AfDB YARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA NISHATI YA UMEME INAYOFADHILIWA NA BENKI HIYO NCHINI


Na Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB,  Dkt. Akinumwi  Adesina, amesema Benki hiyo imeridhishwa na utekelzaji wa miradi ya nishati hapa nchini kwani inachochea mageuzi katika maisha ya wananchi .
 Akizungumza mara baada ya kuwasili Mkoani Dodoma na kutembelea  kituo cha kupoza umeme cha Zuzu, mkoani Dodoma, amesema kuwa  benki hiyo inatambua na kupongeza juhudi za  Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika kusukuma mbele kurudumu la maendeleo.
Dkt. Adesina ameeleza kuwa ujenzi wa kituo hicho cha kupoza umeme ni mkakati wa Serikali ya Awamu ya Tano ya kuondoa changamoto ya upatikanaji wa nishati ya umeme kwa wananchi wake na umelenga pia kupunguza tatizo la upatikanaji wa umeme katika nchi jirani zinazopakana na Tanzania ikiwemo Burundi na Kenya.
Alisema kuwa katika kuhakikisha mpango huo wa kupeleka umeme huo na kuunganisha na nchi jirani, Benki yake imetoa kiasi cha dola za Marekani milioni 75 kufanikisha mradi huo wenye thamani ya zaidi ya dola milioni 220.
"Umeme ni jambo muhimu sana katika maendeleo ni sawa na damu katika mwili wa binadamu, ukiwa na damu mwilini unakuwa na hai kama huna unakufa! kwa hiyo uchumi bila umeme wa uhakika hauwezi kushamiri" alisisitiza Dkt. Adesina
Aliahidi kuwa Benki yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kukuza maendeleo ambapo hivi sasa Benki yake iko katika mazungumzo na Serikali ili mkopo nafuu wa dola za Marekani milioni 165 uweze kupatikana kwa ajili ya kujenga mradi wa nishati ya umeme katika ukanda wa Kaskazini Magharibi mwa nchi.
"Vile vile tutawasilisha kwenye Bodi ya Wakurugenzi wa Benki yetu ili kiasi cha dola za Marekani milioni 45 kinachoombwa na Serikali kwa ajili ya kujenga mradi wa umeme unaotokana na joto ardhi uweze kupatikana ili kuboresha na kuwa na umeme wa uhakika nchini kwa ajili ya kusukuma maendeleo ya viwanda nchini" alisema Dkt. Adesina
Alisema kuwa kwa ujumla Benki yake katika kipindi cha miaka miwili ijayo (2018/2019 na 2019/2020) Benki yake itatoa kiasi cha dola za Marekani bilioni 1.5 katika sekta ya umeme na kueleza matumaini yake kwamba hatua hiyo itawawezesha wazalishaji mali wadogo, wa kati na wakubwa kuzalisha bidhaa na mali mbalimbali na hivyo kukuza uchumi wao na wa Taifa kwa ujumla.
Kituo cha kupoza umeme zuzu ni sehemu ya mradi wa umeme unaonufaisha mikoa ya Iringa, Dodoma, Singida na Shinyanga ambapo vijiji zaidi ya 121 vimeshanufaika na maradi huo   wa uzalishaji na usambazaji wa umeme kwa mikoa husika.
Alisema kuwa miradi inayoendelea hivi sasa nchini Tanzania kupitia ufadhili wa Benki yake imefikia thamani ya zaidi ya dola za Marekani bilioni 2 ambapo uwekezaji mkubwa uko katika sekta za nishati ya umeme, usafiri, miundombinu ya barabara, kilimo, maji na usafi wa mazingira, kusaidia Bajeti Kuu ya Serikali pamoja na uendelezaji wa rasilimali watu.
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amesema kuwa Serikali ya Tanzania inashukuru kuwa Benki ya Maendeleo ya Afrika ni mshirika mkubwa wa Maendeleo wa Tanzania kutokana na kusaidia Serikali katika uwekezaji mkubwa unaogusa  nyanja mbalimbali ikiwemo nishati na miundo mbinu mingine kama barabara.
Aliongeza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Benki hiyo katika kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli kwa kuwa hiyo ndio dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nishati Mhe.  Subira Mgalu amesema kuwa Benki hiyo ni mshirika wa kweli katika sekta ya nishati na imewezesha kufanikiwa kwa miradi mbalimbali ya umeme ukiwemo ule unaoinifaisha mikoa ya Iringa, Singida, Dodoma, Shinyanga na Dodoma.
Miradi inayotekelezwa hapa nchini kwa sasa  kupitia ufadhili wa Benki ya AfDB imefikia  zaidi ya dola za Marekani bilioni 2 ambapo uwekezaji mkubwa uko katika sekta za nishati ya umeme, usafiri, miundombinu ya barabara, kilimo, maji na usafi wa mazingira, kusaidia Bajeti Kuu ya Serikali pamoja na uendelezaji wa rasilimali watu.
Ushirikiano wa AfDB na Tanzania ulianza tangu mwaka 1971 na mpaka sasa benki hiyo imeipatia Tanzania kiasi cha dola za Marekani bilioni 3.6, karibu shilingi trilioni 8 za Tanzania.
 Rais wa AfDB  yuko nchini kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kwa mwaliko wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
 Naibu Waziri wa  Nishati Mhe. Subira Mgalu akisalimiana na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt.  Akinumwi Adesina mara baada ya kuwasili mjini Dodoma ambapo alitembelea na kukagua mradi wa kituo cha kupoza umeme  cha zuzu mkoani humo .
 Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip  Isdori  Mpango ( Mb)  akimuongoza   Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt.  Akinumwi Adesina mara baada ya kuwasili mjini  Dodoma ambapo alitembelea na kukagua mradi wa kituo cha kupoza umeme  cha zuzu mkoani humo.
 Rais wa wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt.  Akinumwi Adesina akisalimiana na Mhandisi  Peter  Kigadi mara baada ya kuwasili mjini Dodoma ambapo alitembelea na kukagua mradi wa kituo cha kupoza umeme  cha Zuzu mkoani humo .
 Rais wa wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt.  Akinumwi Adesina akisisisitiza jinsi Benki hiyo inavyoridhishwa na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa nishati hali itakayochochea maendeleo.
 Mhandisi Mkuu wa Kituo cha kupoza umeme cha Zuzu, Mkoani Dodoma Bw. Joseph Mongi akitoa maelezo kuhusu namna kituo hicho kinavyofanya kazi wakati wa ziara ya Rais  wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt.  Akinumwi Adesina katika kituo hicho.
 Sehemu ya Miundombinu ya kituo cha kupoza umeme cha Zuzu kilichoko mkoani Dodoma kama inavyoonekana.
 Rais wa wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt.  Akinumwi Adesina akiwa kwenye picha ya pamoja na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdori Mpango (Mb) na Naibu Waziri wa Nishati  Mhe. Subira Mgalu.
 Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip  Isdori  Mpango (Mb)   na Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Subira Mgalu,  wakimuongoza    Rais wa wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt.  Akinumwi Adesina kukagua miundombinu ya Kituo cha kupoza umeme cha Zuzu, mjini Dodoma.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano-Wizara ya Fedha na Mipango)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni