VIJANA WENGI WAMEJAA TAARIFA BADALA YA MAARIFA-JANUARY

*Ahimiza vijana kusaka maarifa kwa nguvu zote ili wawe viongozi bora
*Ataka wazee kurithisha vijana yale yaliyofanywa na Mwalimu Nyerere

Na Said Mwishehe ,Globu ya jamii

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira katika Serikali ya Awamu ya Tano Januari Makamba amesema vijana wengi nchini kwa sasa wamejaa taarifa badala ya 
maarifa.

Hivyo amesema ili vijana wawe viongozi bora na wanzuri kwa Taifa letu ni vema wakafanya juhudi na kuhakikisha wanapata maarifa ambayo yatakuwa dira na muelekeo kwa nchi yetu.January amesema hayo leo wakati wa Kongamabo la Kumbukizi ya Mwalimu Julius Nyerere ambayo imefanyika katika Chuo cha Kumbukumbu cha Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaa. 

Mada kuu kwenye kongamano inasema Kuelekea uchumi wa kati mchango wa Mwalimu Nyerere kuhusu amani,umoja wa kitaifa na uwajibikaji.Amesema yeye kama viongozi kijana ametumia kongamano hilo muhimu kuhusu mchango wa Mwalimu Nyerere katika ujenzi wa taifa hili na kwa sehemu kubwa aliongoza kwa maarifa makubwa na yenye tija kwa nchi yetu.

Hivyo amesema kwa vijana wote wa Tanzania hasa wanaotaka kuwa viongozi ni vema wakajikita kitafuta maarifa zaidi badala ya kujaza taarifa vichwani ambazo nyingine hazina tija.

"Taarifa inakuwezesha tu kuwa mzuri kwenye mazungunzo katika vijiwe vya kahawa na katika kupiga soga.Lakini ukiwa na maarifa yatakufanya kijana kuwa kiongozi bora kwa nchi yetu.Nimebahatika kwenda Butiama na nilipofika nilifanikiwa kuingia maktaba yake Mwalimu, utaona namna ambavyo 
amesoma vitabu vingi sana ili kuwa na maarifa mapana kwa ajili ya kuliongoza vema taifa letu,"amesema January.

Ametoa mwito kwa vijana nchini kuhakikisha wanatumia muda mwingi kusaka maarifa badala ya taarifa na kuongeza Mwalimu Nyerere alifika Dar es Salaam akiwa na umri wa miaka 32 lakini kutokana na maarifa yake wazee walimuamini na akawa Rais wa Tanu.

Amefafanua kwa bahati mbaya kwenye mitandao ya kijamii kwa sehemu kubwa vijana wanaangalia zaidi mambo ambayo hayana maana na kutoa mifano kwa kueleza wengi wanaangalia taarifa za wasanii."Nenda kwenye youtub kisha angalia hotuba za Mwalimu Nyerere ambayo zinazungumzia mambo mapana ya nchi yametazamwa na watu ngapi.

Kisha angalia mambo yanayohusu wasanii yametazamwa 
na watu wakangapi.Utaona taarifa za wasanii zinaangaliwa zaidi kuliko hotuba za Mwalimu ambazo ni muhimu kuangaliwa na kila kijana,"amesema.

Pia amesema vijana waliofanya kazi na Mwalimu Nyerere wametimiza wajibu wao kwa kuhakikisha wanajenga nchini na kuweka misingi imara ya umoja na mshikamano, hivyo swali ambalo vijana wa sasa wamepanga kufanya nini kwa ajili ya nchi yetu.Amefafanua Mwalimu Nyerere wakati wa uhai amewahi kutoa hutuba ambayo alizungumzia kuanza kuona nyufa,hivyo vijana waliopo leo lazima watafakari nyufa hizo bado zipo na nini wanafanya kiziziba.

Kuhusu umuhimu wa kukumbukizi ya Mwalimu ,January amesema ni muhimu kuwa na kongamano hilo kwani linatoa nafasi kwa vijana kufahamu Mwalimu Nyerere alifanya nini kwa ajili ya Taifa letu.
Baadhi ya wageni waalikwa na wanafunzi wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu kilichopo Kigamboni jijini Dar es Salaam wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi kwenye Kongamano la Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere January Makamba(hayupo pichani) leo.
Mgeni rasmi kwenye Kongamano la Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere January Makamba akiwa kwenye picha ya pamoja na wageni waalikwa na viongozi wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere baada ya kufungua rasmi kongamano hilo ambalo lilikuwa na mada mbalimbali. kongamano hilo limefanyika leo chuoni hapo

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni