Kijana Frank Japhet (23), mkazi wa Mbezi, Dar es Salaam, amelazimika
kujisalimisha katika Kituo cha Polisi Mlandizi, Kibaha, Pwani, baada ya
mzigo wa mahindi unaokadiriwa kuwa na uzito wa kilogramu 20, anaodaiwa
kuuiba kung’ang’ania mabegani.
Wakati akihojiwa kituoni hapo, mtuhumuwa huyo amesema mzigo huo,
uliofungwa kwenye kiroba aliuiba kwa mama mmoja eneo la Mtaa wa
Nyambwiro, Mlandizi, Kibaha, mkoani Pwani majira ya saa 7.00 usiku wa
kuamkia leo Mei 3, 2018, akaongeza kwamba aliondoka na mzigo huo hadi
eneo la Stendi ya Mlandizi alipokuwa auache kwa mwenzake ili arudie
mzigo mwingine, ambapo mzigo huo uling’ang’ania kichwani.
Ameendelea kusema kwamba alijitahidi kufanya kila aliloweza ili mzigo
huo utoke kichwani ikiwa ni pamoja na kulala ili akinyanyuka ubaki chini
lakini aliponyanyuka, alinyanyuka nao kichwani! Baada ya kuzunguka nao
kwa muda mrefu, alidai alichoka hivyo akalazimika kujisalimisha polisi
ili asije akauawa na raia wenye hasira watakapobaini kuwa ni mwizi.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani Jonathan Shanna amesema walilazimika
kumtafuta mhusika wa mzigo huo ili kuweza kumsaidia kijana Frank Joseph
ambaye aliiba kiroba hicho, baada ya wao kushindwa kumtua.
Kamanda Shanna ameendelea kusimulia kuwa wakati wakijaribu kumtua kijana
huyo kiroba cha mahindi alichoiba alikuwa akilalamika kupata maumivu
makali, na ndipo wakamsaka mmiliki wa mzigo ili kumsaidia.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni