuwa riba za mikopo
katika soko zinaendelea kupungua.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni