DK. KIGWANGALLA AITAKA KAMATI INAYOCHUNGUZA TUHUMA ZA MAUAJI YA TEMBO KATIKA IKOLOJIA YA RUGWA-RUAHA KUTENDA HAKI


Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk.Hamisi Kigwangalla akisalimiana na Kamanda wa Polisi Mstaafu wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova ambaye ni Mwenyekiti wa kamati inayochunguza tuhuma za mauaji ya tembo katika Ikolojia ya Rugwa-Ruaha ambazo zilitolewa hivi karibuni na kituo cha habari cha ITV LONDON cha nchini Uingereza, alipokutana na kamati hiyo leo ofisini kwake mjini Dodoma. Wengine pichani ni wajumbe wa kamati hiyo.

Na Hamza Temba-Dodoma
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla ameitaka kamati inayochunguza tuhuma za mauaji ya tembo katika Ikolojia ya Rugwa-Ruaha ambazo zilitolewa mwishoni mwa mwaka jana na kituo cha habari cha ITV London cha Uingereza kufanya kazi hiyo kwa uaminifu na uadilifu mkubwa bila kumuonea mtu ili ukweli ubainike na Serikali iweze kuchukua hatua stahiki.

Dkt. Kigwangalla ametoa rai hiyo leo mjini Dodoma alipokutana na wajumbe wa kamati hiyo ambayo imewasilisha taarifa za awali za kazi ilizoanza kuzifanya za kupitia taarifa mbalimbali kuhusu tuhuma hizo kabla ya kwenda kuzifanyia uchunguzi maeneo husika.

Amewataka wajumbe hao kuchunguza ukweli wa tuhuma hizo ili kubaini kama kweli kuna watumishi wa Wizara waliohusika katika mauaji hayo pamoja na tuhuma kuwa mauaji ya tembo yalikuwa ni makubwa kama ilivyoripotiwa na chombo hicho cha habari.

Dkt. Kigwangalla pia ameitaka kamati hiyo kuchunguza ukweli wa tuhuma kuwa fedha za ufadhili wa mradi wa SPANEST zilizotolewa na Shirika la Maendeleo ya Umoja wa Mataifa (UNDP) zilitumika vibaya kufadhili mauaji hayo kama ilivyoripotiwa na chombo hicho cha habari.

“Msimtafute mtu, wala msimuonee mtu, fanyeni kazi hii kwa uadilifu na uaminifu mkubwa ukweli ujulikane ili sisi kama Serikali tuweze kuchukua uamuzi unaostahili” alisema Dkt. Kigwangalla.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye ni Kamanda wa Polisi Mstaafu wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova amesema kamati yake itafanya kazi kwa uaminifu na weledi wa hali ya juu na kuleta taarifa za ukweli na mapendekezo yatakayoisaidia Serikali kufanya maamuzi sahihi kuhusu tuhuma hizo.

Mapema mwezi Januari mwaka huu, Waziri Kigwangalla na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Natalie Boucly wakiwa katika ofisi ndogo ya wizara hiyo jijini Dar es Salaam walikubaliana kuunda kamati ya pamoja kuchunguza tuhuma hizo.

Kamati hiyo iliyoundwa mapema mwezi januari mwaka huu inajumuisha wajumbe tisa wakiwemo wawili kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na wajumbe wengine kutoka taasisi mbalimbali za Serikali.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk.Hamisi Kigwangalla akisalimiana na Ndugu Robert Mande ambaye ni mjumbe wa Kamati hiyo kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii.Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk.Hamisi Kigwangalla akisalimiana na Bi. Getrude Lyatuu ambaye ni mjumbe wa Kamati hiyo kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk.Hamisi Kigwangalla akisalimiana na wajumbe wa kamati inayochunguza tuhuma za mauaji ya tembo katika Ikolojia ya Rugwa-Ruaha ambazo zilitolewa hivi karibuni na kituo cha habari cha ITV LONDON cha nchini Uingereza, alipokutana na kamati hiyo leo ofisini kwake mjini Dodoma.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni