WADAU USALAMA BARABARA WAMPONGEZA RAIS MAGUFULI MATUKIO YA AJALI


Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake nchini (TAMWA), Bi. Edda Sanga (katikati) ambaye ni mmoja wa wadau kutoka Asasi za kiraia unaotetea marekebisho ya sheria na sera ihusuyo usalama barabarani Tanzania akizungumza na vyombo vya habari kutoa tamko la kumpongeza na kumuunga mkono Rais John Magufuli kwa hatua anazochukua kudhibiti matukio ya ajali za barabarani.
Mkutano wa Wanahabari na wadau kutoka Asasi za kiraia unaotetea marekebisho ya sheria na sera ihusuyo usalama barabarani Tanzania ukiendelea leo jijini Dar es Salaam.
Program Ofisa wa TAMWA, Edson Sosten (kushoto) akizungumza na wanahabari kuelezea mafanikio na hatua zinazochukuliwa na mtandao wa Asasi za kiraia unaotetea marekebisho ya sheria na sera ihusuyo usalama barabarani Tanzania kudhibiti ajali za barabarani.

MTANDAO wa wadau kutoka Asasi za kiraia unaotetea marekebisho ya sheria na sera ihusuyo usalama barabarani Tanzania, umetoa kauli ya kumpongeza na kumuunga mkono Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli kwa kuguswa na kutoa maagizo mara kadhaa kunapotokea ajali za barabarani ambazo zimekuwa na athari nyingi kiuchumi na kijamii.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam kwa niaba ya asasi hizo, Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake nchini (TAMWA), Bi. Edda Sanga alisema matukio hayo ya ajali za barabarani yamekuwa yakiwasababishia wananchi madhara makubwa yakiwemo kupoteza maisha, majeraha makubwa, ulemavu wa kudumu, mali kuharibika ikiwa ni pamoja na kuacha familia nyingi zikiwa tegemezi baada ya kuondokewa na watu wanaowategemea.

Alisema taasisi hizo zinaunga mkono kauli ya Rais aliyoitoa hivi karibuni ambapo alitoa maagizo kwa vyombo vya usalama barabarani kufanya uchunguzi wa kina wa ajali iliyotokea katika kijiji cha Makomero, Wilaya ya Igunga Mkoani Tabora Aprili 4, 2018. Ajali hiyo ilitokea usiku na kusababisha vifo vya watu 12 baada ya basi la City Boy la kutoka Karagwe kuelekea Dar es Salaam kugongana uso kwa uso na lori aina ya Fuso lililokuwa linatoka Singida.

“Aidha, nalitaka Jeshi la Polisi, Kamati za ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya na Mamlaka zote zinazohusika na usalama Barabarani kujitathimini, na kutafuta majawabu ya kwa nini ajali za barabarani zinaendelea kutokea kwa kusababishwa na uzembe na uvunjaji wa sheria za barabarani”. alinukuu tarifa ya maagizo ya Rais Magufuli aliyoitoa baada ya ajali hiyo.

"Pamoja na agizo la Mheshimiwa Rais, la kuvitaka vyombo vya ulinzi na usalama barabarani na mamlaka yake kutafuta majawabu kwa nini ajali zinaenaendelea kutokea nchini, sisi kama Taasisi za Kiraia kwa muda sasa tumekuwa pia tukijiuliza swali kwa nini ajali za barabarani zimeendelea kutokea nchini?. Baada ya tathimini na tafiti mbalimbali tulipata jawabu kwamba, kuna haja ya kufanyia tena mapitio na kuboresha Sheria yetu ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973".

Alisema sheria hiyo imejitahidi kwa kiasi kikubwa kukabiliana na changamoto za usalama barabarani isipokuwa utafiti uliofanyika unaonesha kuna mapungufu kadha wa kadha ambayo yanahitaji kufanyiwa maboresho ili yaendane na hali ya sasa na pia iweze kukabiliana kikamilifu na changamoto za ajali za barabarani pamoja na madhara yatokanayo na ajali hizo.

Alizitaja sheria ambayo wamependekeza kufanyiwa kazi ni pamoja na; mwendokasi, matumizi ya mikanda, kofia ngumu, matumizi ya vilevi na vizuizi vya watoto.

"...Mwendo kasi (Speeding): Mwendokasi ndio unatajwa kuwa ndio chanzo kikuu cha ajali- “the faster the speed the greater impact in the crush”. Kifungu cha 51(8) cha Sheria yetu ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973 inatamka mwendokasi maeneo ya makazi ni 50km/h, kwa maeneo mengine utadhibitiwa na alama za barabarani, na magari makubwa zaidi ya tani 3500 hayatazidisha 80km/h.

"Mapungufu ya sheria ni kwamba inatambua maeneo machache katika kuzuia mwendokasi. Tunapendekeza kuwa sheria itamke maeneo yote na si yale ya mjini tu/makazi, itamke wazi kuhusu maeneo ya shule, nyumba za ibada, maeneo ya michezo na mbuga za wanyama," alisisitiza Bi. Sanga.

Asasi zilizoshirikiana kumpongeza na kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli ni pamoja na TAWLA, TAMWA, WLAC, TCRF, TLS, TMF, RSA, AMEND TANZANIA, SHIVYAWATA, TABOA na SAFE SPEED FOUNDATION.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni