Baada ya miongo kadhaa ya minong´ono, uchunguzi na kesi
kufuatiliwa kwa karibu, huenda msanii wa Kimarekani Bill Cosby
akaelekea gerezani akiwa na umri wa miaka 80 kwa makosa ya udhalilishaji
wa kingono.
Msanii huyo wa vichekesho alipatikana na hatia siku ya Alhamisi yya
kumpa dawa za kulevya na kumdhalilisha kingono mfanyikazi wa Chuo Kikuu
cha Temple Andrea Constand katika makazi yake yaliyoko Philadelphia
mwezi Januari, 2004.
Wanasheria wanawake wameutaja uamuzi huo
kuwa wa kihistoria. Vuguvugu kwenye mitandao lenye jina #MeToo,
limethibitisha kuwa waliokuwa wakimtuhumu Cosby siku zote hawakuwa na
makosa: Haiba yake ya uungwana sasa imevurugwa .
Lili Bernard,
aliyesema kuwa Cosby alimdhalilisha kingono kabla ya kumpa nafasi katika
kipindi chake maarufu cha "The Cosby Show" mwaka 1992, alijawa na jazba
katika mahakama kiasi cha kugonga kichwa chake bila ya kukusudia kwenye
meza iliyokuwa mbele yake.
"Nimezidiwa na furaha, alisema Bernard nje ya mahakama huku akidondokwa na machozi." Je, nimeamka? Huu ni muujiza."
Zaidi ya wanawake 60 wamelalama kuhusu Cosby
Uamuzi
huo, wa kwanza unaomhusisha msanii anayetambulika katika kipindi cha
#MeToo, inahujumu sifa za msanii mkubwa aliyevuka mipaka ya rangi
katika jukwaa la kuigiza la Hollywood na kubobea kwenye Televisheni .
Ni
moja ya kesi iliotokana na visa vilivyowakumbuka zaidi ya wanawake 60
waliodai kuwa Cosby aliwapa dawa za kuelevya na kisha kuwadhalilisha
kingono kwa kipindi cha miongo mitano, lakini ambao kadhia zao
hazikuaminika ama zilipuuzwa kabla ya kuanza kampeni kwenye mitandao ya
kijamii yenye anwani #MeToo iliyoangazia dhulma za kingono
zilizotekelezwa na wanaume wenye ushawishi mkubwa katika jamii.
Cosby
alitumbua macho maelezo ya jaji yakisomwa, lakini baadaye akapaza sauti
akimpinga jaji Kevin Steele baada ya mwendesha mashtaka kutaka Cosby
apelekwe gerezani mara moja.
Mwendesha mashtaka aliambia mahakama
kuwa Cosby ana ndege ya kibinafsi na huenda akiachiliwa akatoroka.
Cosby alikanusha kwa hasira kuwa anamiliki ndege na kumtusi mwendesha
mashtaka .
Cosby alishtakiwa kwa makosa matatu ya udhalilishaji
wa kingono, kila moja likiwa na kifungo cha kati ya miaka mitano hadi 10
gerezani.
Mashtaka hayo huenda yakajumlishwa ama kuunganishwa
kwa ajili ya hukumu, lakini ikizingatiwa umri wa Cosby, kifungo chochote
kinamaana kuwa huenda akafia gerezani.
Cosby amesema kuwa atakata rufaa
Utekelezaji
wa kifungo chake huenda ukafanyika katika kipindi cha miezi mitatu.
Kabla ya hayo Cosby lazima afanyiwe uchunguzi kuthibitisha iwapo kuwa ni
mtumiaji wa nguvu wa dhulma za kingono. Aidha atajiandikisha kuwa
mkosaji wa kingono kwa kuzingatia sheria za Megan.
Jopo la wanaume saba na wanawake watano lilishauriana kwa muda wa masaa 14 kabla ya kutoa uamuzi dhidi ya Cosby.
Constand-
45, mfanyikazi wa Chuo Kikuu cha Temple, alisema Cosby alimlemaza kwa
kumpa tembe tatu kisha akakosa fahamu, kisha akamdhalilisha kingono kwa
kutumia vidole vyake alipokuwa amelala hana nguvu za kukubali ama
kukataa. Cosby anadai kuwa kitendo hicho kiliafikiwa na wote.
Cosby
aliupungia mkono umati ambao ulikuwa nje ya mahakama na kuingia kwenye
gari lake na kuondoka bila ya kusema chochote. Wakili wake Tom Mesereau
alitangaza, "vita havijakamilika" na kusema kuwa atakata rufaa.
Mawakili
wa upande Cosby wakiongozwa na Mesereau, aliyeshinda kesi dhidi ya
Michael Jackson kuhusu kuwadhalilisha watoto kingono, walishambulia
Constand wakati wa kesi hiyo huku wakimuita muongo ambaye alimsingizia
Cosby kwa lengo la kutaka kuwa tajiri.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni