Na Mwashungi Tahir-Maelezo Zanzibar
30-5-2018
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Haroun Ali Suleiman, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na Serikali za Falme za Kiarabu katika kuleta maendeleo zaidi nchini.
Akizungumza na Waziri wa masuala ya kiislam na mihadhara ya kidini kutoka falme za kiarabu Sheikh Saleh bin Abdulaziz Al Sheikh ofisini kwake Mazizini mjini Zanzibar, amesema Zanzibar na Saudi Arabia zina ushirikiano wa muda mrefu unaostahili kuendelezwa.
Ameahidi kuwa serikali ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Saudia kwa lengo la kuimarisha sekta za maendeleo na huduma za kijamii.
Kwa upande wake, Waziri Saleh Abdulaziz alieleza kufurahishwa na mapokezi mazuri wanayoyapata wakati wanapofika nchini Zanzibar na Tanzania Bara akisema jambo hilo ni kielelezo cha uhusiano na mapenzi yaliyopo kati ya nchi zao.
Alisema ushirikiano uliopo baina ya nchi mbili hizo, umesaidia kukuza udugu na upendo kwa kufanya mambo mengi ya maendeleo hapa nchini na hivyo kuimarisha uchumi, elimu, afya na huduma nyengine za kijamii.
“Nimefarijika zaidi kuona miradi tunayoileta nchini inaendelezwa, na ninaahidi kuwa tutaleta miradi mingine mizuri zaidi ili kustawisha hali za wananchi wa Zanzibar na kuimarisha udugu, na uhusiano wetu,” alisema Waziri huyo.
Aliongeza kuwa, lengo kuu la ziara hiyo ni kuendeleza mshikamano pamoja na mpango wa Serikali ya Saudia Arabia kukuza miradi ikiwemo kujenga misikiti hapa Zanzibar.
Aidha alisema nchi yake itaendelea kutoa nafasi za masomo ya elimu ya juu kwa wanafunzi wa Zanzibar katika mji wa Madina ili kukuza uelewa wao katika fani ya dini ya kiislam.
Waziri huyo alimpongeza Mufti Mkuu wa Zanzibar pamoja na Kadhi, kwa namna wanavyosimamia vyema utaratibu wa kusafirisha mahujaji wa Zanzibar wanaokwenda mjini Makka kutekeleza ibada ya Hijja, na kusifu utulivu wa mahujaji wa hapa wanapokuwa huko katika msimu wa ibada hiyo.
Waziri huyo ameahidi kukuza umoja, mshikamano na maelewano mazuri baina ya serikali ya nchi yake na Mufti Mkuu wa Zanzibar ili kuendeleza shughuli za kuinua uisilamu nchini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni